Kumbukumbu kutoka kitabu cha TUJIFUNZE LUGHA YETU! Kitabu cha darasa la nne. Wengi natumaini mnakumbuka, binafsi nimekumbuka na nimefurahi sana. Binafsi nimekumbuka na nimefurahi sana soma ufaidi au ukumbuke pia:-)
Kusala ni mtoto wa Songea. Anasoma shule ya Lilambo. Ana mjomba wake, anafanya kazi jiji la Dar es Salaam, ambao ni mji mkuu wa Tanzania. Ni karani wa bandari.
Wakati wa likizo, Kusala alikwenda Dar es Salaam kumsalimu mjomba wake. Alichukua sanduku lake la mbao na kifurushi cha chakula, akaenda mpaka mjini Songea. Kesho yake akaondoka kwa basi kwenda Dar es Salaam.
Basi hili lilipitia njia ya nNjombe. Jioni likafika Iringa. Hapa wakalala. Asubuhi yake wakaanza safari kwenda Morogoro kupitia Mikumi. Mikumi ni mbuga ya wanyama.
KUsala aliona wanyama wengi. Kutoka hapo walikwenda moja kwa moja mpaka Morogoro ambako walifika kama saa kumi jioni. Baada ya kupumzika kidogo waliondoka kuelekea Dar es Salaam.
Walipokaribia Dar es Salaam, Kusala aliona majengo makubwa upande wa kushoto. Alimwuuliza mwenzake aliyekuwa karibu naye, ”Yale ni majumba gani?” Mwenzake akamjibu, ”Yale ni majengo ya Chuo Kikuu. Ni mahali maarufu sana hapa nchini.” Kusala akauliza tena, ”Je? Wapo watoto ?” Akajibiwa, “La, wasommao pale si watoto. Ni watu wazima.” Akaendelea kuuliza, “Wanasomea mpaka madarasa gani?” Akajibiwa tena, “Hawana madarasa. Wanasomea shahada za elimu mbalimbali.”
Walipofika katikati ya mji, Kusala alishangaa sana kuona taa zenye rangi mbalimbali. Taa hizo zilitundikwa juu ya milingoti mirefu ya chuma. Aliona magari makubwa, mabasi mengi na motokaa ndogo nyingi. Alishangaa sana kuona magari mengi hivi. Wakati wote huu alikuwa na wasiwasi. Hakujua atakalofanya ikiwa hatamkuta mjomba wake kituoni. Basi lilipofika kituoni alifurahi sana kumwona mjomba wake amekuja kumpokea. Usiku ule Kusala alilala sana kwa ajili ya uchovu wa safari.
Asubuhi yake Jumapili, mjomba wake aliwachukua yeye na binamu yake, Njoli, akawatembeza mjini. Kwanza walitembelea kiwanje cha ndege. Kusala alishangaa kuona jinsi kiwanja kilivyo kikubwa. Aliona ndege kubwa zikitua, akauliza, “Mbona Songea hakuna ndege kubwa kama hizi?” Mjomba wake akamjibu, “Songea ni mji mdogo. Hauna kiwanja kikubwa cha kutua ndege kubwa kama hizi.”
Kutoka kiwanjani Kusala alipelekwa kutazama Jengo la Bunge. Mjomba wake alimweleza kuwa humo Wabunge hukutana na kupanga mipango ya Serikali na maendeleo ya nchi. Baada ya hapo walikwenda kwenye kivuko cha bahari kupitia Ikulu. Hapo Ikulu, Kusala aliona askari walinzi. Pia aliona mbuni, tausi na kudu. Kusala akauliza, “Askari hawa wanafanya nini?” Njoli akamjibu, “Wanalinda zamu. Hapa ndipo Ikulu.” Kusala akauliza tena, “Ikulu ni nini?” Mjomba wake akamwambia, “Ni makao rasmi ya Mtukufu Rais wetu.
Walipofika kwenye kivuko walikata tikiti wakaingia katika pantoni na kuvuka mpaka ngámbo. Huko walitembelea mtambo wa kusafisha mafuta. Mtambo huu husafisha na kutenganisha lami, dizeli, mafuta ya taa na petroli.
Waliporudi walikwenda bandarini. Mjomba wake akawaonyesha ghala kubwa na mshine za kuinulia mizigo. Pia waliona meli nyingi kubwa kwenye magudi. Zilikuwa zikipakua na kupakia bidhaa. Pia yalikuwapo madau pamoja na mitumbwa. Wavuvi hutumia madau na mitumbwa kuvulia samaki.
Kusaka vilevile alitembezwa kuona stesheni kubwa ya gari la moshi. Hii ilikuwa mara yake ya kwanza kuona gari la moshi. Alishtuka aliposikia makelele na kuona moshi mwingi. Watu wengi walikuwa wakingojea gari liondoke.
Siku nyingine Kusala alipelekwa kuona viwanda. Aliona watu wengi wakifanya kazi. Kusala na Njoli waliona viwanda vya kutengeneza nguo, mablanketi, sufuria na madebe. Walipofika Ubongo, alistaajabu kuona watu wengi wamesimama msululu nje ya kiwanda cha kutengeneza nguo. Kusala akauliza, “Hawa wanafanya nini?” Mjomba wake akamjibu, “Watu hawa wanatafuta kazi. Ni wageni mjini. Wameshindwa kukaa vijijini” Kusala alihuzunika sana, akamwambia mjomba wake, “mimi napendelea kuishi kijijini kwetu. Vijijini hakuna haja ya kusimama msululu kutafuta kazi. Maana kazi za shamba ni nyingi. Nitakapomaliza masomo yangu nitaanza kulima na kufuga kuku. Mimi sipendi kukaa mjini bila kazi.”
Kutoka Ubungo walipitia Kariokoo. Hili ni soko kubwa la Dar es Salaam. Vyakula na matunda mengi huuzwa hapo. Biashara nyingi huendeshwa katika maduka makubwa karibu na soko hilo. Kusala alisikia muziki wa redio ukiwastarehesha wauzaji na wanunuzi.
Kwa kweli, Kusala aliona mambo mengi mageni. Aliona watu wakikimbilia mabasi. Wengine wakienda mbio kwa miguu. Siku ya mwisho alitembelea kiwanda cha kutengeneza nyama za makopo. Alipoondoka alimshukuru sana mjomba na ndugu zake. Alipofika Songea aliwaandikia barua ya kuwashukuru na kusema kuwa alifurahi sana kuona jiji la Dar es Salaam.
Hivi ulifikiria nini kutuwekea hii hadithi hapa.
ReplyDeleteYaani umenikumbusha mbali sana leo.
Nimekumbuka hadithi nyingi tulizokuwa tunazisoma kwenye vitabu vya kiswahili wakati ule.
hadithi kama, Kapulya mdadisi, Brown ashika tama, siku ya gulio Katarero, Kibanga ampiga mkoloni, naikumbuka sana hadithi hii kwani niliwahi kupewa jina la Kibanga baada ya kumpiga mtoto wa kiarabu tuliyekuwa tukisoma nae wakati huo nadhani nilikuwa darasa la tatu kama sikosei.(Lakini ilikuwa ni utoto tu msije mkani Criticise)
Hadithi nyingine ni kama vile, Nunda mla watu, Sizitaki mbichi hizi, hii imeacha msemo ambao unatumika mpaka leo, asiyesikia la mkuu, Fikiri mimi masikini, Mweka nadhiri na shetani, Zimwi likujualo.
halafu kuna vile vitabu vya Darubini nadhani vinaitwa ujinga wa mwafrika, anayekumbuka atanikumbusha, zilikuwepo hadithi kama, Urembo wa Ndonya, hii nadhani inawagusa wanawake zaidi kutokana na kujiremba kwao, zingine ni, Kawambwa na kapu la Karanga, Chai ya Mzungu, na nyingine nimezisahau, jamani naomba mnikumbushe!!!!!
Alaa kumbe! Kusala alitokea Songea.
ReplyDeleteLeo mambo yamebadilika. Yale majengo marefu upande wa kushoto hayapo karibu na Dar es Salaam, bali yapo Dar kabisa, mji umepanuka sana. Pale bado ni maarufu sana, ila siku hizi ni maarufu sana kwa migomo na maandamano. Kusala, unataka kujua kwa nini? Serikali inawayeyusha wanafunzi.
Kiwanda cha kusafisha mafuta TIPER sina hakika nacho kwa sasa. Magari moshi bado yanachapa mzigo kama kawa TZR na TRL.
Ama kweli vitabu vile vilileta hamasa nyingi. Kama hukuwahi kukanyaga Dar, ulikuwa ukipata shauku kubwa. Utaandika barua nyingi kwa kina mjomba, shangazi na wengineo kuomba wakuzingatie wakati wa likizo.
Sina hakika kama vitabu wanavyosoma sasa vimejaa misisimuko tena. Hapa juzi kati kuna mabwana ubinafsishaji waliivuruga vuruga mitaala ya elimu..
Ahsante da Yasinta, umenifanya niwakumbuke marafiki zangu enzi hizo, wachache bado nawasiliana nao.
Kazi nzuri, lazima kila mtu aisome. Kumbe Songea mpo juu.
Markus upo? We hukwenda Dar wakati wa likizo?
Unatabasamu nini?
Asante kwa kumbukumbu Nzuri!
ReplyDeletenitafute nina ujumbe wako dada yangu..edondaki@yahoo.com or +358408709619
ReplyDeleteDah! Kweli walisema "you never miss your water, till your well runs dry"
ReplyDeleteNimekumbuka sana "wakati huo"
Asante Yasinta