Sunday, June 29, 2008

JUNI 29,2008 Upendo

Leo nimekumbuka sana nilipokuwa msichana mdogo au nisema miaka 18-20 kama hivi nilipatwa na mtihani mkubwa sana kama wasichana wote, yaani kumchagua nani atakuwa mume wangu katika maisha yangu. Eeeh ndugu zanguni ilikuwa kasheshe sana maana kila kijana aliyekuja wazazi wangu walisema hafaii. Basi mwisho nilimpata huyu mume wangu aliyenioa, ila cha kusikitisha ni kwamba hakuna mtu aliyenisaport kwa hiyo nilikuwa peke yangu. Yaani hapa nataka kusema shida kubwa ilikuwa ni kwamba kati ya hawa vijana walionichumbia watatu walikuwa ni familia moja kwa hiyo ilikuwa shida sana kuamua ni nani atakuwa mchumba wangu kwani wote walinipenda na walikuwa vijana wazuri. Kwa hiyo kwa hasira na uchungu niliamua kukubali kuolewa na huyu mume wangu sio kwamba sikumpenda hapana nilimpenda na yeye alinipenda na bado tunapendana. Lakini kuna kipindi bado nawakumbuka wale vijana watatu je kuna msomaji anaweza kuniambia kwa nini bado nawakumbuka. kwani katika hii ndoa nina watoto wawili na pia tunapendana sana. Naomba maoni yenu ndugu zangu.



Na ;Yasinta Ngonyani

3 comments:

  1. Ni kweli mapenzi ni kitu cha ajabu sana, Je hao jamaa watatu bado huwa unawasiliana nao mara kwa mara? Kitu cha msingi ni kwamba wanawake unampenda mtu unaanzia ndani yaani unamuweka moyoni. Na maandika yako wazi kwamba Linda sana moyo wako maana huko kuna chemichemi za uzima, Kitu kikiwekwa moyoni ni kazi sana kufutika, kiwe cha uzuri au ubaya ndiyo maana pia maandika yanasema moyo ni mdanganyifu kuliko kitu chochote. Hivyo ni kweli hukuolewa na mmoja wao kwa kuwa uliwaweka moyoni ni ngumu sana wao kufutia hadi ufanyie moyo wako therapy itakayosaidia kuwasahau. Hata hivyo kama ndoa yako ipo safi na mnapendana basi hakuna shida kwani maisha ndivyo yalivyo.
    Inaonekana uliwapenda sana na kweli uliwajaza moyoni mwako wazima wazima.
    Upendo daima

    ReplyDelete
  2. Ndiyo naungana na kaka Mbilinyi hapo kwamba moyo hunena kwa matendo,hisia na mtazamo hata kama binadamu tunajaribu kujificha juu ya yale tuyapendaye.Ni wazi uliwapenda lakini sijui unajichukuliaje wakati huu,hata hivyo unapaswa kupigana na moyo wako kwa njia salama tu ambazo hazitaathiri moyo wako.Kwani naamini kuwa heri akupendaye kuliko umpendaye.Hii falsafa ngumu kwani hata Fresh Jumbe anatueleza katika wimbo wake wa Penzi ni kikohozi.Anasema huwezi kujificha na huwezi kutoweka lakini umependa shauri moyo unahiari kupenda.Unachopaswa jiangalie sana wakati huu kwani ni ishara ya mapambano ya nafsi,huu ni muda ambao utaeleza busara zako.Tulia,ungekuwa karibu ningelimwomba Mwanafalsafa{Mwanamuziki wa bongofleva anajiita hivyo} akuimbie wimbo wake wa 'BADO NIPO NIPO'.Hoja yake ni kwamba hekima ni tiba,mapenzi ni shida uwe unapenda au hujapenda.Lkini inagharibu kuchukua uamuzi wa lawama.Hao jamaa wakumbuke kama binadamu wengine. Umesahau kisa cha Yasinta?

    ReplyDelete
  3. Asanteni sana sana kaka zangu kwa maoni yenu. Kaka Mbilinyi jibu ni ndiyo mmoja wa hao bado nina mawasiliano naye na mmoja nimepata habari amefariki na huyu mmoja hatuwasilianai. Na ndiyo kaka Markus nakumbuka sana kisa cha Yasinta kwa nini?

    ReplyDelete