Monday, May 10, 2021
MKE ASIYE NA MUME, AKAMCHUMBIE NANI?
Niolewe na nani mie!
Isingekuwa vigeni, mwanamke kuchumbia
Ningepita mitaani, mume kujitafutia,
Nisimuudhi Manani, ndio nimejizuia.
Mke asiye na mume akamchumbie nani?
Ndege maingainga, si jambo la kujitakia,
Mume mwema natamani, vipi tajitafutia?
Na mwanamume haini, sitaki kunichumbia,
Mke asiye na mume akamchumbie nani?
Nimetulia nyumbani, sina mume kunioa,
Wanifuatao ndani, si wachumba wa kuoa,
Hutaka kunirubuni, maasini kunitia,
Mke asiye na mume akamchumbie nani?
Ndege maingainga, si kosa langu sikia,
Niliolewa zamani na mume mwenye udhia,
Kanitia kilabuni, pombe kumchuuzia
Mke asiye na mume akamchumbie nani?
Mimi nikamuamini, huku machozi nalia,
Mume hii kazi gani, alokataza jalia?
Kheri tukate kuni, mimi nitakuuzia.
Mke asiye na mume akamchumbie nani?
Akapanda hasirani, na maneno akafyoa:
Mke wee mke gani, dini lini ulijua!
Alipozidisha kani, ndoaye nikajivua.
Mke asiye na mume akamchumbie nani?
Wako mabwana wa shani, ningependa kunioa,
Hawamtii shetani, Munguamewaongoa,
Nao wamomashakani, kwa mabibi walooa,
Mke asiye na mume akamchumbie nani?
Tu wema hatujuani, wake na waume pia,
Twaingia mashakani, kwa wenzi waso murua,
Namlilia Manani, mume mwema kunioa,
Mke asiye na mume akamchumbie nani?
Nawe muombe, ndoa yenu kutulia,
Tusikuone mwakani, viragoumepania,
Mke na mume nyumbani, mumche Mola Jalia.
Mke asiye na mume akamchumbie nani?
Shairi hili limetungwa na Sheikh Amri Abedi, nami limenivutia nikaona niliweke hapa ili tujifunze kwa pamoja
Mwana uvute subira kwani inavuta heri
ReplyDeletenasema si masihara, itakuijia heri
japo huoni ishara, wewe muombe Kahari,
Mke ni mwenye mme aso naye msichana
aso na mme si mke, anaitwa mwanamke
na wala usimcheke, na usichana avuke
vyote vi manani mwake, muombe ili uvuke,
mke ni mwenye mme aso naye mwanamke
uendelee kuenga, Bahawa atakuenga
ujiepushe kudanga, usiende kwa waganga
ni yeye mwenye kupanga, anayo yote maninga,
aso na mme si mke mke shurti ni mume
tofauti mwanamke, japo mke mwanamke
na ili awe mke, mume aonyeshe wake
kwani siyo kila mwanamke aweza kuitwa mke
mke ni alo na mume, aso naye mwanamke
huna haja kuumia, ukisaka wanaume,
pale utapojaliwa, waje na uwakome,
wewe muombe Jalia, kwani yeye ndo ngome
mke ni alo na mume aso naye mwanamke