Tuesday, January 21, 2020

HISTORIA:- VITA KATI YA WANGONI NA WAMATENGO.....

Kabila la Wamatengo ni Kabila la Asili, halijaundwa kwa kutokana na makabila mengi yaliyochanganyika kama ilivyokuwa kwa kabila la Wangoni, ndio maana hata lugha yake haijaathiriwa na lugha zingine kwa kiasi kikubwa.

Ni makabila machache tu yaliyotoka katika koo nyingine ukoo wa akina KAPINGA, KOMBA (Hanze), MAPUNDA na LUANDA; ni koo ambazo ziliingia kutoka upangwa. Vile vile koo kama akina NDIMBO na NCHIMBI zilitoka Magharibi ya pwani ya ZIWA NYASA. Koo hizi ambazo zilitoka nje hazikuleta athari katika lugha ya kimatengo, ukizingatia kuwa koo hizo zilikuwa chache kiidadi kuliko wenyeji wa asili ya nchi ya UMATENGO.

MAKITA KAYUNI wa ukoo wa akina NDUNGURU ambaye ni Babu kati ya watawala waliokuwa machifu katika nchi ya Umatengo mwishoni inasadikika kuwa, kwa asili alitoka kabila la WANINDi, aliishi chini ya mlima Matogoro karibu na Songea.

Alipoingia MPUTA MASEKO katika nchi ya Ungoni. MAKITA KAYUNI alishindwa kupigana naye akasalimisha jeshi lake kisha akajiunga naye na akapata fursa ya kujifunza mbinu za kivita.

Kayuni alijipatia uhuru wa kufanya chochote na kwenda kokote alikotaka baada ya Mputa Maseko kufukuzwa katika Wilaya ya Songea, akaamua kuhamia katika nchi ya umatengo huko LITEMBO ambako alipokelewa kwa ukarimu mkubwa mno na KAWANILA HYERA pamoja na LIHUHU KINUNDA.

Kayuni alikuwa na ufundi katika masuala vita pamoja na akili ya maisha, watu wa Litembo (Wamatengo) waliona anafaa kuwa kiongozi; alipokufa Kawamila bwana Makita alichaguliwa kuwa mrithi wake.

Baba wa Kayuni Mzee Kapitingana alifika Litembo na kuweka makazi yake; licha ya kwamba Kayuni hakuishi Litembo maisha yake yote lakini alizaliwa katika ardhi ya Litembo kwa Ndenya Ndunguru. Kayuni alipewa jina la ukoo wa Mama yake kwa kuwa Baba yake Mzee Kapitingana hakulipa Mahari.

Familia ya Makita kipindi cha Mputa Maseko (1864 -1865)
Ukoo wa Babu, Baba, Makita na Familia yake waliishi Litembo, familia ya Makita ilifika Litembo baada ya Mputa Maseko kuikimbia Songea mwaka 1864s.

Inaelezwa mwaka 1866s Kayuni alipata bahati ya kuzaliwa; hivyo kuna uhakika kwamba Makita Kayuni aliuawa akiwa na umri mkubwa kwenye vita ya mwisho kati ya Wangoni na Wamatengo ambayo ilikuwa miaka minne kabla ya kifo cha Nkosi Mharule kilichotokea mwaka 1885.

MAKAZI YA WAMATENGO NA TAKWIMU ZAO KABLA YA WANGONI KUJA SONGEA

Kabla ya Wangoni kuja Songea na kujenga Makazi yao, Wamatengo waliishi katika vijiji ambavyo vilitengana tengana au kutawanyika (Musi musi) kama vile Litembo, Mapera, Ungima (Ngima), Hanga, Kitogota, Kimati, Nkuka, Ungwindi, Baruma, Matiri (karibu na Milima ya Lilengalenga).

Wamatengo walipata shida sana kulinda Miji yao dhidi ya vita ya Wangoni walipoelekea umatengoni ili kufanya makazi yao. Kundi kubwa la watu wailishi katika Bonde la Litembo.

Mwandishi Fullborn amefafanua kwamba, kijiji cha Makita kilikuwa na watu 5,000 kwa mujibu wa Sensa iliyofanywa na Wajerumani mwaka 1904 huku idadi kubwa ya watu ikitoka katika bonde la Litembo katika eneo la Makita, suala ambalo lilipelekea ulinzi kuwa mdogo wakati wa vita.

Wageni waliobahati kutembelea katika kijiji cha Makita wanafafanua kwamba mitetemeko yote inayohusiana na milima ya Litembo ilijengwa vibanda, mapango katika milima ya Litembo yalitumika kwa ajili ya kujificha wakati wa vita. Bro. Laurentius Brenner aliyapima baadhi ya mapango mwaka 1906 na akaandika mambo muhimu aliyoyabaini.

“Wamatengo wengi wanaishi katika mapango. Sehemu zingine katika hivi vibanda havionyeshi kama wanaishi watu, lakini wanaishi pale, inaonekana miamba mikubwa ndio nyumba zao.
Inavyotokea wazungu wanajitokeza kwao hujificha kwenye miamba hiyo; katika baadhi ya mapango hakuna anayeweza kuingia akiwa wima, nililiona pango mojawapo liliokandikwa kwa udongo ambalo lilijazwa kuni pande zote”
“Ni jambo la kushangaza pango hilo lilikuwa na kina cha mita mbili hadi tatu, hadi kukifikia chumba kulikuwa na ngazi zilizoelekea katika eneo la kuchota maji. Hata hivyo palikuwepo na mapango mengine ambayo haikuwa rahisi kuona mlango wa kuingilia, ila shimo dogo la kutokea moshi lilionekana”
“Mapango mengine yana kina lakini hayaruhusu mwanga wa jua kuingia wala kupenya, inaonekana watu huyatumia wakati wa usiku tu! kuna baadhi ya mapango yana mlango wa pili ambao ni ngumu mno kuuona kwa macho, uenda unatumika wakati wa hatari tu!” alisema Brenner.

Kama si Mapango Wamatengo wangeteketezwa na Wangoni
Hata katika kipindi cha Mputa Maseko na hawaya Wangoni walifanya mashambulizi ya kivita dhidi ya kabila la Wamatengo na kuteka mali za Wamatengo na mifugo yao.

Wamatengo walipoamua kuishi katika bonde la Litembo jeshi la Wangoni lilipata shida mno wakati wa mapambano mara nyingi walirudi ungonini bila kutekeleza mipango yao ya kuwasambaratisha Wamatengo.

Vita ya maana yenye kukumbukwa ni ile iliyotokea mwaka 1885 ambayo ilikuwa ni vita ya mwisho kati yao. Makita alishauriwa na baadhi ya watu kwamba amdharau Nkosi Mharule na kutuma baadhi ya watu wakachukue aina ya nyasi ziitwazo ‘Sekela” ili kuzungushia wigo kwenye vibanda vyake.

Kitendo ambacho kilimfanya chifu Mharule achukie kwa kudharauliwa na Makita na hivyo akaenda umatengoni kupambana nao. Inaelezwa kwamba Mfanyabiashara Litunu alitumwa umatengoni, alipita katika ardhi ya wamatengo kuelekea Ziwa Nyasa, inasadikia njiani alishambuliwa na watu ambao iliilezwa walikuwa ni Wamatengo.

Kutokana na kupea kwa urafiki kati ya Litunu pamoja na Mharule hivyo hata biashara zake zilikuwa chini ya utawala wa Nkosi Mharule, hivyo Mharule alipata sababu za kuwapiga Wamatengo na wakati huo alikuwa amehamia sehemu iitwayo karibu na Matomondo kwenye barabara inayoelekea Mbambabay.

Kuuawa kwa Makita katika vita baina ya Wangoni na Wamatengo
Manduna wa Kingoni walioshiriki kwenda kupiga vita hiyo katika nchi ya Wamatengo ni pamoja na Nduna Songea, Sanangula, Mpangile, Chikuse na wengine. Wakati wa vita hiyo Makita mwenyewe alisimama juu ya mwamba mkubwa ili kuwapa moyo Askari wa Kimatengo.

Wakati vita ilipokuwa imepamba moto katika vijiji mbali mbali mke wa Makita alikuwa na mume wake muda wote juu ya mwamba huku akimwaga dawa ya vita toka kwenye kikapu chake na kumtia moyo ili Wamatengo waweze kushinda katika vita ambayo ilidumu kwa muda mrefu bila kufikia ukomo.

Askari wa kingoni kwa kutumia bunduki yake alimtungua Makita akiwa juu ya Mwambo huo kisha akadongoka na kupoteza maisha pale pale, tukio hilo lilipelekea Askari wa makita kujisalimisha mikononi mwa Askari wa Kingoni na wakajitangazia ushindi na wakafanya sherehe.

Wangoni walirudi katika ardhi yao huku wakiwa na Mateka mengi pamoja na mali zao, baadhi ya waliotekwa ni Makita Ndunguru ndugu yake Makita Kayuni ambaye alitekwa na watu wa Sanangula; lakini baada ya kuwasili huko Sanangula aliteuliwa kuwa kiongozi wa Wamatengo wa Sanangula.

Mtoto mkubwa wa Makita Kayuni alirithi kiti cha Baba yake na akatawala nchi ya Wamatengo kwa mika mingi, mwaka 1897 wakati wa utawala wa Mandawa Wajerumani walifika Songea.

Machi 1902 Wamatengo waliwaasi Wajerumani na wakakataa kulipa kodi kwenye serikali ya Kijerumani na wakachoma moto shule ya msingi Litembo ambayo ilianzishwa na Padre Yohannes Hafliger wa Kigonsera tarehe 11-9-1901.

Kitendo hicho kiliisha mara moja wakati wa utawala wa Mandawa na baadaye alimwachia madaraka mdogo wake Mtwara ili kumpa heshima ambaye naye aliitawala umatengo yote. Vita ya Maji Maji ilipoingia umatengoni hawakupenda kushirikiana na Wangoni ambao ni maadui zao wa zamani ili kuwapiga wajerumani.

Kufuatia kifo cha Mtwara, cheo chake kilichukuliwa na Tekambwani mtoto mwingine wa Makita Kayuni, ambaye alifariki baada ya kutawala kwa kipindi kifupi. Watoto wengine wa Makita Kayuni waliikosa fursa ya kuitawala nchi ya umatengo kwa kuwa walikuwa wadogo mno hivyo wazee wa kimatengo wakamchagua Kapungu na akawa chifu wao.

Mwaka 1916, Waingereza walipoichukua Tanganyika na kuitawala kwa mabavu, Kapungu aliondolewa madarakani kisha akawekwa Makita Kipwele Kayuni mtoto wa mtoto wa Makita Kayuni wa I.

Baadaye alilithiwa na Magnus b. Bunungu na baadaye Mrithi wake akawa Yohannes Christomus Makita Kayuni, jina la Makita kutoka Makita Kayuni II Kipwele.

1 comment: