Thursday, May 18, 2017

MAMA HIVI ULIMPA MUNGU SHILINGI NGAPI?


Baada ya miaka saba ya ndoa bila kupata mtoto, Magreth alimuambia mumewe Benjamin kuwa atafute mwanamke mwingine wa kuzaa naye. Walishahangaika sana kuzunguka mahospitalini na kwa waganga wa kienyeji bila mafanikio.

Nyumba yao ilikua na amani na Ben alishakubaliana na ile hali, lakini ndugu zake walikua wanasumbua sana, walimtukana mkewe matusi mengi, wakimuambia kula, kulala anawajazia choo, walimnyanyasa sana na Mage hakuwa na raha.

Aliona njia pekee ni kumruhusu mumewe kuoa mwanamke mwingine ili angalau apate mtoto na ndugu zake waache kumsakama. Ben hakuwa tayari kuoa mwanamke mwingine, alikataa katakata lakini mkewe alisisitiza huku akitishia kuondoka kama asingeoa mke mwingine.

Siku moja Ben aliamua kuwaita ndugu zake wote, na wote waliitikaa wito  aliwaambia ana kitu kikubwa cha kuwaambia kwani na yeye alishachoka suala la mtoto na alitaka kufanya mamauzi makubwa. Wakiwa na shauku ya kujua ni nini walifika.

Ben aliwapokea vizuri na baada ya chakula Ben alimuambia mkewe akachukue begi liko kitandani. Ndugu zake walitabasmu wakijua mtoto wao kaamka na sasa anamfukuza mkewe ili atafute mke mwingine na kupata mtoto.

Mkewe alienda kitandani, alichukua begi kubwa na kulileta pale. Ndugu walikaa kimya, Ben alilichukua na kulifungua, lilikua limejaa pesa tu, noti za shilingi elfu kumi  zimepangwa vizuri.

Kila mtu alishangaa na hata mkewe alishangaa. Ben alianza kuongea. “Ndugu zangu nimewaita hapa kwa kuwa  nina tatizo kubwa nyie wote mna watoto Mungu kawabariki hata wewe mdogo wangu hapa ni mjamzito na Mungu akijaalia utajifungua salama.

Lakini mimi na mke wangu Mungu hajatubariki kuwa na  watoto” Alitulia kidogo huku akifuta machozi, yaliyotaka kudondoka. “Sasa nimewaita hapa mnisaidie kitu kimoja tu. Nianze na wewe Mama kwani kila siku umekua ukiniambia kuhusu mjukuu.

Aliongea huku akimgeukia Mma yake. “Chochote mwanangu…” Mama yake aliitikia kwa shauku. “Ninachotaka Mama ni kwamba uniambie ulimpa Mungu shilingi ngapi mpaka akakupa watoto…

Maana mimi nimejaribu imeshindikana, hizi ni hela zote nilizonazo benki na  kesho nitaongea na Dalali ili tuuze nyumba mimi na mke wangu tukapangishe lakini tupate mtoto.”

Alitulia kidogo, watu wote walimshangaa, lakini aliendelea. “Ndugu zangu nisaidieni, nyie mna watoto mlimpa Mungu shilingi ngapi au nini mlitoa, mlimuona wapi mkampelekea, mimi nipo tayari kutoa kila kitu katika maisha yangu ili tu na mimi niitwe Baba na mke wangu aitwe Mama.

Niambieni tu ni bei gani Mungu anapokea?” Wote walinyamaza kimya, hakuna aliyeongea tena, walimuangalia huku wakiangaliana kwa aibu. Hakuna aliyejaribu kunyanyua mdomo.

“Sasa ndugu zangu kama hamjui kiasi ambacho Mungu anapokea ili kutoa watoto basi sitaki kusikia tena hili suala. Mimi na mke wangu tuna furaha, sitaki mtuingilie, siku mkitaja mtoto mje mniambie anauzwa wapi na bei gani nitanunua!

Kama nyie mlinunua au ni wajanja sana mpaka mkampata nifundisheni huo ujanja….Mama…” Alimgeukia Mama yake. “Nakupenda sana lakini mimi sina uwezo wa kujipa mtoto, kama unajua Mungu anataka kiasi gani basi niambie ila kama na wewe hujui basi sitaki umsumbue mke wangu.

Kila siku mnampigia kelele kuwa hazai hazai hivi mnafikiri yeye hataki mtoto, mnafikiri yeye hataki kuitwa Mama, sasa mimi nimemaliza, hizi pesa narudisha ndani siku mkisikia Mungu anauza watoto basi niambieni nitakuja kununua la sivyo mtuache na ndoa yetu..”

Alimaliza kuongea, wote walitoka kimyakimya bila kuongea chochote. Tangu siku hiyo hakukuwa na maneno tena ya mtoto wala nini. Ben na mkewe bado hawajajaaliwa kupata mtoto, wameamua kuasili mtoto yatima na wanaishi naye kama mtoto wao na wote wanafuraha.

***** Imeandikwa Na. Iddi Makengo

Kabla hujamnyanyasa mtu kwa kitu ambacho hana uwezo nacho hembu jiulize wewe ulimpa nini Mungu mpaka akakupa hicho kitu?

 Kwani kuna watu ambao wanadhani kuwa Mungu anawapenda wao zaidi na wao ni bora kuliko wengine.

No comments:

Post a Comment