Wednesday, April 12, 2017

KUTOKUWA KARIBU NA FAMILIA KUNAVYOATHIRI TABIA ZA WATOTO

MALEZI katika mazingira yetu ya Kiafrika ni suala nyeti. Hatuna historia ya kupuuza watoto tunaowazaa. Kwa kutambua umuhimu wa malezi katika kujenga jamii yenye ustawi, tumekuwa na desturi ya kuelekeza nguvu zetu nyingi katika malezi ya watoto wetu. Kwa mfano, tangu mtoto anapozaliwa, ilikuwa ni lazima alale kitanda kimoja na wazazi wake kwa muda unaozidi miaka miwili. Mtoto mchanga hakuachwa alale kwenye kitanda chake mapema.
Aidha, alikulia mikononi mwa watu wazima aliowafahamu vyema kwa sababu ama aliishi nao kwenye boma la wazazi wake au walitoka miongoni mwa jamii inayomzunguka. Muda mwingi alibebwa mgongoni kwa mama yake au dada zake kuthibitisha kuwa ukuaji wa mtoto ulifuatiliwa kwa karibu mno na wazazi wake.
Jambo hili halieleweki kwa wageni wa bara hili wanaodhani ni aina ya udhalilishaji wa mtoto. Kitendo cha kumbeba mtoto mgongoni  kimethibitika kisayansi kusaidia kujenga muunganiko wa kihisia kati ya mzazi na mtoto.
Wakati wa jioni, familia zilikuwa na desturi ya watoto kukaa na wazazi wao kijinsia. Baba aliota moto na watoto wa kiume akiwasimulia mambo mbalimbali ya kimaisha. Kadhalika, mama naye alifanya kazi za jikoni kwa ushirikiano wa karibu na watoto wa kike. Chakula kilipokuwa tayari kililiwa kwa ushirikiano. Muda wa chakula ulifahamika na kila mtoto aliwajibika kupata chakula. Desturi hii ya kukaa karibu na watoto na kufanya mambo mengi kwa pamoja mbali ya kuwasaidia wazazi kuwafundisha watoto maarifa na ujuzi wa aina mbalimbali, ilikuza uhusiano wa karibu wa kifamilia ambao uliwahakikishia usalama wao. Hali ya mtoto kumwamini na kujisikia salama mikononi mwa mzazi inategemea uwapo endelevu wa mzazi kimwili na kihisia tangu anapozaliwa.
Hata hivyo, kadri mwanadamu anavyozidi ‘kuendelea’ na ‘kustaarabika’, ndivyo desturi hii ya kupatikana kwa wazazi nyumbani inavyozidi kukosa umaarufu. Kwa mfano; ipo dhana inajengeka katika jamii kwamba maendeleo halisi ni vitu. Matokeo ya imani hii ni kutufanya tutumie muda mwingi kujilimbikizia vitu kwa gharama ya uhusiano na ustawi wa familia zetu.
Kadhalika, zipo changamoto nyingine za kijamii zinazotishia desturi hii ya familia. Kuna masuala kama kazi/ajira zinazowatenganisha wazazi na familia, misukosuko ya kimahusiano inayozaa talaka na/ama kulazimisha malezi ya mzazi mmoja, ujio wa shule za bweni kwa watoto wadogo pamoja na matatizo kadha wa kadha yanayofanya watoto wadogo wakue katika mazingira magumu yasiyo na uangalizi mzuri.
Kwa hiyo, tafiti zinazochunguza matokeo/athari za mazingira ya kimalezi katika ukuaji wa mtoto ni jitihada za kutafuta majibu ya changamoto hizi zisizokwepeka. Kwa kifupi, tunaweza kutaja mambo mawili kwa kutumia matokeo ya tafiti hizo. Kwanza, uhusiano wa mzazi na mtoto ndiyo unaoamua uhusiano kati ya mtoto na watu wengine na namna mtoto huyo atakavyojitazama yeye mwenyewe na watu wengine akiwamo mzazi wake.
Suala la pili ni matokeo ya umbali -kimwili na kihisia – unaotokea katika kipindi cha awali kabisa cha maisha yake, unaoweza kujenga hitilafu za kitabia kwa mtoto.
Mwandishi ni mwalimu wa Saikolojia katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). 

2 comments:

  1. Ni kweli kabisa, ujumbe huu ni muhimu kwetu sote wazazi....

    ReplyDelete
  2. Ndugu wa mimi ahsante sana ni kweli huu ujumbe ilibidi wengi wasome hasa wazazi/walezi

    ReplyDelete