Thursday, January 12, 2017

HADITHI:- DALILI YA MVUA NI MAWINGU

Hii ni hadithi kuhusu kijana mmoja, aliyechagua msichana wa kumwoa, na kuzaa naye watoto, na kwa kali hiyo kuukuza ukoo wake. Lakini kabla ya mipango ya mwisho ya harusi na baba mkwe wake, aliamua awajaribu wakwe zake kwa mtihani mdogo.

Asubuhi moja, akaomba ruhusu kwa wake zake aende kijijini kwao akachukue vifaa vyake vya kulimia, na angeshukuru kama shemeji yake, dada wa atayekuwa mkewe atafuatana naye. "Umekuja hapa, kumtafuta mke utakayeishi naye, karibu tutakuwa ndugu, kwa hiyo shemeji yako akikubali, sisi hatuna kuzuizi," wakwe walimjibu.

Hivyo Kijana na shemeji yake wakaondoka, na walipofika kijijini kwake, badala ya kuchukua vifaa vya kilimo, akachukua mkuki, pamoja na shemeji yake, wakaenda kuwinda. Kijana akauwa mnyama mkubwa, wakaanza safari ya kurudi kijijini kwa wakwe zake. Shemeji yake akawa amebeba kitoweo huku kijana amebeba mkiku wake.

Njiani akamwambia shemeji yake, kuwa kuleta kitoweo nyumbani, ni njia mojawapo ya kuhakikisha uhodari na uwezo wa kuwatunza wakwe na familia yake. Wakapokewa kwa shangwe, kijana naye akapongezwa kwa uhodari wake.

Usiku huo huo, akawaeleza wakwe zake kwamba alitaka ajaribu tena jwenda kuwinda na vile vile akaomba ruhusu ya kufuatana na shemeji yake.
"Sasa tuko kama ndugu, sisi tunataka tukusaidie kwa kila njia tutavyoweza!" Baba mkwe akamwambia.

Hivyo, siku iliyofuata, wakaondoka tena na haikuchukua muda, kijana kwa uhodari wake, akauwa mnyama wapili. Mara hii mnyama aliyemwua alikuwa mkubwa na mzito kiasi kwamba, wote wawili walishindwa kumbeba. Uamuzi ukawa kwamba yule kijana, arudi kijijini kwenda kuomba msaada, na shemeji yake abakie kuchunga kitoweo. Kijana alipoondoka, yule msichana akapanda juu ya mti, kuhofia wanyama wakali, akisubiri msaada ufike.

Kijana alipofika kijijini akajitupa kwa kilio chini ya miguu ya mkewe wa mtarajiwa. Akisema kama amefanya kosa kubwa sana.
Badala ya kutupa mkuki kumchoma myama, sababu ya giza alimchoma dada yake ambaye sasa amemwacha amekufa porini.
Familia nzima wakajiwa na chuki na wakaanza kumtukana maneno mbali mbali, kusikia kisa hicho. Wakaanza kumpiga vile vile: " unawezaje kusema wewe ni mwindaji hodari, kutaka kutunza familia ikiwa umefanya upumbavu kama huu?" Walimpiga sana mpaka kidogo azirai. wakagundua kwamba wakiendelea kumpiga wanaweza kumuua na wasiweze kupata maiti ya msichana wao. Maana ni yule kijana peke yake alifahamu maiti ilipo. Wakamwamuru yule kijana ambaye alikuwa hai kwa mapigo, aongozane nao akawaonyeshe maiti ya msichana wao ilipo.

Walipofika, walistaajabu sana kumwona msichana wao akiteremka toka juu ya mti. Akishangaa na kuwauliza kwa nini yule kijana alikuwa katika hali mbaya hiyo huku ametapakaa damu. Familia nzima  ilishindwa kusema cho chote kuhusu kitendo hicho kwa kuona aibu, Kwa maovu waliyomfanyia. Wakamwomba msamaha yule kijana. Wakasaidiana kumchukua yule mnyama na kumkata vipande. Wakavibeba hivyo vipande na kurudi kijijini. Walipofika tu, yule kijana akafungasha mizigo yake na kabla hajaondoka, akawaambia kuwa hataoa msichana kutoka kwenye familia ya watu wasiokuwa na huruma na wakorofi.  Hivyo akafunga safari na kuondoka.

Haukupita muda, kwenye kijiji kingine alichohamia, akapata mchumba mwingine. Vile vile akawajaribu wakwe zake kama alivyofanya awali na mchumba wake wa kwanza. Safari hii mambo yakawa tofauti! Wakwe zake wapya, walishtuka na madhara yaliyotokea, akasamehewa kwa ajali iliyotokea na wakamwomba yule kijana akawaonyeshe sehemuu ambapo ajali ilitokea, ili wachukue maiti na kuja  kuzika ipasavyo. Walipofika sehemu ya ajali ilipotokea wakamkuta shemeji yake, yaani msichana wao mzima kabisa amesimama kando ya mnyama aliyeuawa na mkwe wao.

Ikabidi yule kijana aeleze mkasa toka mwanzo mpaka mwisho, akatoa sababu za kufanya kitendo hicho. Na kamaliza kusema kwamba, sasa amepata mke aliyekuwa  akimtafuta ambaye tabia yake pamoja na familia yake, ni ya watu adili. Akamuoa mchumba wake, wakaishi kwa muda kabla ya kuhamia kijijini kwa yule kijana na kuishi maisha yao yote
CHANZO:-  HADITHI NA VISA KUTOKA TANZANIA

No comments:

Post a Comment