Wednesday, December 14, 2016

HILI NENO, "MWANAUME NI KICHWA CHA NYUMBA," HUWAPA KIBRI SANA HAWA VIUMBE



Kuna jambo moja ambalo hufundishwa na viongozi wa dini mbalimbali, ambalo pia waumini hulihubiri vizuri kila mahali wapatapo nafasi ya kufanya hivyo. Nalo si jingine ni lile la ‘mwanaume ni kichwa cha nyumba,’ ikiwa na maana kuwa mwanaume ndiye mkuu wa nyumba au familia. Suala hili linazungumzwa kama kwamba, mwanaume kuwa mkuu wa familia ni jambo la kimaumbile, lakini pia huzungumzwa kama vile, ukuu huo ni tiketi ya mwanaume kuikandamiza familia au mke. 


Nijuavyo mimi, wanaume wengi kuwa wakuu wa nyumba au familia ni suala la mazoea zaidi kuliko maumbile. Kwa miaka milioni kadhaa, mwanaume amejikuta akiwa ndiye mkuu wa familia. Kutokana na mazoea haya, jambo hili limekuwa kama vile ni la kimaumbile, yaani haliwezi kubadilika au kubadilishwa.



Lakini mbona kuna wanawake ambao ndiyo wakuu wa familia na familia hizo zinakwenda vizuri tu. Lakini vilevile kuna wanawake ambao hawana waume na wanaongoza vyema familia zao. Kwa bahati mbaya kwenye jambo hili, ni kwamba, kumekuwa na msisitizo kuwataka wanawake wawaheshimu waume na siyo wanandoa kuheshimiana. ‘mwanaume ni kichwa cha nyumba, ndiye msemaji wa mwisho. Inabidi aheshimiwe.’ Kuna watu ambao bila aibu huzungumza lugha hii.



Ni kweli wanaume wanahitaji au wanapaswa kuheshimiwa. Lakini siyo wanaume peke yao, bali binadamu wote wanapaswa kuheshimiwa bila kujali wanafanya nini au wakoje. Kwa hiyo siyo kwa sababu ni wasemaji wa mwisho, basi wao ndiyo wanaopaswa kuheshimiwa. Kwa kuamini hivyo wanaume wengi wamekuwa wakitumia nafasi hiyo kuwakandamiza wake zao na hata watoto. ‘Mimi ndiyo msemaji humu ndani, nimesema sitaki, basi.’ Mara nyingi matumizi ya mabavu kwa namna hiyo hutumika.



Kuna haja kwa wanaume kujua kwamba, kuwa kwao viongozi wa familia hakuwapi ubora wa ziada. Wanawake nao wanapaswa kujua kwamba, kutokuwa kwao wasemaji wa mwisho wa familia, hakupunguzi hata chembe ya thamani ya ubinadamu wao, kwani binadamu na wanandoa wanapaswa kuheshimiana. 
HABARI HII NIMEITOA  KWA MDOGO WANGU KOERO HAPA

3 comments:

  1. Kwangu na mke wangu kila mmoja ni kichwa hasa ikizingatiwa kuwa kichwa ndicho binadamu. Angalia passport au Driver's licence yako na vitambulisho vingine uone kama kuna kiwiliwili. Hivyo, kwenye ndoa imara na ya kutaka kuepuka mifarakano ya kijinsia wanandoa wanapaswa kuogopa zana hii kama ukoma. Kwa waumini katika usawa wa binadamu, dhana hii ni potofu. Nina wasi wasi. Hata kwenye vitabu vya dini imeingizwa si kwa amri ya Mungu bali woga wa mfumo dume wa wakati ule. Hata hivyo, kwa kizazi kilichoendelea na kujitambua vya kutosha ni ajabu kuongozwa na falsafa za miaka elfu mbili iliyopita.

    ReplyDelete
  2. Kaka Mhango...nimependa maoni yako kwa kweli. Kuhusu wanaume kuwa wakuu wa nyumba hii ni jinsi tu ya malezi yetu na hasa tamaduni zetu. Ila mimi ningependa kusema si kweli kabisa ni maelewano tu katika kila ndoa......

    ReplyDelete
  3. Msidanganyane
    Mwanaume ni kichwa

    ReplyDelete