Wednesday, August 24, 2016

AFRIKA YETU...TANZANIA:-MILA NA UTAMADUNI WETU... UNAWAFAHAMU WAMASAI


Kama tujuavyo Tanzania yetu ina makabila mengi sana kwa hiyo na mila pia tamaduni zitakuwa nyingi...Kwa hiyo nimeona si mbaya nikianza na Kabila la kimasai fuatana nami.....

Kwa kweli hakuna kabila hapa nchini kwetu Tanzania linalotutoa kimasomaso kama kabila la Kimasai kwa kujali na kuendeleza MILA, na kabila hili liko madhubuti kwenye kufuata mila. kuanzia kufuata mila, vyakula wanavyokula mavazi pamoja na ndoa  kwa kweli kuna haja kubwa sana kwa makabil mengine kuiga mfano wa kabila la wamasai.

Kwani ndio kabila ambalo lipo mbele katika kuenzi na kulinda tamaduni zao huwezi kutembea ukamkuta mMasai akiwa hajavaa vazi lao la kimasai tofauti na makabila mengine.  Kwani makabila mengine wanavaa mavazi yao mpaka kuwe na sherehe za kimila/ kitamaduni. Lakini hivi hivi huwezi kuwakuta wakiwa wamevaa, ila kabila hili la kimasai wenyewe mpaka kwenye harusi hawakubali kuiga na kuvaa nguo za aina nyingi

Wamasai wana ustadi unaohitajika kuishi katika pori la Bonde la Ufa. Wao hutembea mbali sana kutafuta malisho na maji kwa ajili ya mifugo yao, nao huchunga mifugo miongoni mwa makundi ya kongoni, punda-milia, twiga, na wanyama wengine wanaoishi katika pori hilo.
Wamasai wanaamini kwamba ng’ombe wote duniani ni mali yao. Imani hiyo inatokana na hekaya inayosema kwamba hapo mwanzoni Mungu alikuwa na wana watatu, naye alimpa kila mmoja zawadi. Yule wa kwanza alipokea mshale wa kuwindia, yule wa pili alipokea jembe la kulimia, na yule wa tatu alipokea fimbo ya kuchunga ng’ombe. Inasemekana kwamba yule mwana wa mwisho alikuwa babu wa kale wa Wamasai. Ijapokuwa watu wa makabila mengine wanafuga ng’ombe, Wamasai wanaamini kwamba ng’ombe hao ni mali yao. Mwanamume mwenye ng’ombe na watoto wengi huheshimiwa na kupewa hadhi katika jamii ya Wamasai. Mwanamume aliye na ng’ombe wanaopungua 50 huonwa kuwa mtu maskini. Kwa msaada wa wake zake na watoto wake wengi, mwanamume Mmasai hutarajia hatimaye kuwa na kundi kubwa linaloweza kufikia ng’ombe 10000. Wamasai hupenda ng’ombe zao. Kila mtu katika familia hutambua vizuri sauti na utu wa kila mnyama kundini. Mara nyingi, ng’ombe hurembeshwa kwa kuchorwa alama za mistari mirefu inayojipinda-pinda na mapambo mengine kwa kutumia chuma chenye moto. Nyimbo hutungwa juu ya sura nzuri za ng’ombe mbalimbali na jinsi wanavyopendwa. Fahali wenye pembe kubwa zilizojipinda hupendwa sana, na ndama mdogo hutunzwa na kushughulikiwa kana kwamba ni mtoto aliyezaliwa karibuni. Nyumba za Wamasai hujengwa na wanawake, nazo hujengwa kwa matawi na nyasi na kisha hukandikwa kwa samadi ya ng’ombe. Nyumba za Wamasai ni zenye umbo la mstatili nazo huzunguka boma ambamo ng’ombe hulala usiku. Nje ya nyumba hizo kuna ua wa matawi yenye miiba unaowalinda Wamasai na ng’ombe zao dhidi ya fisi, chui, na simba wanaowinda usiku. Wamasai hutegemea sana mifugo yao, kwa hiyo ni lazima ng’ombe wawe na afya na nguvu. Wamasai hunywa maziwa ya ng’ombe na kutumia samadi ya ng’ombe kujenga nyumba. Wamasai huchinja ng’ombe mara chache sana.,
Wao hufuga mbuzi na kondoo wachache kwa ajili ya chakula.,Lakini ng’ombe anapochinjwa, kila sehemu ya mnyama hutumiwa. Pembe hutumiwa kutengeneza vyombo, kwato na mifupa hutumiwa kutengeneza mapambo; na ngozi zilizolainishwa hutumiwa kutengeneza viatu, nguo, matandiko, na kamba. 
Wamasai ni watu warefu, wembamba, na wenye sura nzuri. Wao hufunga mashuka yenye rangi nyangavu nyekundu na samawati. Wanawake hujirembesha kwa kuvalia mikufu mipana yenye shanga, na mapambo ya vichwani yenye rangi nyingi tofauti tofauti. Nyakati nyingine mikono na miguu hukazwa kikiki kwa nyaya nyingi nene za shaba. Wanawake na wanaume hurefusha masikio yao kwa kuvaa mapambo na vipuli vizito vyenye shanga. Madini mekundu yaliyosagwa huchanganywa na mafuta ya ng’ombe nayo hutumiwa kupamba mwili. Mida ya jioni  Wamasai  wanakusanyika ili kucheza ngoma, husimama katika duara na kusogea kwa kufuatana na mdundo. Mdundo wa ngoma ukizidi, ile mikufu mipana mizito yenye shanga kwenye mabega ya wasichana inaruka-ruka kwa kufuatana na mdundo. Kisha, moran (mpiganaji) mmoja baada ya mwingine anaingia katikati ya mduara na kuanza kurukaruka juu sana. Wacheza-ngoma wanaweza kuendelea kucheza usiku kucha hadi wote watakapochoka kabisa.

No comments:

Post a Comment