Monday, June 27, 2016

MABALAA HUMUANDAMA MTOTO WA KIKE TANGU AKIWA TUMBONI………!


Tatizo hili hufahamika kama Female Infanticide, yaani mauaji ya kukusudia yanayofanywa kwa mtoto wa kike. Achilia mbali kile kitendo cha mtoto kuuawa muda mfupi tu baada ya kuzaliwa, utelekezwaji wa mtoto wa kike mara tu anapozaliwa na kutoa mimba baada ya ugunduzi kwamba, ni mtoto wa kike, zote ni njia za kumuondoa mtoto wa kike duniani. Tatizo hili liko katika jamii zote zinazomchukulia mtoto wa kike kama balaa na yule wa kiume kama baraka kwa familia.
Kwa hapa nchini mtoto wa kike huuawa kwa njia isiyo ya moja kwa moja. Watoto wa kike hudharauliwa na kuachwa linapokuja swala la elimu katika familia. Ukichunguza hata wewe utabaini kwamba, katika familia nyingi, ambapo watoto wa kiume wamepata elimu bora, watoto wa kike katika familia hizo wamepuuzwa na hata kutopewa kabisa elimu.
Watoto wa kike, hasa wale wanaozaliwa nje ya ndoa wametelekezwa kirahisi, wamekataliwa na baba zao kirahisi, ukilinganisha na watoto wa kiume. Idadi ya watoto wa kike wanaokufa kutokana na kutelekezwa na kukataliwa na baba zao ni kubwa kuliko ya watoto wa kiume. Hata zile kesi nyingi za watoto kukataliwa na baba zao zinahusisha watoto wa kike zaidi.
Ni jambo la kushangaza kwamba ndoa ambayo ina watoto wa kike watupu hutazamwa kwa bezo na dharau ukilinganisha na ile yenye watoto wa kiume watupu. Hata wale wanawake wanaozaa watoto wa kike watupu hujihisi vibaya na kuamini kwamba walistahili kuzaa watoto wa kiume pia.
Kwa maeneo ua vijijini na katika familia masikini, watoto wa kike hutazamwa kama, ‘biashara ya kesho’ambapo watauzwa kwa njia ya mahari. Kwa hiyo thamani yao ni kuolewa, ni ile ya kibidhaa na sio kibinadamu. Na ndio maana mtoto wa kike anaposhindwa kuolewa huanza kuonekana kama mzigo usio na thamani, na hata kuzongwa hutokea.
Ili kujinasua na tatizo hili, msichana huenda kwa mwanaume yeyote kama kwa kujilazimisha. Kila mtu anajua kuhusu wazazi hapa nchini, ambao wamekuwa wakiwalazimisha binti zao kurudi kwenye ndoa za mateso kwa hofu ya kurejesha mahari. Kinachotokea ni binti hao kuuawa na waume zao. Ni wazi hii ni njia ya makusudi ya kuwapunguza wanawake, bila kujali mtu ataieleza vipi……………….
Chanzo........Jamii Forum

No comments:

Post a Comment