Thursday, May 12, 2016

UPELEKAJI MIHOGOCHINA WAZUA BALAA BUNGENI

Dodoma. Mbunge wa Songea Mjini (CCM), Leonidas Gama amemtaka Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage kufuta kauli ya kusafirisha mihogo ghafi kwenda China.
Mbunge huyo alisema jana kuwa, kauli hiyo inapingana na hotuba ya waziri huyo iliyosheheni mipango ya Serikali ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati kupitia viwanda ifikapo mwaka 2025.
Mbali na mbunge huyo, wabunge wengi waliochangia hotuba hiyo bungeni walionyesha wasiwasi wa Tanzania kuwa nchi ya viwanda kwa vile Serikali haielezi itajenga viwanda vya aina gani.
Gama alimtaka waziri huyo kufuta kauli yake ya kupatikana kwa soko la mihogo China kwani inapingana na mipango aliyoianisha na pia ni kuhamishia ajira nchini humo.
“Mheshimiwa Mwijage aone namna ya kufuta ile kauli. Kuna kauli moja alitoa Aprili 19, alisema anawaomba wananchi wa Lindi wazalishe kwa wingi muhogo umepata soko China,” alisema mbunge huyo.
“Sasa kwa maelezo haya, tukipeleka muhogo China maana yake tunahamisha ajira China. Kama viwanda viko China vya kuchakata muhogo kwa nini visije Tanzania?” alihoji.
Mbunge huyo alisema ni vyema viwanda hivyo vikajengwa Lindi na Songea ili mchakato wa kusindika muhogo ufanyike Tanzania na siyo China na kuwa katika hilo hatamuunga mkono.
Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Annatropia Loikila aliitaka Serikali itumie msemo kuwa “ipo siku moja Tanzania inaweza kuwa na uchumi wa viwanda” badala ya kutoa hakikisho.
“Nimeona ni namna gani tunataka kuwahadaa wananchi kwamba Tanzania itakuwa ya uchumi wa kati ifikapo 2025. Ni bora tuseme iko siku moja tunaweza kwenda kwenye uchumi wa kati,” alisema.
Mbunge wa Bagamoyo (CCM), Dk Shukuru Kawambwa alisema tangu 2008 Serikali ilipofanya tathmini ya fidia, wananchi hawajalipwa ili eneo hilo liwe huru kwa ajili ya ujenzi wa viwanda.
Hata hivyo, Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Peter Serukamba alisema Serikali ni lazima iwe na mtazamo unaoeleweka kwamba inataka kujenga viwanda vya aina gani badala ya kutoa kauli ya jumla.
“Waziri ni lazima utuambie unataka kujenga viwanda vya nini. Focus (mkazo) yetu ni nini? Tungeanza na viwanda vya sukari, mafuta ya kula na ngozi ili wakulima wetu wafaidike,”alisema.
Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Hawa Mwaifuga aliitaka Serikali kulinda kwanza viwanda vya ndani kabla ya kufikiria kujenga vipya akisema bidhaa kutoka nje ndizo zinaua viwanda.
CHANZO:-  Daniel Mjema, Mwananchi- Tuesday, May 10, 2016.

No comments:

Post a Comment