Monday, February 1, 2016

NI MWEZI MPYA: NA BLOG YA MAISHA NA MAFANIKIO IMEONA TUANZA HUU MWEZI KIHIVI:- TUANGALIE MISEMO NA METHALI TOKA TANZANIA NA MAANA YAKE....!

1. Anayetembea huokota, anayekaa huvimba tumbo (Kikerewe)
Maana ya methali hii ni kwamba riziki hupatikana kwa kutafutwa siyo kwa kukaa tu na kusubiri. Methali hii hutumika kwa wale wasiojishughulisha na kwa wale wanaojishughulisha na kufanikiwa kwa kudhihirisha ukweli wa juhudi yao

2. Atembea na moto mgongoni (Kibena)
Maana ya methali hii ni kwamba kama wewe si mkarimu, basi ujitegemee mwenyewe kwa kila kitu popote pale utakapokwenda. Methali hii hutumika kama fundisho kwamba hakuna mtu anayeweza kutenda kila jambo bila msaada wa wenzake Umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu.

3. Penye majani makavu mabichi hayawaki (Kizigua na kinguu)
Maana  yake nikuwa penye wazee ni heshima kwa watoto au vijana kuwaachia wazee wakate mashauri; ikiwa vijana watakata shauri mbele ya wazee ni utovu wa adabu. Hutumika kuwaonya watoto wawe na heshima mbele ya wazee hasa katika kusema.

4. Siku hufanana laini hazilingani (Kiha)
Maana ya methali hii ni kuwa kila mtu anayo bahati yake, leo wewe kwsho mwingine. Methali hii hutumika wakati wa kufariji mtu aliyepatwa na maafa.

5. Kichwa cha msitu (Kipare)
Maana yeke, kichwani mwa mtu kuna siri nyingi kama ulivyo msitu mkubwa. Methali hii hutumika wakati wa kuwambia watu kuwa hata kama ukifanya nini, huwezi kuzifahamu siri za mtu. Ni yeye peke yake anayeweza kuzifahamu siri zake mwenyewe. Huweza pia kutumika kwa kuwaonya watu wasiwadharau wengine wanapokuwa kimua kwani huenda wanafikiri mengi kichwani mwao.

6. Kushindwa na kufa ni mapacha (Kimasai)
Ushujaa huheshimiwa sana katika jamii kwa sababu unadumisha ulinzi wa nchi. Ushujaa na ujasiri vikipunguka maadui wa kila aina na dhiki kadha wa kadha husumbua jamii. Mashujaa wakishindwa basi jamii hufadhaika kwani mipango yake yote huvurugika. Methali hii hutumika kama onyo na pia kwa kukaza ujasiri.

7. Leo ni ugali wa kumpigia mbwa kiko cha mkono (Kisukuma)
Maana yake ni kwamba leo tunakula nyama. Mara nyingi Wasukuma hawapendi kumchinja ng`ombe bila sababu maalum. Kwa hivi hutumia mboga za majani kama kitoweo, wapatapo nyama hugawana mikononi wakati wa kula kwa hiyo hutumia kiko cha mkono kumfunza mbwa anayekaribia. Hutumika wakati mtu anapotunukiwa kitu kizuri.

8. Maneno mengi huvunja nyumba (Kichaga)
Maneno mengi nyumbani huvuruga unyumba kwa sababu mwisho wa maneno hayo ni ugomvi uletao mafarakano. Methali hii inatumika kama onyo kwa jamaa, ikiwa kumbusha kwamba maneno mengi ndio chanzo cha kugombana na kukosana.

Naona kwa leo inatosha lakini kama nawe unayo Misemo/methali usisite kuongezea...elimu ni kugawana...TUPO PAMOJA

No comments:

Post a Comment