Thursday, May 8, 2014

WAGONJWA WA DENGUE WAFIKIA 376

Na Hudugu Ng'amilo
Homa ya dengue inaendelea kushika kasi nchini baada ya takwimu za Januari hadi juzi kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, kuonyesha kuwa watu 376 wamekwishagundulika kuugua ugonjwa huo.
Mtaalamu wa Ufuatiliaji wa Magonjwa wa wizara hiyo, Dk Janeth Mugamba alisema hadi jana watu wawili walikuwa wamepoteza maisha, idadi ambayo alisema inaweza kuwa kubwa zaidi endapo upimaji utafanyika katika kila wilaya. "Pengine idadi inaweza kuwa kubwa zaidi kwa sababu wengi hawapimwi, Ijumaa (kesho) tutatoa, taarifa zaidi," alisema.
Alisema Wilaya ya Kinondoni ina wagonjwa wengi zaidi, ikifuatiwa na Ilala na Temeke. Hata hivyo, alisema huenda wilaya zenye idadi ndogo ya wagonjwa hazijaweza kupima na kubaini watu wenye maradhi hayo ikilinganishwa na Kinondoni.
Juzi, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid alisema hali ni mbaya na wananchi wanatakiwa kuchukua hadhari wasipate maambukizi ya ugonjwa huo.
Mtafiti wa malaria, tabia za mbu na mazingira, wa Taasisi ya Afya ya Ifakara, Dk Nicholas Govela alisema tayari wameshatuma maombi ya kufanya utafiti wa kina kuwajua mbu wanaoeneza homa ya dengue nchini. "Utafiti huu utasaidia kujua ni mbu kiasi gani wameathirika na virusi hivyo. Tukifanya hivyo tutajua ukubwa wa tatizo, tutajua wanapatikana wapi zaidi na virusi vyao vimetokea wapi," alisema.
Dk Govela alisema ni lazima utafiti huo ufanyike ili kudhibiti maambukizi zaidi ya homa hiyo akisema zipo sababu kadhaa zinazohisiwa kusababisha maradhi hayo, ikiwamo ya wahamiaji kuleta virusi hivyo vinavyosababisha homa hiyo na kuambukizwa kwa njia ya kuumwa na mbu.
"Ugonjwa huu umeenea zaidi nchi za Amerika ya Kusini na Kusini mwa Bara la Asia. Hapa kwetu mbu hawa walikuwapo lakini ugonjwa wa dengue haukuwapo kwa kiasi hiki, ndiyo maana sababu zinazohisiwa zaweza kuwa ni wahamiaji," alisema.
Alisema maambukizi ya homa ya dengue hutokea baada ya mtu mwenye ugonjwa huo kuumwa na mbu hao aina ya Aedes Egyptiae na mbu hao wakichukua virusi, huvisambaza kwa watu wengine. "Inawezekana tatizo ni kubwa zaidi ya hivi inavyofikiriwa kwa sababu wanaokuja hospitali kupimwa na kugundulika ni wachache, wengi wasiofika hawawezi kujulikana," alisema.
Makazi duni hatarini zaidi
Daktari Kiongozi na Mtaalamu wa homa ya dengue, Mrisho Rupinda alisema watu wanaoishi katika makazi duni wapo hatarini kuathiriwa zaidi kwa sababu ya kuwapo kwa taka nyingi na madimbwi.
Alitoa mfano wa wagonjwa wa kwanza wilayani Kinondoni, akisema walitokea maeneo ya Kambangwa, Mwananyamala Komakoma ambako kulikuwa na madimbwi na bwawa la maji.
"Wagonjwa wengi huonekana zaidi kwenye makazi duni kwa sababu ya mpangilio mbovu na kuzagaa kwa taka. Lakini pia maeneo mengine ambayo watu huhifadhi maji kwenye matenki au ndoo kwa muda mrefu bila kuyafunika," alisema.
CHANZO MWANANCHI

2 comments:

  1. Yaani nimekuwa nafuatilia huu ugonjwa kwa Tz, inasikitisha mno! Mungu atuhurumie na kutuondolea huu ugonjwa hatari mno wa dengu. Serikali na wataalamu walitakiwa kuwa waliishaanza hizo tafiti ila ndio hivyo mpaka kuanza kuomba pesa nje! Mungu ibariki Tz na watu wake.

    ReplyDelete
  2. Nakwambia... hapa nipo hoi maana ninategemea kwenda kutafuna mahindi. Kws kweli inabidi tujitahidi sana kutotunza maji machafu, katika madimbwi . Pia kuwa makini na vyandarua visiwe na matundu. Inawezekana kwa vile mwaka huu mvua zimekuwa nyingi mno.

    ReplyDelete