Thursday, February 28, 2013

TUUMALIZE MWEZI KIHIVI:- NANGOJA ANIUE, NIKIONDOKA WANANGU WATATESEKA!

Kama mnavyojua kuwa hivi karibuni nilikuwa huko nyumbani Tanzania, na nilikuwa pande za huko kwetu Ruhuwiko Songea ambapo nilikaa kama mwezi  hivi.
Kusema kweli yapo mengi ya kushangaza, ya kutisha na yenye kufurahisha ambayo niliyashuhudia, na kusema kweli kuna mengi nimejifunza. Lakini labda niseme tu kwamba aina ya maisha niliyoyakuta huko kijijini, kwa kweli yalinipa picha kwamba bado kuna safari ndefu sana katika kuufikia ukombozi wa huyu kiumbe mwanamke.
Ninayo mifano mingi lakini tukio nililolishuhudia siku moja nikiwa katika matembezi yangu liliniacha mdomo wazi, na labda niseme kwamba limenikaa hadi leo akilini nikijaribu kuwaza na kuwazua lakini sipati jibu.
Sijui nianze vipi?...Ahh! Kuna siku katika matembezi yangu nikakutana na kundi la akina mama wamekaa wakipiga gumzo, lakini nyuso zao zilikuwa zimegubikwa na huzuni. Nilishikwa na tashwishwi, nikajongea pale walipo ili kujua kama kuna jambo gani limetokea kiasi cha kuwakusanya pale huku wakiwa na nyuso za huzuni.
Si mnanijua tena mie KAPULYA MDADISI. Nikawauliza, ‘jamani ndugu zanguni, kulikoni mmekaa na nyuso za huzuni, JE KUNA MSIBA?’
Wote waligeuka kuniangalia, lakini walionekana kusita kunijibu, na ndipo mmoja wao akaniambia kuwa usiku wa jana kulitokea kutoelewana kwa wanandoa wanaoishi hapo mtaani kiasi cha mume kumpiga mkewe mpaka akapoteza fahamu.
Niliuliza sababu ya ugomvi wao, na ndipo nilipoelezwa kwamba, sababu kubwa ni kwamba wanandoa hao wana watoto wanne ambao bado ni wadogo na mume anataka kuongeza mtoto wa tano, lakini mkewe hataki kwa kuwa hali ya uchumi hairuhusu, na pia bado wanalo jukumu la kuwalea hawa watoto wanne ambao kwa kweli ni wadogo. Hata hivyo alimshauri mumewe wavute subira kwanza ili watoto hao wakue.
Mume hakukubali ushuri wa mkewe na ndipo ugomvi ulipoanza.Walibainisha kwamba ugomvi wao ni wa mara kwa mara na sababu kubwa ni hiyo ila ugomvi wa safari hii ulikuwa ni mkubwa na kama sio majirani kuingilia kati basi mume yule angemuua mkewe.
Nikataka kujua kama anapata kipigo cha aina hii kila mara kwa nini asirudi kwao?
Wakanijibu kuwa, kwanza hana nauli ya kurudi kwao kwani si mtu wa Songea. Pili anaogopa watoto wake watateseka.
Mh! Nilishusha pumzi, ujinga gani huu. Hivi sisi wanawake ni nani ameturoga, yaani unakubali mtu anakutesa na kukunyanyasa kiasi chakutaka kukutoa roho lakini wewe umo tu! Ukiulizwa sababu unadai, eti watoto wangu watateseka!
Bado najiuliza hivi watoto wanne bado hawatoshi? Hili tukio kwa kweli nimekuwa nikijiuliza tangu nirudi huku Sweden, na mpaka leo sijapatajibu kwamba tatizo ni nini? Kutokuelewa haki zetu, ujinga au ni nini?
NAWATAKIENI WAOTE MWISHO MWEMA WA MWEZI HUU FEBRUARI (PILI)

7 comments:

  1. Inasikitisha sana, inabidi kina mama tujue haki zetu kisheria ili uonezi kama huo ukitokea kushtaki kwenye vyombo vya haki. Mana hao kina mama uliowakuta wameketi kusikitika wangeweza kuchukua jukumu la kwenda kwenye uongozi wa serikali ya kijiji nadhani ingesaidia kidogo, kuliko kukaa wanazungumzia huo ugomvi bila kuwa na ufumbuzi wowote ule. Pia unamuzi wa kuondoka unawezekana ila nao ni mgumu, mana pia unakoenda kama ndio wanakutgemea!, sijui inakuwaje hapo? Na kuacha watoto ni ngumu kwani kina mama tumeumbwa na huruma sana hasa kwa watoto wetu. Hii ni mitihani ya maisha. Mungu atusaidie. Kina mama mpo? Unajua mama mwenye kipato ni rahisi kuondoka tena na watoto kulikoni anayemtegemea mume wake kwa kila kitu. Pia kina mama wa vijijini wanahitaji kukombelewa au kuelemishwa hasa kuhusu haki zao. Dada Yasinta tuanzishe NGO ruhuwiko ya kuelimisha kina mama kuhusu haki zao? Kusanya kusanya basi jiweke vizuri na tulifanyie kazi hilo swala. Baadae tunatafuta na wafadhili Sweden, eh unaonaje? Mana sisi ndio wa kuwasaidia kina mama na sio mtu mwingine toka mashariki ya mbali au unasemaje?

    ReplyDelete
  2. Yasinta wakati mwingine kuondoka sio tija ya kutatua tatizo. Ila kutafuta njia muafaka za ufumbuzi. Mie nilidhani wewe ungewashauri waende kwenye serikali ya kijiji, au vyombo vya sheria na haki za kina mama kulikoni kuwaacha tu! Au wewe yasinta ungechukua jukumu la kutafuta wapi haki ya huyo mama inaweza kupatikana na kuchukua mawasiliano yao na ukaulizia hapo songea, then ukarudi kwa hao kina mama na kuwaambia muende sehemu fulani mpeleke hilo tatizo na hata kwa mwingine ikija tokea hivyo wangekuwa tayari na pa kupeleka shida zao. Wakati mwingine sie kina mama tunaonajua vitu fulani ni vizuri kuelimisha, kushauri ili kusaidia, sasa wewe unasema eti nashangaa kwa nini asirudi nyumbani? Mh Yasinta wewe unaishi nje ungeweza japo kutoa msaada fulani, wa mawazo, ushauri au hata kutafuta wapi wanaweza kupeleka hiyo shida, kwani sasa walipokwambia umeishia kushangaa! eti kwa nini asiondoke ukidhani ni kitu rahisi sana! Jitahidi ukienda nyumbani usaidie na wengine kwani huo utakuwa mchango wako mkubwa ukizingatia unaishi nje na umepata elimu nje hivyo ni vizuri ukaitumie vizuri kwenu. Hata ukirudi sweden kina mama wangeendelea kukutafuta na kukumbuka juhudi zako. Usikubali kuambiwa tatizo na kulirudisha kama lilivyo bila kutoa tija yoyote ile, mana nawe unakuwa huna tofauti nao kimawazo wakati si kweli! Samahani nadhani sijakukwaza ni mtazamo wangu tu. Nimeiweka kisomi zaidi.

    ReplyDelete
  3. Mliotangulia Aanteni kwa Maoni yenu ...Wanawake wa Afrika wanahitaji ukombozi.

    Asante KADALA kwa hili ukichukulia tunaelekea SIKU YA WANAWAKE.

    ReplyDelete
  4. Kweli wanawake tukiamua twaweza hapo juu naunga mkono.

    ReplyDelete
  5. PM..nimeyapenda maoni yako na wala hujanikwanza hata chembe. Labda niseme hivi wanawake ni watu wa huruma sana na usidhani niliachia hapo tu lakini mwanamke akipenda anapenda hata apigwe kama nini na kabisa akishakuwa na watoto ndo inakuwa ngumu zaidi kumpa ushauri. Wazo lako nimelipenda sana ambalo zinazunguka kichwani kwangu kila kukicha lakini kwanza inatakakiwa wanawake wenyewe tujitambue kwanza na pia kuwa wapesi kupokea ushauri ...PM..ningefurahi kama ningejua kirefu cha jina lako..natanguliza shukrani.
    Kachiki..Rachel.. Huwezi kumkomboa mtu kama hawezi kukombolewa...

    Shalom..Ni kweli kabisa tukiaamua twaweza hakuna kichowezekana hapa duniani.

    ReplyDelete
  6. Mwanamke anakomboka jamani, sio kuwa hataki ni kuwa anatakiwa kupata elimu ndogo tu, kujua wapi aende..wapi atasaidiwa...na haki yake ikoje. Wanawake wengi hawajui haki zao, hawana elimu ya kutosha. Unajua kwenye hilo tatizo hata akienda kwenye vyombo vya haki akaambiwa si na mumewe ataambiwa aende naye, wote wakielezwa pamoja nadhani mumewe anaweza kuelewa na kujua kuwa alikuwa anakosea..na maisha yakaendelea tena kwa amani tu. Kwenda kwenye haki na kuelimishwa sio kuwaachanisha hata kidogo. Ila mume akiwa kaidi na sio muelewa hapo labda hatua zingine zinaweza kuchukuliwa ili kumsaidia/ kumkomboa huyo mama. Mada nzuri sana. Wanawake na maendeleo. Kujitambua si mpaka apate elimu fulani, yani asipopata watu wa kumpa hiyo elimu hawezi kubadilika inakuwa ngumu hivyo mimi na wewe tunaweza kabisa kumsaidia kwa kukaa chini kumuelezea na mpaka mnakubaliana mie naamini watabadilika tu.

    ReplyDelete
  7. Usiye na jina wa 11.06...Ahsante sana kwa maoni yako ..Nakubaliana nawe wanawake wanahitaji haki ya kuelimishwa..ni wanawake wote duniani si hapa Afrika tu maana wengi wanafikiri ni Afrika tu wanawake wanaonewa....kwa mtindo huu wa kuelimishwa hakika hata miminaamini kunaweza kuwa na mabadiliko...Ahsante kwa kuona mada nzuri pia.

    ReplyDelete