Monday, January 28, 2013

KWANGU MIMI ILIKUWA NI KAMA NDOTO....!

Jana wakati nipo kazini nilipata nafasi kidogo na kupita hapa kwenye kibaraza cha kaka yangu mzee wa Utambuzi. Nikakutana na kisa hiki hapa kwa kweli kilinigusa sana kiasi kwamba nimeona niweke hapa na wengine msome...haya karibuni.......
...............................................................................................................................................
Hadi leo naona kama ndoto.............!
(Picha haihusiani na habari hii.)
Nakumbuka ilikuwa ni mwaka 1991 wakati huo nikiwa nafanya kazi kwa mtu binafsi, Muasia mmoja. Nakumbuka katika mojawapo ya majukumu yangu, nililazimika kwenda Nairobi nchini Kenya. Nilikwenda huko kikazi na nililazimika kukaa kwa mwezi mmoja. Nilipomaliza kazi ile, niliamua kukaa kama siku tatu zaidi ili kujionea hali ya Kenya ilivyo. Nilizunguka jijini Nairobi na kwenda maeneo ya karibu kama vile Thika, Kinangop na miji mingine iliyo karibu na jiji hilo maarufu katika ukanda huu wa Afrika Mashariki.
Siku moja wakati natoka kwenye matembezi yangu nje ya jiji hilo la Nairobi, nilikutana na mtu mmoja. Huyu bwana alikuwa anaonekana kuchoka sana, ama kwa kuumwa au kwa njaa. Nilikaa naye kiti kimoja kwenye Matatu, yaani daladala za Kenya. Huyu bwana alikuwa ananitazama mara kwa mara na kujitahidi kutaka kama kutabasamu, ingawa hakumudu sana.
Niliingiwa na huruma na kulazimika kumuuliza kama alikuwa yu mzima wa afya. Alisema anaumwa na hana hata senti tano ya kulipia matibabu yake. Nilimuuliza kama anao ndugu. Alisema hana na familia yake iko mashambani, ambapo haina kitu kabisa. “Nina watoto watatu mmoja amemaliza shule hana kazi na wawili wanasoma, lakini ni kwa mashaka sana, kwani mara nyingi hurudishwa nyumbani kutokana na kukosekana ada.” Aliniambia.
Ilibidi nimchukue yule bwana hadi hospitalini ambapo alichukuliwa vipimo. Aliambiwa arudi kesho yake kuchukua majibu yake. Tuliagana tukutane pale hospitalini kesho yake. Kwa kweli hakuamini kwamba, nilimfikisha hospitalini na kumlipia matibabu. Hakuweza hata kushukuru na nilielewa ni kwa sababu gani. Mshangao ulikuwa ni mkubwa sana kwa upande wake.
Kesho yake alipata majibu yake ambayo yalionyesha kwamba alikuwa na maji kwenye pafu moja pamoja na kifua kikuu. Ilibidi aandikiwe dawa. Hakuwa na fedha kabisa. Ilibidi nitoe fedha zote za matibabu yake. Ilikuwa kama silimia 20 ya pesa zote nilizozipata pale Nairobi kama posho. Lakini hiyo haikunisumbua. Nilikuwa najisikia vizuri kuona angeweza kupona.
Ilibidi niombe ruhusa ya siku saba zaidi ili nikae Nairobi kukagua hali ya yule jamaa. Wakati huo huo nilimwambia kwamba, kama anaweza kumwita mkewe akae naye pale mjini wakati anatibiwa ingekuwa vizuri. Nilimwambia ningemsaidia pesa kidogo za kumwezesha mkewe kukaa naye angalau kwa siku kadhaa. Alikubali na kumwita mkewe. Mkewe alipofika hakuamini kwamba niliweza kumsaidia mumewe vile. Yule mama alilia sana na aliniombea sana kwa kikwao, yaani Kikikuyu kwa majina ya mizimu yote. Nilijisikia furaha kwa namna mke wa jamaa alivyojisikia vizuri kuona mumewe amepata matibabu.
Niliondoka Nairobi siku ya tatu tangu mkewe kuja. Niliwaachia hela kiasi cha shilingi 14,000 za Kenya, ambazo nilimwambia yule mama zingemsaidia kufanyia shughuli yoyote ambayo ageona inafaa. Niliondoka bila hata kuwaachia anuani yangu wala simu yangu. Labda wao walitegemea ningewapa anuani yangu, lakini sikufanya hivyo. Mimi sikuona sababu ya kuwapa kwani, niliwasaidia kama binadamu ambao wanahitaji msaada wangu, siyo ili wanijue au tuwe marafiki.
Hivyo ndivyo nilivyo hata leo. Sijisifu kwa sababu sioni kuwa ni sifa, bali naona kila binadamu angetakiwa kuwa hivyo, ila basi tunazuiwa na choyo ya kufundishwa. Sikuwahi kusoma kuhusu masuala ya kusaidia na kupata furaha wala kumsikia mtu. Tabia hii nilitoka nayo kwetu, niliitoa kwa baba yangu ambaye, alikuwa mtu wa kusaidia sana bila kujali malipo. Hilo nalijua.
Mambo yangu yalienda vizuri hadi mwaka 1994. Mwaka huo nilipoteza kibarua change na hata shughuli zangu zikawa zimepoteza umaarufu kutokana na mabadiliko ya teknolojia. Ilibidi nianze kuhangaika. Kufikia mwaka 1996, nilikuwa hoi bin taabani kiuchumi. Watoto wangu watatu wakawa hawaendi tena shule, hakuna ada. Tulishindwa kulipa kodi ya nyumba, ambapo ilibidi tufukuzwe na kwenda kuishi kwa ndugu wa mke wangu. Huyu naye hatukukaa hata mwezi masimango yakaanza. Siwezi kumlaumu, kwani kusaidia siyo jambo rahisi, ingawa naamini ndipo mahali furaha ya binadamu ilipo.
Tulilazimika kuhama na kwenda kuishi Mtoni Kijichi. Huko hatukuwa tumepanga. Jamaa yangu mmoja alikuwa anajenga kule na alikuwa anataka mlinzi, ambapo nilimwambia ningefanya kazi hiyo. Hivyo tukawa tunaishi kwenye kibanda cha mtumishi. Lakini tulihisi nafuu. Hata hivyo watoto wote walisimama shule, kwani hata nauli ya kuwapa ili waende shule ilikuwa ni vigumu.

4 comments:

  1. "Kuna jambo naomba sana nikusaidie kulifahamu. Hili ni jambo ambalo linaonekana halina maana, lakini ndio ubinadamu wenyewe. Jitahidi sana popote ulipo kuwasaidia watu, bila kujali kama watakukumbuka au kukulipa ama hapana."

    ReplyDelete
  2. Kaka Ray! yaani hapa ni bonge la darasa na asiyejifunza kitu hapa basi tu...

    ReplyDelete
  3. Thank you for the auspicious writeup. It
    in truth was a leisure account it. Glance complex to more delivered agreeable
    from you! However, how can we be in contact?
    My web site ... diet that works

    ReplyDelete
  4. Dada Yasii;
    Hapa nakumbuka ule msemo wa kale:"Ubaya hauna kwao lakini wema hauzoni".["Ubaya hauna nyumba lakini wema una makazi"].

    ReplyDelete