Monday, December 27, 2010

MUDA UNAPITA,LAKINI.....

‘Bwana wewe nikuambie siri moja ya maisha,…’Mzee mmoja alikuwa kaka karibu nami kwenye daladala kaniambia, tulikuwa tumekaa wote kwenye daladala na muda huo nilikuwa nimechoka, sikupenda kusumbuliwa, hamu yangu ilikuwa kupata usingizi kidogo, kwasababu najua nina zaidi ya masaa mawili ndani ya daladala hadi kufika kwangu, siunajua tena foleni.


Nikamwangalia yule mzee, alikuwa kaniangalia kuonyesha kuwa ana jambo muhimu nikaona nimsikilize na kumwambia , `Niambie mzee, huenda likanisaidia katika maisha yangu…’

‘Katika mipangilioa yako ya maisha , fanya juhudi pangilia mambo yako, fanya kazi kwa bidii na ipende dunia kama vile utaishi milele..siunaniona mimi hapa nimezeeka nina miaka sitini, lakini najihisi kama nina miaka mingine sitini mbele, sijipweteki, na kusema aah, mimi mzee basi tena, nasubiri cha kupewa, nani atakupa hivihivi dunia hii. Najitosa hivyohivyo kama vile nitaishi milele, ingawaje kwa kweli naukumbuka sana, na kuujutia ujana wangu…’ akaniangalia kwa macho makali. Akaongezea kusema `wakati ni mali, lakini wakati ni ukuta, unahitaji mipangilio…’ akatikisa kichwa na kuendelea kusema;

`Pili muabudu sana mungu wako kama vile utakufa leo, au hata sasa hivi, huwezi jua, hapa gari linaweza likadondoka, tukawa wote marehemu au nikafa mimi peke yangu, au hata bila kudondoka gari unaweza ukakauka ghafla, na ukafa. Sasa ni bora umwabudu aliye na mamlaka na hiyo roho yako kwasababu hujui muda gani ataichukua roho hiyo. Omba, muabudu mola wako kama vile hapo unapoomba ni sekunde au dakika yako ya mwisho…’ akainama chini na nilijua anamuomba mola wake!

Nilijiukuta nimelala na nilipoamuka yule mzee akawa hayupo, ina maana aliteremka kituo nyuma wakati mimi nimelala, nilijuta sana, kwani alionekana ana busara na mengi yakunieleza, lakini nimechelewa keshaondoka.

Mzee huyu namfananisha na mwaka huu, unayoyoma, ni muda mchache umebakia tutauita jina jingine, mwaka jana au sio , na tutaukaribisha mwaka mpya. Mwaka huu tulikuwa nao na tulikuwa na mengi ya kufanya, na sijui mangapi tulifanikiwa kuyafanya na mangapi hatukufanikiwa, sidhani wengi wetu tuna kawaida ya kuweka kumbukumbu hizo, sidhani. Kumbukumbu hizo tunaziona kwenye bajeti za serikali, bajetiza makazini, lakini sio bajeti ya mtu mmoja mmoja.

Mwaka huu tupo nao kwenye kiti una mengi ya kutuambia, lakini tunajifanya tumechoka, tunajifanya tupo busy…labda tungelitulia tukatafakari na kuwa nao bega kwa bega k wa mipango, huenda tungelifanikiw sana. Tumekuwa tukikimbizana na hili na lile na huenda hayo tunayokimbizana nayo haya maana, tunapoteza muda mwingi kwenye vilevi, kucheza bao, kuongea na kufanya mambo ambayo ukiangalia ni ya kupotezea muda, muda uishe ulale, siku ipite. Ndio siku inapita, umri unakwisha na mwaka huo unakwisha, tukiamuka tutaukuta haupo tena!

Tukiangalia katika maisha yapo mambo mengi yanaharibu miili yetu hasa vyakula, vinywaji, vipodozi, hasira zisizo na msingi na mambo kadha wa kadha ambayo unayaona mazuri kwa umri wa miaka hadi telathini ujanani yaani, lakini ukifikia zaidi ya umri huo, hayo hayo uliyokuwa ukiyaona mazuri yanageuka kuwa sumu mwilini mwako. Mfano vyakula vya mafuta, pombe, starehe , madawa, vipodozi na mambo anuai, ni mazuri, yanastarehesha katika umri wa ujanani, lakini ikifikia uzeeni hayo matamu yanageuka kuwa machungu, yanakuwa sumu. Tunajikuta tunaamndamwa na presha, kisukari, ugonjwa wa moyo, vidonda vya tumbo nk, kwasababu ya yale matamu tuliyokuwa tukiyafadi ujanani. Kosa hatukua na mipangilio, hatukuali kusoma na kujifunza uzuri na ubaya wa hilo unalilofanya au kula!

Sasa wakati umefika kabla mwaka haujaisha kaa na huu mwaka kabla haujaisha, kumbuka yale ya muhimu, panga matarajio ukiwa na malengo kuwa utaishi milele. Na mipango hiyo haiwezi kuja kichwani tu, chukua karatasi pata muda, hata ikibidi soma, tafuta , uliza, kaa na mkeo au mumeo, angalieni matarajio, majukumu na mambo mbali mbali ya kimaisha yapangeni vyema na jinsi gani ya kuyatatua matatizo, jinsi gani ya kupata kipato, jinsi gani ya kusaidiana na hata kama huna kitu lakini kwa kujua nini kifanyike na kipi cha muhimu kwanza inasaidia, kuliko kulala, au kunywa pombe, au kusubiri mwisho wa siku ukaanza kupiga mayowe , kurusha mawe kwenye mabati eti unashagilia mwaka umekwisha, lakini umekwishaje? Ulikuwa nawo kweli wewe au ulikuwa umelala…!

Mkumbuke mola wako, kwani imani ni kitu muhimu sana, mola wako ndiye mwenye mamlaka na mwili wako, wangapi ulikuwa nawo siku za karibuni au mwaka huu sasa hawapo, je ina maana wao walikuwa na makosa na wewe uliyebakia huna makosa. Kumbuka wangapi wapo mahospitalini wagonjwa, wengine hawana viungo, wengine wanaomba mola awachukue kwa mateso wanayopata ya kansa au mengineyo, je wao walikuwa wanjua haya, je wao walimkosea Mungu ndio maana wanapata mateso haya, na wewe ni mbora zaidi yao ndio maana leo upo mzima. Hapana, wao hawajakosa, na wala wewe sio mbora sana mbora zaidi ni yule mcha mungu, ni yule anayemuomba mungu kuwa sala yangu hii huenda ikawa ya mwisho kuwa mzima, kuwa hai…nahivyo Sali kama vile hutaiona sekunde inayofuata.

Ujumbe huu nimetumiwa na msomaji wa Maisha na Mafanikio aishiye Arusha. Binafsi umenigusa sana nimeona nisiwe mchoyo niwajumuishe na wenzangu.

6 comments:

  1. Yasinta nimeguswa sana na maongezi ya mzee kwenye daladala,bila kufundishwa na mtu nilikuwa naumia sana mwisho wa mwaka na kujikuta sikutimiza malengo yenye manufaa hata moja katika mwaka ule, kwa maisha yangu. Mimi nilikuwa nahesabu lazima niwe nimefanya jambo la maana hata kama kubeba mimba na kushirikianana uumbaji na mungu katika mwaka ule naihesabu kama ni baraka kwangu pia nahesabu kunakitu cha maana katika mwaka ul nilichokifanya. Hivyo hata tendo dogo ni la maana kwangu nalihesabu ni baraka tele ili kuukomboa wakati. Kama mzee alivyosema wakati ukuta bali hausubiri. Hivyo ni busara kuukomboa na kufanya la maana kila mwisho wa mwaka kujiuliza umefanya nini cha maana kwa ajili yako kipindi upo hapa na kwa mungu wako. Mungu akubariki Yasinta kwa ujumbe mzuri sana huu

    ReplyDelete
  2. Maneno ya busara sana na yanagusa katika ile tabia yetu inayokera ya kumakinikia mambo ambayo wala hayana tija sana katika maisha yetu japo kwa wafuasi wa falsafa ya Existentialism watadai kwamba kila jambo alifanyalo binadamu hapa duniani lina tija - hasa ukizingatia kwamba anao muda mchache tu kabla hajaingia katika mdomo wa kifo (ponda raha kifo chaja!)


    Tuyazingatie haya hasa katika wakati huu tunapojiandaa kuingia katika mwaka mpya. Nyote barikiweni!

    ReplyDelete
  3. Dada Yasinta asante sana kwa ujumbe huu mzuri, na kwaujumla mimi nimeguswa sana na kipengele cha familia kwa vile mimi binafsi ni mama wa familia.Kwa kweli mipango ni kitu muhimu sana ktk maisha ya mwanadamu yoyote ila kwa sisi waafrica ni wachache sana wenye utaratibu huo, hivyo hii ni changamoto uliyotupa ili mwaka ujao tujipange kila familia iangalia je ilikosea wapi kwa mwaka uliopita,je ni lipi liliofanikiwa na nini cha kufanya ili mwaka ujao mafanikio yaongezeke zaidi.
    Jambo lingeni lililonigusa ni moyo wa kumjua Mungu, najua wengi wetu hasa tukiwa na maisha mazuri tunamsahau Mungu na kujua kuwa wakati wa kumuita ni wakati wa matatizo tu! la hasha ni vema kwa kila anayeamini kumcha,ili milango ya baraka izidi kumiminika ktk mwaka wa bwana unaokuja.
    Kuna familia nyingi hazina amani,wanagombana,awaongei hawashirikiani kwa lolote wanaitwa Baba na mama kwa nje tu,lakini wakiingia ndani kila mtu anakunja mdomo, niwakati sasa wa kuacha yote hayo na kukumbuka kwamba sisi wote ni wapitaji, hata umfanyie ubaya mumeo au mkeo au ndugu yako haisaidii,unapoteza muda tu, ni bora kila aliyeumbwa na Mungu akaishi maisha ya furaha na upendo.
    Asante sana.

    ReplyDelete
  4. Ujumbe poa!

    Nafikiri ni M3 ndio aliyeuandika ujumbe huu pale kwake chini ya kichwa :


    Wakati ni mali,lakini_

    Tarehe 24/12/2010

    ReplyDelete
  5. Habari
    Ni kweli hiki ni kipindi cha kukaa na kufanya tafakari ya kina juu ya nini umefanya,na ufanikiwa kwa kiasi gani au la umejifunza nini ili ujipange vizuri kwa mwaka unaofuata.

    Si vibaya ukajikagua na kuona nini umefanya na kwa kiasi gani
    Baada ya yote ni kufanya uamuzi na kutenda tena natena bila ya kuchoka.
    Tunacojifunza kutoka katika mzee aliyekuwa katika daladfala kuwa katika maisha hakuna nkuchelewa bali kuna kuamua na kutenda kwa nia ya dhati na dhamira badala ya kuwa orodha ya matumaini katika mambo ambyo hautayafanyia kazi.
    Kila la kheri tubadilike tutende zaidi kwa mkabala wa kuweza na kufanikiwa tunashinwa kufikia matarajio yetu tusivunjike moyo na kukata tamaa badala yake tujipe shime.

    Kila la kheri

    ReplyDelete
  6. MMMh, ujumbe murua huu, nshukuru kuwa umekwenda mbali zaidi, nashukuru kuwa umegusa jamii, na wengi wameupenda.

    ReplyDelete