Monday, September 6, 2010

‘Housigeli’ anataka kuniharibia ndoa

Mama mkwe
habari yako. Nategemea mzima wa afya na hutasita kunisaidia kunipa ushauri unaonifaa. Mimi ni mwanamke mwenye watoto wawili. Tangu nimeolewa miaka sita iliyopita, nimekuwa na msichana wangu wa kazi mmoja ambaye nimempenda sana hasa kwa kuwalea vizuri watoto wangu na kuwa mwepesi wa kazi. Kutokana na kuishi vizuri na ‘housigeli’ huyu, amekuwa kama mtoto wa nyumbani na hata ndugu zangu na wa mume wangu wanampenda sana na wamemzoea kupita kiasi.
Tatizo hili la kuwazoea ndugu wa mume wangu sasa naona linataka kuharibu ndoa yangu kwani huyu msichana ameanza tabia mbaya na amemweleza mkwe wangu kuwa mimi situlii nyumbani na sina muda wa kumshughulikia mume wangu kwani kazi zote anafanya yeye, mimi kazi yangu kusafiri na kushinda kazini. Huyu mama mkwe wangu kusikia hayo, amekuja juu na sasa anamshinikiza mume wangu aniache eti nashindwa kuhudumia nyumba na badala yake amuoe ‘housigeli’. Mume wangu ameshtuka na amenieleza kila kitu hali iliyonikasirisha sana.
Sasa naomba ushauri wako kwani mama mkwe bado yupo kwangu, je, nifanyeje kabla hajaondoka kurudi kwake? Mama Kelvin Tabata, Dar es Salaam. Mama Kelvin pole sana kwani inaonekana huyo mama mkwe wako hajaelimika vya kutosha. Uzuri wa mwanamke haupimwi kwa kazi za nyumbani pekee, bali kuna mambo mengi na mkwe wako anapaswa kutambua kuwa wewe unafanya kazi hivyo huwezi kukaa nyumbani muda wote na ndiyo sababu ukatafuta msaidizi.
Lakini pia ni vyema ukiwa nyumbani ufanye kazi zilizopo ikiwamo kumpikia mumeo na kumhudumia ipasavyo. Usiwe na hasira za haraka kwa msichana wako wa kazi kwani inawezekana aliulizwa kimtego naye akajibu vizuri tu lakini mkweo akawasilisha kwa mumeo vibaya. Nadhani mumeo pia anapaswa amweleze mama yake kwa upole kuwa wewe unafanya kazi na huwezi kufanya kazi zote za nyumbani. Pia amweleze kuwa huyo msichana wa kazi kamwe hawezi kuwa mke wa mtoto wake.
Naamini mtoto wake akimwelimisha na akawa na msimamo, mama mkwe wako ataelewa au hata kama hataelewa, atashindwa kuendelea kusisitiza anachotaka. Ni vyema pia ukakaa na mshichana wako na kumhoji ilikuwaje hata wakazungumza hayo na mkweo na ukiona kama alichokonolewa basi mtahadharishe akae mbali na mama mkwe na asiwe mwepesi kueleza mambo ya ndani ya nyumba kwa mkweo.
Hata hivyo fanya uchunguzi wako kwa siri na ukiona msichana wako anapalilia ili aolewe yeye, basi ni vyema ukatafuta msichana mwingine wa kazi na huyo kumwondoa ili asije kuharibu ndoa yako. Haina haja kugombana na mtu yoyote kwani naamini huyo mkweo ataondoka na nyinyi mtaendelea na maisha yenu. Pia jifunze kuvumilia kwani wakwe wengine uelewa wao ni mdogo.

Habari hii nimeipata jamii forum na nimeona si vibaya kama nikiweka hapa Maisha na Mafanikio.

5 comments:

  1. Haya matatizo ya wafanyakazi wa ndani sasa yamekuwa yakizidi kila siku! Nakumbuka kwa watu wa imani watanisaidia kuna binti mmoja alienda kwa baba yake kumuomba amtafutie mfanyakazi wa ndani.
    Baba yake alimwambia, ni bora kuumia kwa kazi kuliko kuwa na mafanyakazi wa ndani, kwani mitihani yake ni mikubwa.
    Na kweli tunayaona haya.
    Kwa ushauri wangu ni kwa huyu dada kujitahidi kuwa karibu sana na mume wake, kwani wakipendana wawili wengine hawana nafasi. Hakikisha unampagawisha mume wako iwezekanavyo...wewe unajua bwana, usijaribu mtu kukunyang'anya ukipendacho!

    ReplyDelete
  2. Duh!!! pole sana, huyo beki tatu ni wakufukuza halafu na wewe kama kuna sehemu unazembea kwenye majukumu yako nyumbani basi jirekebishe fasta

    ReplyDelete
  3. Kwanza mumeo anakupenda

    Pili jitahidi unapokuwa nyumbani ujishughulishe au umuangaikie mumeo

    Tatu mface mama mkwe na umwambie kwa upole kwamba unajua alicho shauri na hauko tayari.

    Nne mruhusu mdada aondoke akafanye kazi kwingine apate umaarufu kama huo tena

    ReplyDelete
  4. Kwanza pole sana kwa yaliyo kkuta unajua kwenye ndoa lazima uwe mvumulivu alafu mama wakwe wengine huwa hawana busara kwasababu hicho alichokifanya kwa kumwambia m umeo si vizuri hata kama ungekuwa wewe umemfanyia hivyo kwa mumewe angefurahia chamsingi kwasababu mumeo ameamua kuwa wazi kwako house girl hakufai kwenye nyumba yako alafu kinginekila kinacho muhusu mume wako fanya mwenyewe na si house girl Unajua ndoa nyingi zinavunjika wsababu ya house girl mimi hapa mwenyewe huwa najitahidi sna kufnya kila kinachomuhusu mume wangu nafanya mwenyewe na mimi ni mfanyakazi kwahiyo usibweteke hata anaweza kufanya makusudi kwenye chakula kwenye kufua kwenye kunyoosha ili uwonekane mbaya kwa mumeo TAKE CARE SI UNAKUMBUKA KIAPO CHA NDOA .

    ReplyDelete