Nakushuru sana Mungu, mema umenijalia,
Ewe muumbaji wangu, sifa nakurudishia,
Bariki maisha yangu, uniangazie njia,
Nasema ahsante sana.
Nakushukuru sana mama, kwanza ni kwa kunizaa,
Umenilea kwa wema, kwa nyota inayong'aa,
Nitashukuru daima, umeniwashia taa,
Nasema ahsante sana.
Nakushukuru mwandani, mpenzi wa moyo wangu,
Kwangu unayo thamani, kwani u sehemu yangu,
Daima uwe pembeni, sitoweza peke yangu,
Nasema ahsante sana.
Ndugu nawashukuruni, mnanithamini sana,
Tangu mwangu utotoni, tungali tukipendana,
Ninawapenda moyoni, na mbarikiwe sana,
Nasema ahsante sana.
Nashukuru marafiki, Mungu amenijalia,
Tungali tupo lukuki, pamoja twafurahia,
Kwa raha ama kwa dhiki, ndani ya hii dunia,
Nasema ahsante sana.
Siku niliyozaliwa, ambayo naadhimisha,
Furaha niliyojawa, ninyi mmesababisha,
Kwa umoja tumekuwa, imara kwenye maisha,
Nasema ahsante sana.
Upendo ndiyo silaha, hakika tunapendana,
Upendo una furaha, kweli twafurahiana,
Na hivyo huleta raha, raha kifani hakuna,
Nasema ahsante sana.
Ahsante pasi kipimo, nawashukuruni sana,
Upendo pasi kikomo, ninawapendeni sana,
Furaha tele iwemo, maisha marefu sana,
NASEMA AHSANTE SANA.
Nawashukuruni sana, mara zisizo na idadi kwa upendo wenu muuoneshao kwangu, siku zote. Ninatamani kusema maneno mengi kuonesha wingi wa furaha na shukrani zangu kwenu, lakini maneno hayajitoshelezi. Ninasema, nawashukuruni sana, ninawapenda sana, na ninawaombea furaha na mafanikio daima.
Pamoja sana.
Shairi hili limeandikwa tarehe 14/11/2009 na mtani wangu Fadhy Mtanga ukitaka kusoma mashairi yake zaidi tembelea hapa. Nakuhakikishia hutapenda kukusa kutembea mara kwa mara.
Kaka Fadhy ni shairi nzuri sana na ningependa watu wengi wapite hapa na kusoma mashairi yako.Ahsante sana!!
ReplyDeleteNasema ahsante sana
ReplyDelete