Sunday, May 2, 2010

Ujumbe wa Jumapili ya leo:- Mwanangu!!

mama na mwana (Yasinta na mwanae)

Shairi hililimenigusa sana na ndio maana nimeamua kuwaka hapa kibarazani kwangu kama huamini soma na utaona utamu wake.
Mwanangu uketi chini, mambo haya nikwambie,
Nisikie kwa makini, kichwani yazingatie,
Usiyaweke pembeni, kazi ukayafanyie,
Mwanangu hii dunia, yahitaji umakini.

Mwanangu wajuwe watu, uishi nao vizuri,
Jifunze kuwa na utu, utende kwa kufikiri,
Usiwadhulumu katu, wemawo uwe hiyari,
Mwanangu katende wema, usingoje shukrani.

Mwanangu wacha papara, wende mwendo taratibu,
Itangulize busara, hata panapo majibu,
Jisafishe yako sura, uepuke majaribu,
Nawe wonekane vema, uwe na yako staha.

Mwanangu wewe ukuwe, ili uje kuyaona,
Siyo majumba ya Kawe, ama jiji kubwa sana,
Bali ukayaelewe, maisha kila aina,
Yenye watu ndani yake, wenye vitu ndani yao.

Mwanangu si lelemama, maisha ni kupambana,
Kuna watu waso wema, kwa macho hutowaona,
Ikuze yako hekima, nayo ikuchunge sana,
Maana ndiyo silaha, dunia yajaa hila.

Mwanangu kuza imani, umtegemee Mungu,
Sidhulumu masikini, ukavunja chake chungu,
Uzidishe umakini, kwao hao walimwengu,
Dunia wala si mbaya, wabaya ni walimwengu.

Mwanangu ujihadhari, na vicheko midomoni,
Mioyoni si wazuri, wala usiwaamini,
Wajichimbia kaburi, wewe kufukiwa chini,
Marafiki wasaliti, ndivyo iwavyo daima.

Mwanangu hii dunia, imejaa uhadaa,
Mambo yakikunyokea, marafiki wanajaa,
Siku yakikuchachia, wote wanakukataa,
Kwao urafiki vitu, bilavyo hakuna pendo.

Mwanangu chunga kauli, pindi unapoongea,
Penda kusema ukweli, mema ukayatetea,
Uepuke ubatili, ubaya sije endea,
Mdomo ndio ubao, watu ndipo hukusoma.

Mwanangu nakushukuru, najua umesikia,
Ninakuombea nuru, Mola kukuangazia,
Mola atakunusuru, na mabaya ya dunia,
Mwanangu uishi vema, maisha kufurahia.



Kila mzazi anapenda mwanawe awe na wakati mzuri maishani. Bado sina mtoto, lakini nimejaribu kuvaa uzazi na kuandika tungo hii. Naamini kila mzazi huwa anamfundisha mtoto wake namna bora ya kuishi na watu duniani. Shairi hili ni zawadi kwa wale wote ambao ni wazazi.



Shairi limetungwa na Fadhy Mtanga ukitaka kusoma mashairi yake zaidi soma hapa nami nimevutiwa nikaona niweka hapa ili tujifunze kwa pamoja. NA NAPENDA KUWATAKIENI WOTE JUMAPILI/DOMINIKA NJEMA. NI JUMAPILI YA 18 YA MWAKA HUU NA YA KWANZA YA MWEZI HUU WA TANO!!!!

9 comments:

  1. Ahsante, nawe pia.... Lakini hiyo picha.... Inanikumbusha wakati nafanya kazi Ngorongoro :-(

    ReplyDelete
  2. Ahsante sana dada Yasinta. Mungu akubariki sana.

    Nashukuru kwa heshima ya kipekee kibarazani pako.

    ReplyDelete
  3. Mimi si Mwanamashairi, ila nimevutiwa na hii picha, na ulivyolifagilia hili Shairi, nitakuja hapa kibarazani kwako badae nisome kwa utulivu. Jumapili njema nawe!

    ReplyDelete
  4. Mwanangu Yasinta kua, kuwa uyaone.
    Dunia hii ni chungu, mfanowe shubiri
    haihiaji kusimuliwa, naamini umeyaona,
    Amini nakwambia, dunia hii haitaki ndweo,
    Na kama huamni, basi kamuulize Matondo,

    Mwenda mbwani Ngali usu, walisema wahenga,
    na kila mla kuku wa mwenzie, miguu humwelekea.
    Katu usidhulumu, na wala usichukue cha mtu,
    Ukitaka kuishi vyema, yakupasa uache maringaringa.

    Shairi hili limetungwa na Koero.....LOL

    ReplyDelete
  5. Ujumbe wa Shairi hili unamgusa kila mtu sio wenye watoto tu. ni nyenzo nzuri ya kutengeneza maisha yenye usalama. Asante fadhy, Asante Yasinta.

    ReplyDelete
  6. Asante sana Dada Yasinta kwa ujumbe mzuri na wakuvutia, hata mimi si mwana mashairi lakini ni ujumbe ambao nimeupenda sana, pia nakumbuka sana Mama yangu alikuwa akisisitiza karibu kila siku, ukiwa mcheshi na mwaminifu utaishi na watu wote duniani bila shida yoyote na utajisikia upo nyumbani tu. Nami kweli nimeamini sana mafundisho haya. Umenikumbusha mbali sana asante sana.

    ReplyDelete
  7. Dada Yasinta!

    Kama ni wewe kweli katika picha hiyo, basi utakuwa bomba sana.

    Picha hiyo inaonyesha ni jinsi gani mwanamke wa kiafrika alivyomzuri, sio kwa sura pekee yake bali na kwa umbile lake, ikiwa ni pamoja na rangi yake "NYEUSI".

    It's Great To Be Black=Blackmannen

    ReplyDelete
  8. Napenda kuchukua nafasi hii kwa kuwashukuru wote. na pia naamini wote mmekuwa na jumapili njema. Mie nilikuwa na wakati mzuri na pia leo kulikuwa na kajua kidogo hapa. Nimeota jua na nimepata rangi zaidi.Ahsanteni sana!! UPENDO DAIMA

    ReplyDelete