Ni miaka miwili leo tangu mwalimu wa utambuzi MUNGA TEHENAN atuache. Nami ninapenda kumkumbuka/tumkumbuke kwa makala hii aliyoiandika kwenye kitabu chake cha MAPENZI kuchipua na kunyauka. Haya tujumuike na kuisoma makala hii:-
Msichana mdogo wa miaka 18 aliwahi kuja kwangu na kuniomba msaada. Hakuhitaji msaada mkubwa sana kama mwenyewe alivyosema, kwani alitaka kusaidiwa kupata jibu la swali ambalo lilikuwa likimtatiza kwa muda mrefu.
”Nataka kujua maana ya kupenda.” ilikuwa ndiyo kauli yake, fupi na inayoeleweka. Sikujibu swali lake moja kwa moja bali nilimwambia, ”umesema unahitaji msaada mdogo, lakini unayemwomba hana uwezo wa kukusaidia.” Nilizidi kumwambia kwamba, hata mimi nimekuwa kwa muda mrefu nikitafuta jibu la swali hilohilo.
Hivyo, sikuweza kumsaidia na niliona jambo lile lilinipa changamoto nami kuanza kusaka jibu la swali lile. Lakini, bahati nzuri ni kwamba, kabla yule msichana hajaondoka kwangu nilimuuliza nami swali moja. ”Ni kwa nini unataka kujua maana ya kupenda”? Alinijibu bila kufikiri mara mbili kwamba, ni kwa sababu gani anataka kujua kama mpenzi wake anampenda. Pengine jibu lake lilinizindua na nilihisi kama vile ndani ya jibu hilo kungeweza kupatikana pia jibu la lile swali lake. ”Ukishajua kama anakupenda ndiyo itakuwa nini baada ya hapo?” Nilimuuliza, pengine nikiwa sitegemei jibu.
Alikuwa ni msichana ambaye majibu yake yameandaliwa tayari kutolewa. ”si ndiyo nijue hanidanganyi, sasa nitampenda vipi kama yeye hanipendi!” alipomaliza kunijibu, nami nikawa nimepata jibu la swali lake.
Wengi husubiri kupendwa kwanza:
Siyo msichana yule tu, bali wengi miongoni mwetu tunasubiri kupendwa au huwa tunataka kwanza kuwa na uhakika kuwa tunapendwa, ndipo nasi tupende. Ukimfuata mtu na kumwambia kuwa unampenda, ungependa awe mpenzi wako au mwezi wa baadaye maishani na mtu huyu akawa mkweli na kukuambia kwamba, yeye hakupendi, utaumia sana. Utaanza hapohapo kumchukia au hata kumfanyia visa.
Unakuwa katika hali hiyo kwa sababu kuu mbili. Kwanza, ni kwa sababu hujui kwamb, kinyume cha kupenda siyo kuchukia. Unapomtaka mtu uhusiano na akasema hapana, unamchukulia kuwa anakuchukia kwa sababu, kwako kama hakuna kupenda, basi ni lazima kuwe na kuchukia.
Tumelelewa na kukulia katika mazingira ambayo yametufundisha kukitazama kila kitu katika uwili. Kwa hiyo, `sikupendi`masikioni mwetu inasikika kama, `nakuchukia`.
Pili, ambavyo ni kubwa, ni kwa sababu kila binadamu anahitaji kupendwa. Wataalamu wengi wa saikolojia wanabainisha kupendwa kama moja ya mahitaji muhimu kwenye ngazi ya mahitaji ya binadamu.
Tangu tukiwa na umri wa siku moja, tunataka kukubaliwa kupokelewa na kulindwa. Haya ya kupendwa ni kama jambo la kimaumbile kwa binadamu. Unapogundua kuwa watu wote hawakupendi ni lazima utababaika, utachanganyikiwa na kwako maisha yanaweza kupoteza maana.
Wengi tunafanya tuyofanya au kuacha kufanya katika kutafuta kupendwa. Kwa hiyo, kila mmoja wetu ana kiu kubwa ya kupendwa. Hapa ndipo linapochipuka tatizo kubwa linalofanya wengi kushindwa kujibu swali la , `kupenda ni nini?` Hushindwa kwa sababu, hakuna anayejali kupenda, karibu wote tunajali kupendwa, tuna kiu ya kupendwa, siyo kupenda Kama nguvu zetu zote tumeziweka kwenye kupendwa, kupenda kunakuwa na nafasi gani kwetu? Ndiyo maana wengi hatuju kupenda ni nini?
Ni kitu gani kinatokea? Ni kwamba, badala ya kuwekeza kwenye kupenda, tunawekeza kwenye kupendwa ambako hakutuhusu. Ni sawa na mtu kuchukua fedha zake na kuziingiza kwenye akaunti ya mwingine akiamini kwamba anaziingiza kwanye akaunti yake. Siku anapokuja kutaka kutoa fedha na kukuta hazipo atazusha zogo kubwa na balaa lisilowezekana. Atadai kwamba benki hazifai na hazina ukweli.
Unaposubiri au kutarajia na mbaya zaidi kudai kupendwa, unapoteza muda wako bure, kwa sababu hilo ni jambo lisilokuhusu. Ni jambo ambalo huwezi kulipanga wala kulidhibiti kwa sababu linamhusu mtu wa upande wa pili. Inawezeakana vipi wewe umalazimishe mtu akupende? Haiwezekani, lakini tunafanya. Tunafanya lisilowezekana.
Lakini unaweza kupenda, kwani ni jambo linalotoka kwako , lililo ndani ya uwezo wako. Kwa hiyo, unapokutana na mtu, kama amekuvutia, wewe ndiye unayetakiwa kumpa upendo, bila kujali kama naye anakufanyia hivyo. Huna haja ya kujali kama naye anakufanyia hivyo kwa sababu, wewe umeamua kumpenda, lakini huna haki na huwezi kumfanya akupende kama yeye hataki.
Bila shaka huwa unakutana na vitukovya karne kila siku kuhusu jambo hili. Mtu anaambiwa na mwingine kwamba hampendi. Inawezekana kuwa ni wapenzi wa muda mrefu-mke na mume au hata wa muda mfupi. Badala ya huyu anayeambiwa huapendwa kukubali jambo hilo kwa sababu hawezi kulibadili, kupinga. Wengine huenda hata mahakamani au kuwauwa wapenzi waliowakataa. ITAENDELEA…….
HABARI HII NIMEITOA KATIKA KITABU CHA MAPENZI KUCHIPUA NA KUNYAUKA KILICHOANDIKWA NA MAREHEMU MUNGA TEHENAN.
uuuuwiiiii, li mwaka la pili limepita, jamaa alituaga kinamna kumbe kafa
ReplyDelete@Kamala: kama uko na utambuzi wa hali ya juu waweza kujua jinsi utavokufa na siku 3 kabla waweza kuwa na taarifa na kuwajulisha wapendwa wako.
ReplyDeleteBwana Jizazi mwenyewe alijua hata kujua kile kingetokea baada ya kuwekwa pangoni a.k.a kaburini :-(
RIP Munga
Leo mi sina maneno...navuna tu maarifa
ReplyDeleteAhsante sana dada Yasinta kwa hii mada ni nzuri sana imenibariki.
ReplyDeleteMimi mtazamo wangu upo tofauti sana na hii maada, Neno UPENDO ni kubwa kuliko tunavyofikiri,Na pendo halisi lipo kwa Mungu. Pendo halisi, halichagui, halijivuni, halitakabari, halihesabu mabaya na halichoki. Kulingana na ulivyoelezea hiyo maada kupenda kunaweza kugawanya mara 2.
1.kupenda kwa ajili ya kukidhi matakwa ya kibinafsi, ambako ndiko kumetutawala sana,(eg mke na mume). Na huku ndiko kunakotupelekea hata kujiua ukigundua mwenzio anakusaliti, au hakupendi. na sometimes unakuwa hujiamini hata mwenzio akikuambia anakupenda.
2. Kupenda pendo halisi(agape). huu upendo haujali jinsia, unapenda toka rohoni na haijalishi kama umpendae anakupenda. unapata msukumo toka rohoni na unatenda kulingana na msukumo wa pendo, pendo huvumilia na halioni uchungu