Thursday, January 7, 2010

WANAWAKE NA SHERIA YA KUBAKWA


Nilipokuwa nyumbani Tanzania mwaka juzi, niliwahi kuzungumza na binti mmoja ambaye ni mhitimu wa sheria chuo kikuu. Katika mazungumzo yetu nilimuuliza juu ya tatizo la ubakaji hapo nchini kuwa sheria za nchi zinasemaje juu ya makosa ya aina hiyo?
Kama nilimnukuu vizuri, binti yule aliniambia kuwa sheria ya ubakaji ipo na inafanya kazi, kwa mujibu wa maelezo yake, alidai kuwa sheria hiyo inamlinda mwanamke kwa kiasi kikubwa sana. Kwa mfano hata kama mwanamke aliridhia kufanya kitendo cha kujaamiana na mwanamume, na baada ya kitendo kile bila kujisafisha akaenda polisi na kuripoti kuwa amebakwa, na ikathibitika kupitia vipimo vya DNA kuwa (manii) shahawa zilizaokutwa katika uke wa mwanamke yule ni ya mwanaume mtuhumiwa, basi moja kwa moja mwanaume huyo atakuwa matatani.

Kwani kwa mujibu wa sheria inasema, kama mwanamke yule angekuwa ameridhika kuingiliwa na mwanaume mtuhumiwa basi asingekwenda kuripoti polisi. Nilimuuliza mbona makosa ya aina hiyo yapo sana hapa nchini na yanaandikwa sana katika vyombo vya Habari? Alinijibu kuwa tatizo ni ukosefu wa ushirikiano kati ya wanawake wanaobakwa na polisi kutokana na wanawake wanaofanyiwa vitendo hivyo kuona haya kwenda kuripoti, hususani wale walioolewa, huogopa kutoa taarifa katika vituo vya polisi ili kuepuka kuachika pindi waume zao wakifahamu. Polisi nao kwa upande wao, hawatoi ushirikiano wa kutosha kwa waathirika wa vitendo hivyo kwani huwakejeli na kuwapuuza kwa madai kwamba waliyataka wenyewe.

Tulizungumza mambo mengi yanayofanana na hayo, na kusema ukweli yule binti alinifumbua macho kwa kiasi fulani, kwani kabla ya hapo sikuwa nikiyafahamu hayo.

Bila shaka wasomaji wa blog hii mtajiuliza kulikoni leo kuzungumzia jambo hili.
Ni kwamba nimekuwa ni mfuatiliaji sana wa habari za huko nyumbani na nimekuwa nikishangazwa sana na kuripotiwa kwa matukio ya watu kubakwa kwa kiasi cha kutisha, niliwahi kuweka habari moja ambayo niliichukua kutoka katika gazeti la Mwananchi juu ya waendesha pikipiki wa kule Songea maarufu kama yeboyebo jinsi wanavyowabaka wanawake pindi wanapowabeba kuwapeleka katika safari zao kwani usafiri huo hutumika kama taxi kule vijijini.
Ni jambo la kushangaza kuwa pamoja na kuwepo sheria hii lakini matukio ya aina hiyo yapo na hayakomeshwi.

Hata hivyo lipo jambo moja ambalo nilijiuliza. Hivi kama kubaka ni kitendo cha mwanaume kulazimisha kumuingilia mwanamke bila hiyari yake, je kwa wanandoa inakuwaje? Ikumbukwe kwamba sheria hiyo haikutenganisha kati ya wanandoa na wale wasio wanandoa, sheria imesema tu kwamba, kama mwanamke akiingiliwa na mwanaume bila matakwa yake akienda kuripoti katika vyombo vya sheria, basi mwanaume yuko matatani.
Kama sheria inamlinda mwanamke kwa kiasi hicho, basi wanawake wengi sana walioko katika ndoa hubakwa na waume zao karibu kila siku, kwani wakati mwingine wanawake walio katika ndoa hulazimika kukubali kufanya tendo la ndoa nje ya utashi wao. Mila na desturi zetu zimemnyima mwanamke uwezo wa kusema hapana pindi mwanaume akitaka, kwani neno “geuka huku” sio ombi ni amri ambayo inatakiwa kutekelezwa bila kupingwa. Bila shaka mtakubalina na mimi kuwa mila na desturi zetu zinatufundisha kuwa kuolewa kwa mwanamke ni kwenda kutumika kama chombo cha kumstarehesha mwanaume na kumzalia watoto, na ndio maana kama ikitokea mwanamke akiolewa halafu asipate mtoto, anayeangaliwa na kushutumiwa ni mwanamke na sio mwanaume kwani aliolewa ili amzalie mwanaume watoto ikiwa ni pamoja nakumstarehesha.
Hata kama mwanaume ndiye mwenye tatizo, bado jamii itamtetea. Niliwahi kusimuliwa kuwa yapo baadhi ya makabila hapo nchini mwanamke hulazimishwa kutoka nje ili amzalie mwanaume watoto ikiwa kama mwanaume amekosa uwezo wa kutia mimba, lengo ni kulinda heshima ya mwanaume, na jambo hilo hufanywa kwa siri sana.

Wanaume huamini kwamba wanazo haki zote kwa miili ya wake zao, lakini wake zao hawana haki hizo, na kutokana na mfumo huo dume wanawake nao wameaminishwa kuwa wenye mamlaka na miili yao ni waume zao.

Kwa kawaida wanawake huishi kihisia, hivyo inapotokea kuathiriwa kihisia na hamu ya kushiriki tendo la ndoa hupotea, hivyo wanaume wanapowambia, “geuka huku” hulazimika kufanya hivyo sio kwa mapenzi yao bali hutekeleza ili kuepusha shari vinginevyo itakuwa nongwa.

Hivi ni mara ngapi tumesikia kupitia vyombo vya habari kuwa mwanaume kamuua mkewe kwa kunyimwa unyumba? Ni mara nyingi tu, lakini binafsi sijawahi kusikia mwanamke kamuua mumewe kisa kanyimwa unyumba, sidhani!


Naamini kuwa kama wanawake walioolewa wataamua siku moja kuwashitaki waume zao kwa kubakwa kama sheria inavyoruhusu, basi magereza hapo nchini yatajaa mpaka pomoni, maaana hakuna atakayebaki, lakini, thubutuuu….nani ajaribu, jamii yote itamhukumu kuwa amekosa adabu kwa mumewe.

16 comments:

  1. Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti!January 7, 2010 at 8:29 AM

    Da Yasinta, ulosema yana ukweli upande mmoja na upande mmoja hapana.

    "Kwa kawaida wanawake huishi kihisia, hivyo inapotokea kuathiriwa kihisia na hamu ya kushiriki tendo la ndoa hupotea". Inategemea na hizo hisia zimeathiriwa na nini... kujitakia ama sababu za msingi. Ninaposema kujitakia na-refer kwa wale wanaotumia madawa ya kuzuia mimba (I am sorry to say that I am pro-life activist) kwa kuwa wanaotumia hayo madawa mara nyingi huwa na tatizo la kutokuwa na HAMU ya tendo! na nina stori ya kadogo kangu kamoja hapa Musoma ambako nkewe anatumia madawa hayo hataki kusikia wala kuambiwa geuka huku na kamjamaa kana-plan kum-send off kwenda kwao mpaka atakapokuwa na hisia... :-(

    Juu ya wadada na wamama kutothema, unadhani ni uoga wa kuachika ama kuchekwa na jamii? kama ni hayo basi lawama zisiende kwao bali kwa jamii nzima kwa kuwa wasingekuwa wanawanyanyapaa basi hayo yasingetokea

    hiyo para ya kwanza imeniacha hoi...lakini pia wanaogopa kuwa wakienda kuripoti polisi wengine wakware huomba wawamege a.k.a wawaonje (hata kama wamebakwa) :-(

    Ubakaji katika ndoa...mh! hilo nalo neno!

    Pole kwa wale wanaotaka kupata denda bila kulipia kama mtakatifu nanihiino kwani sheria hii duh!.... :-(

    Cha muhimu ni jamii kujua thru uelimishaji kama wa akina kamala...lol

    ReplyDelete
  2. Niliwahi kusema wakati fulani kuwa sitamani kuolewa, rafiki yangu Markus Mpangala AKA MCHARUKO na Kamala nusura wanitoe jicho kwa vidole machoni.....

    Nashukuru dada, Yasinta umelinena hili, maana hakika wanaume nao wana vijimambo wakitaka kunaniliu, hata hawana ustaarabu, ni amri moja kwa moja...eti "GEUKA HUKU" utadhani Jeshini?

    CHACHA WAMBURA NG'WANAMBITI naomba nipingane na wewe juu ya swala la madawa ya kuzuia mimba. nakubali kuwa baadhi ya madawa hupelekea mwanamke kupoteza hamu ya tendoa la ndoa lakini hicho sio kigezo cha kubaka, kwani kama mwanaume atamuandaa vizuri mkewe kisaikolojia anaweza kuridhia na akalifurahia tendo la ndoa, lakini kama kutakuwa na kusigishana kwingi kabla ya tendo kufanyika hapo ni lazima kutakuwa na kubakwa na sio kwa utashi wa mke.

    Ki ukweli wanawake wanavumilia mengi katika ndoa, hili likiwemo lakini halisemwi maana ni siri ya chumbani, namshukuru mama yetu kwa kuwa muwazi kwetu na hivyo kufahamu mengi juu ya ndoa na ndio maana najiamini kwa kuwa ninayajua haya na sipigi blah blah hapa.

    Kwa hili naomba wanaume mkiri kuwa mna hako kaudhaifu ka kubaka wake zenu....

    ReplyDelete
  3. hukuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuu GEUKA!!: moja mbili tatu moja, GEUKA! moja mbili tatu moja NIMESEMA GEUKA ''.......................... maweeeeeeeeee..............'

    geukia huko fasta pumbavu!

    endeleeni kuogopa huku ya jamii na sisi tuendelee kujipatia uroda kadri tupendavyo, mlie tuuuuu

    ReplyDelete
  4. Kamala unanikumbusha mambo ya Ng'ang'a.

    ReplyDelete
  5. Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti!January 7, 2010 at 2:07 PM

    @Da Koero: umisema kuwa 'baadhi' ya madawa sivo? Ok. That speaks more than 95%m ha!

    Nadhani hukunisoma vema kwani sikumaanisha kuwa kwa kuwa hataki rigwaride ndo ummege bila konsenti yake. hata hivo nachelea kusema kuwa ANAWEZA KUWA KAKUKUBALIA lakini ukammega bila yeye kujishughulisha na kwa wababa/wakaka wengine wanajisikia kama vile wameBAKA!

    Ama hujasikia makabila FULANI hapa TZ na kwingineko anaweza kumkubalia njemba limuonje kisha akachukua gazeti na kumwambia mbaba 'FANYA KASI YAKO UKIMALISA FUNIKA!' na kumwachia njemba ajikunjeeeee mpaka anamalisa kisha anafunika...(samahani Mt kwa taralila hii!) :-)

    hata wanawake wanawabaka waume zao au unataka ushahidi? :-(

    ReplyDelete
  6. Kupewa kwa hiyari ILE KITU yoteyote na mdada ASIYE NA HAMU ya kutoa tunda nasikia ndude ikichekiwa na daktari inakuwa na mikwaruzo kama tu ya mdada aliyebakwa hata kama safari hii dafu lilitolewa kwa hiari wakati halijaandaliwa vizuri tobo.

    Na inasemekana wako wanadada WENGI wakubalio tu mladafu achokonoe dafu hata kama dafu halijaandaliwa kuchokonolewa kwa kuwa tu WANAMPENDA mtaka dafu na wanataka AJINOME tu ingawa INAUMA au wanahofia kuwa mla dafu akikataliwa kuchokonoa dafu ataenda mawindoni kutafuta MWINGINE mwenye dafu.:-(


    Kwa hiyo kwa mapenzi kuna mpenzi ambaye huumizwa kila siku KWA HIYARI YAKE MWENYEWE na hukubali hilo kwa mapenzi yake kwa mchokonoaji ingawa kitokeacho kina maumivu sawa na mbakwaji ukiondoa tu maumivu ya kisaikolojia ya MTENDEWA aaminipo kitendo kilichotendeka ni UBAKWAJI.

    Na kwa hilo naamini kifikia kuwa ni kawaida kwa mke kumshitaki mume TANZANIA wako wengi ambao watashtakiwa wamebaka na kukawa na ushahidi lakini wafanyacho ni hicho hicho cha kila siku watoto wakilala ila wakati mke hajachukia na HAJAKIFIKIRIA kimkao wa UBAKAJI kivitendo na kisaikolojia na anavumilia MAUMIVU kwa kuwa anataka mume afurahi au tu katika kutunza ndoa. Na anashukuru Mola kuwa midume kibao kupata kibaruti spidi ni Usain BOLT miguno mitatu mbegu za mwagwa hata kwa kukosea kulenga shimo.


    Kuna anayejua utamu wa kubaka unatofauti gani na wakupewa yoteyote bila kulazimisha hapa atueleze?

    Maana nasikia kwa wengine utamu wa mechi lazima mechi iwe na vurugu ati!:-(

    Unafikiri kuna tofauti ya maumivu ya kubakwa kwa mke na mume wake na kubakwa kwa mdada uchochoroni na asiye mjua ukizingatia inasemekana katika kubakwa kiumizwacho zaidi ni UBongo, kisaikolojia?

    ReplyDelete
  7. Kitururu kama wewe ungekuwa ni mume wangu ningekwambia "SHIKA ADABU YAKO" Namsikitikia Mahabuba wako maana najua kazi anayo.

    Kamala: nawe mkeo ana kazi kama mabo yenyewe ni ya KIJESHI namna hiyo......duh! namsikitikia sana nadhani atajuuuuuuuuta kukufahamu....LOL

    Chacha o'Wambura Ng'anambiti: nawe usijidai kutafuna maneno naomba unipe ushahidi wa unaothibitisha kuwa kuna mwanamke aliwahi kumuua mumewe kwa kunyimwa unyumba.....tena nilishahau tu kukwelleza kuwa tabia ya "GEUKA HUKU" iko sana huko kwenu.
    "MAMA BHOKE GEUKA HUKU MARA MARA MOJA"........LOL

    ReplyDelete
  8. @koero, kumbuka wewe ni mpenzi wangu wa zamani na si unajua maana ya mapenzi? zamani ikigeuka ssasa utajuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuta kujiita mpenzi wangu wa zamani

    ReplyDelete
  9. @Koero: Kwani mpaka leo hujastukia maneno hayavunji mfupa?

    ``SHIKA ADABU YAKO´´ ingekuwa na nguvu.

    1.Kusingekuwa na watoto watukutu TANZANIA.

    2. Walalahoi wangesha washikisha adabu MAFISADI Tanzania.

    3. Kila kijeba wa jamii nyingi za KIAFRIKA angepata demu kwa kuwatishia tu WASHIKE ADABU kwani ni mwiko kumuonyesha mwanaume huna adabu ukiwa mwanadada.


    4. Binadamu wasingehitaji kugundua matumizi ya FIMBO kushikisha watoto adabu, kufinya wala MGAMBO wasinggundua kushika watu vibindo kwani maneno yangetosha.


    Swali zaidi kwako DA KOERO nihisiye una adabu:

    Kwani ADABU ni nini na inashikiwa wapi?

    ReplyDelete
  10. MCHARUKO ................Woteeee nyamazaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaa,

    ngoja kwanza sikiliza................ "we mama Sindibadi, ile sindano iko wapi mbona siioni?.. ebu njooo unionyeshe ilipo mi siioni kabisa uje mwenyewe.....unasema ipo juu ya meza sijui wapi...ebu njooo huku wewe..!!!!!

    ha ha ha ha ha MCHARUKO huooooo mie simo ha ha ha HEE KUMBE HATA BABA ANAMBAKA MAMA YANGU?????? walahiii .....................

    @kOERO NAKUNUKUU ""Niliwahi kusema wakati fulani kuwa sitamani kuolewa, rafiki yangu Markus Mpangala AKA MCHARUKO na Kamala nusura wanitoe jicho kwa vidole machoni....."" mwsiho wa kunukuu

    mmmh! sasa...... ok ngoja nina kiu, halafu Zantel wamemaliza kavocha ka internet duh!! MCHARUKO.
    aaaaaaaaaaaaaaaa #Koero si umeseme unakaribia kuzeeka? si ulisema kuna anayekumiliki?.............eeeeehhhh sasa kwanini asikwambieeeee GEUKA....,,,,, HUKU.... waubani... GEUKA tu polepole........

    swali unapokimiliki kitu unakifanyaje?????? ha ha ha ha MCHARUKO ...............Lol

    ReplyDelete
  11. Kaka kitururu, kaja na swali: Eti shika adabu yako maana yake ni nini?
    Ngoja nikaamulize mama Namsifu halafu nitarudi hapa kukujibu.

    Kamala: mzee wa fungate, naamini mpaka fungate ikiiisha safari ya kuhudhuria kliniki haina mjadala....mtarajiwa wa kuongeza dunia.

    Markus; Duh staili yako kali ...yaani si geuka huku tena, bali njoo unisaidie kutafuta sindano....wewe kweli una mbinu. sasa ndugu yangu huko sio kubaka?

    ReplyDelete
  12. Mada nyingine zahitaji kufungwa kwa MAOMBI ili wachangiaje waongozwe na ROHO MTAKATIFU.
    Duh!!!!
    Mie mgeni usawa huu. Wacha nikae pembeni nijifunze

    ReplyDelete
  13. Kauli ya mwaka huu ni kuangalia mambo kwa JICHO LA NDANI. Nimekaa na kuangalia na sasa naanza kuivuta picha taratiiiibu. Na picha hiyo yaja na swali kuwa KWANI KUBAKA NI TENDO AMA FIKRA JUU YA TEND LILIVYOTENDEKA? Nimesikia kuwa mtu anaweza kufanya penzi na mtu na asipomlipa alichotakiwa kumpa, msichana anaweza kupiga kelele na kusema kabakwa na mwanaume akashitakiwa na kuhukumiwa.
    Labda tuanze na swali kuwa KUBAKWA NI TENDO AMA FIKRA? Na je, kubakwa kwaanza kabla ya tendo kuanza ama kunaweza kuamuliwa endapo "mtenda-mwenza" kafikiri hakutendewa haki? Na kwanini wakati mwingine mtu anaweza kutishia kupiga kelele lakini akiongezewa dau anasema amefanya mapenzi badala ya kubakwa?
    NADHANI KUNA NGUVU ZA KIUCHUMI NA KIFIKRA KATIKA SUALA ZIMA LA KUBAKANA.
    Hebu angalia maswali hayo kwa JICHO LA NDANI kisha uyajibu.
    Blessings

    ReplyDelete
  14. Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti!January 9, 2010 at 9:37 AM

    @Mt Simon: ushamaliza yote nilotaka kusema kwani uminyambulisha mineno yote. Laiti ungekuwa karibu tungeshea ze CHIBUKU mpaka asubuhi :-)

    @Koero: bado sijaona kitu hapo. Kwa taarifa yako baadhi ya wa huku kwetu hakuna cha kubakana kwani mambo yanakwenda chapuchapu. Utamsikia binti anamwambia njemba 'tebheta bhongo ngende!' literary akimaanisha 'choma-choma haraka niende'! :-)) Sasa hapo nani amebakwa, mwanaume ama mwanamke? Be frank please :-(

    Kuna mwana-blog mmoja aliwahi kunambia story juu ya njemba alomwagiwa maji machafu na mama wa binti alipotoa maji hayo na kupiga kelele baada ya kumdhania ni kibaka. Awali walizoea mida hiyo binti alitoka kumwaga uchafu na kuingia bafu la 'matete' ambapo kuna tobo na jamaa hujikunja tokea nje na kumalisa shida yake (bila hata maandalizi ambayo Da Yasinta na Koero wanayashabikia)... :-( Nani kambaka mwingine hapo?

    Kama alivosema mt. Simon, dhana ya ubakaji ni pana na kwa mifano hiyo hapo juu nadhani mjadala bado unapaswa kuendelea na siyo hapa kijiweni tu bali katika jamii kwa ujumla.

    Ama hujasikia kuwa kwa baadhi ya makabila si lazima waombane kama Kaka Mpangala alivoiweka? kwa wengine mpaka purukushani na kukimbizana ka kuku :-(


    Labda niseme tu kuwa kuna dimensions tofauti kuhusu jambo hili kwa kuwa baadhi ya sababu ni socially and culturally constructed than being contemporary.

    basi na tuliangalie kwa JICHO la ndani kama anavoiweka kaka Musee ya Chagamoto japo sijui kama jicho hilo ni la kulia ama la kushoto :-(

    ReplyDelete
  15. Heshima kwako kaka Mubelwa Bandio
    Kwa kawaida sina tabia ya kubishana na kaka yangu Mubelwa. Nakubaliana na yeye kwa upande wa jicho la ndani, lakini kwa upande wa jicho la nje…….kaka naomba tutofautiane kidogo tu…
    Ndio ni kweli kuwa pale panapopenyezwa rupia, tishio la kubakwa huondolewa haraka sana….jamani pesa ni sabuni ya roho ati! Lakini hivi hapo ile dhana ya kubaka itakuwepo au la?
    Kamusi ya Kiswahili sanifu inasema kubaka ni kile kitendo cha kulazimisha mapenzi au kufanya mapenzi na mtu awe ni mtu mke au mtu mume bila hiyari yake…..
    Kwa hiyo basi hiyari haikuwepo ila kitendo kilihalalishwa baada ya rupia kupenyezwa…..sijui nimeeleweka.
    Huko vijijini kabla ya hizi taasisi za kutetea haki za wanawake na watoto maarufu kama NGO’s kuanza pilika zao za kutafuta mkwanja kwa njia ya “matatizo yenu tijara yetu” haya matukio yalikuwepo sana, lakini kulikuwa ka utaratibu ka vikao vya wazee kuyamaliza kimya kimya kwa mtuhumiwa kulipishwa faini ya ama Jogoo au mbuzi na wakati mwingine Ng’ombe kulingana na kosa la mtuhumiwa, kama athari hazikuwepo. Jamani swala la kubaka litabaki kama lilivyo ila linahalalaishwa na kitu kidogo au mapoozeo ambayo mara nyingi kwa wakati huo muathirika hanufaiki nayo.
    Kwako Chacha o’Wambura Ng’wanambiti aka mzee wa KUBHETA………..naona wewe unataka kuchanganya mada hapa, swala la mapenzi ya kujifunza ujanani ambayo mara nyingi ni ya kuvizia…sidhani kama yanafanana na tunachojadili hapa…hapa hatuzungumzii mambo ya “NIGWISAI, NIANGUSAGE, KUBHETA, CHAGULAGA, na mengine yanayofanana na hayo, hapa tunazungumzia mambo ya GEUKA HUKU, au NJOO UNISAIDIE KUTAFUTA SINDANO, kama alivyosema rafiki yangu MCHARUKO Markus Mpangala.
    Naomba kutoa hoja………………………

    ReplyDelete
  16. Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti!January 11, 2010 at 6:24 AM

    Da Koero: Duh! Umesahahu kuwa mila, tamaduni na desturi hazina ujana na uzee sivo? :-(

    yalofanywa ujanani si yanaweza kujirudia ukubwani?

    Naacha ila ukweli unabaki palepale kuwa tatizo liko katika malezi, mila, desturi na tamaduni zetu. Pia wengi wetu tunapoingia katika taasisi ya ndoa hatuna uzoefu amaujuzi wa nini tunakiendea na huwa tunategemea makungwi uchwara kama nanihiiino na matokeo yake ndoa huwa ndoano...:-(

    ReplyDelete