Monday, November 2, 2009

KITABU CHA MAISHA NA MAFANIKIO......

SEHEMU YA KWANZA...........

Kila binadamu anajipenda, ingawa wengine hujipenda zaidi kiasi kwamba hujiona wao wenyewe tu, kama kwamba wako peke yao hapa duniani. Kwa kujipenda kwao sana, wengi huingia mahali ambapo huamini kuwa matatizo na shida zao maishani ni matokeo ya wale wanaowaita adui zao wa aina mbalimbali. Kwa kujipenda kwao zaidi husahau kabisa kwamba bila wengine kuwepo na kukamilika, wao pia siyo kamili. Mada hii inaelezea namna ambavyo adui wa watu wengi ni watu hao wenyewe na siyo wengine na inafafanua kuhusu ukamilifu wa binadamu usivyowezekana pale ambapo wengine hawajakamilika.

Mbu anapokuuma utapata malaria huwa unahesabu kama adui yako. Unaweza kutangaza kwa maringo na kujivuna kwamba uko kwenye kampeni ya kumuangamiza adui mbu ili uondokane na adha ya malaria. Lakini je, ni kweli mbu ndiye adui yako?

Siku hizi kuna virusi vya HIV ambavyo vinahesabiwa kama maadui wa watu wote. Kila kona hapa duniani kuna juhudi za kila aina katika kupambana na virusi hivi. Ukimuuliza mtu atakwambia, virusi hawa ndiyo adui zetu katika suala la maradhi haya, lakini je, kuna ukweli wowote katika hili? Kila mtu anafahamu vizuri mazingira ya aina mbalimbali ambao kwake huyaita adui, kila mtu anawafahamu watu wa aina mbalimbali kwake kwa sababu mbalimbali anawaita adui zake na kila mtu anafahamu vizuri vitu fulani maalum ambavyo kwa sababu fulani anaviita na kuamini kwamba ni adui zake.

Lakini huenda hakuna ambaye anajua ni kiasi gani tabia, mienendo na mawazo yake ni adui zake wakubwa. Ni mara chache sana na ni watu wachache sana ambao wako tayari kujiuliza na kukiri kwamba, tabia mienendo na mawazo yao kwa kiasi kikubwa sana huwa vinawadhuru na kuwaumiza, kuwaharibia mipango yao na maisha kwa ujumla, kuliko wanavyodhani kwamba athari hizo hutoka nje yao.

Ni wachache kwa sababu, binadamu hujipenda sana kiasi ambacho huogopakufunua macho zaidi na kuukabili udhaifu alionao. Ukweli ni kwamba, kama mtu atataka kuishi bila kujidanganya, atagundua kuwa hata mbu na virusi wa ukimwa siyo adui zetu atagundua kuwa kwamba, tabia mienendo na mawazo yetu ndiyo adui zetu. Kama mtu ataamua kujikinga dhidi ya mambo yote yanayoweza kumwambukiza virusi wa ukimwi au kuishi katika mazingira ya mbu wengi na kuchukua tahadhari dhidi ya wadudu hao, anakuwa amemkwepa kwa karibu asilimia tisini huyu au hawa anaowaita adui zake.

Kila siku, hata pale ambapo tunatangaza kamba akina fulani ni adui zetu, huwa tunafanya hivyo kwa makosa kwa sababu tu ya kujipenda na hivyo kujipendelea katika kuutazama ukweli. Tunapofilisika tunajitahidi sana kutafuta maadui wa hali hiyo, huku tukiwa tumesahau kwamba tabia zetu ndizo zinazotufilisi. Tunaposhindwa kupata tunachokitafuta maishani, hatuzitazami tabia, mitazamo,mienendo, imani na mawazo yetu, bali tunatazama nje yetu ili kumpata adui. Ilivyo ni kwamba, kama tunatafuta adui, kwa sababu tunataka kumpata ni lazima tutampata. Hivyo tukishampata tutaamini kabisa kwamba huyu ni adui yetu na kuziweka nguvu zetu hapo kujaribu kupambana naye.

Inachukua muda, na wakati huo tunakuwa tumechelewa sana tunapokuja kugundua kwamba tuliyemdhani ni adui alikuwa ndani mwetu. Lakini kwa bahati mbaya sana ni kwamba huwa hatufanikiwi kungámua kwamba huyu tunadhani ni adui yetu siyo adui yetu. Kwa hali hiyo, huwa tunaishi katika katika dhiki, misukosuko na nuksi zisizokwisha tukijaribu kupambana na adui ambaye siye, huku adui yetu akiwa ni sisi wenyewe. Kupigana huku na adui asiyekuwepo popote bali ndani mwetu huweza hata kutupotezea maisha yetu. Kwa nini basi kabla hatujatangaza au kudhani fulani ndiye adui yetu, tusitazame au kuzigundua kwanza tabia zetu, mienendo, imani, na mawazo yetu? Wanasema wataalamu wa nyanja zote za kimaisha katika nadharia zao nyingi kuhusu maisha kwamba, adui wa mtu ni mtu mwenyewe. Tulitafakari hilo kwa makini.

Tusipolitazama kwa makini tutajikuta kila siku tukizidi kuongeza idadi ya maadui huku hali zetu kielimu, kiuchumi na kijamii kwa ujumla zikizidi kudorora. Zitazidi kudorora kwa sababu yule tunayemdhani ni adui yetu atatupitezea muda wetu na kutusumbua sana, wakati adui yetu tunaye ndani mwetu na tunaweza kumuondoa kwa saa kadhaa tu kama tutamgundua.

Kwa nini huwa ni vigumu kwetu kmjua au kumgundua adui yetu pale mambo yetu yanaposhindwa kwenda kama tulivyotarajia au kutaka? Ni kwa sababu tumefundishwa na mazoea kwamba sisi ni vitu vilivyo nje yetu na hivyo, kusimama au kuanguka katika maisha yetu hutegemea wengine na mazingira ya nje yetu. Tunapopata fedha na kuzitumia vibaya, hatujikagui na kujiuliza kama chanzo cha kufikia hatua hiyo siyo sisi wenyewe, bali tunaanza kuwaambia wake zetu kwamba wana nuksi au kuwasingizia jirani zetu kwamba wametuendea kwa waganga kutuharibia bahati zetu.

Tunapotoka nje kwenye ndoa zetu na kufanya uzinzi, hatuko tayari kujikagua ili kuuona ukweli, bali tunachoweza kufanya ni kuwasingizia wake au waume zetu kwamba wao ndiyo chanzo kwa sababu hawatujali, kwa sababu ni dhaifu wa tendo la ndoa au kwa sababu hawana fedha. Ni vigumu kwetu kujiuliza kama sisi siyo chanzo au kujiuliza mchango wetu kwenye suala zima. Tunajipenda sana na kuamini kwamba sisi ni watu nav itu vinavyotuzunguka.

Tunapopoteza kazi zetu hatujikagui kama sisi wenyewe hatukuchangia kufukuzwa huko, kwani adui zetu siku zote wako nje yetu na ni lazima tutawatafuta. Tunaweza kumnyooshea kidole cha lawama bosi wetu au walio chini yetu, tunaweza kudai kwamba ni jirani au ndugu zetu ambao ati siku zote hawakuwa wakifurahia mafanikio yetu. Ndiyo ubaya wa kujipenda na kuamini kwamba adui zetu wako nje yetu na ni lazima kila linalokwenda kinyume na matarajio yetu liwe limesababishwa na watu hao au mazingira hayo. Umefika wakati ambapo inabidi tubadilike sana na kuanza kuujua ukweli kwamba sisi ndiyo waamuzi na waendeshaji wa maisha yetu.Kila linalotutokea ni matokeo ya tabia, mienendo na mawazo yetu.

Makala hii nimeichukua kutoka kwenye kitabu cha Maisha na Mafanikio kilichoandikwa na Hayati Munga Tehenan ambaye alikuwa ni Mwalimu mzuri wa maarifa ya Utambuzi akitoa elimu hiyo kupitia magazeti yake ya Jitambue, vitabu na semina zake nchini Tanzania kabla ya kufariki dunia.

ITAENDELEA...............

5 comments:

  1. Aksante kwa ujumbe huu. Nimeipenda hii "Tunajipenda sana na kuamini kwamba sisi ni watu nav itu vinavyotuzunguka"...

    Lakini nadhani pamoja na kujipenda huko tumeenda zaidi kuamini kuwa sisi ni VITU zaidi ya WATU...lol

    ReplyDelete
  2. Ni kweli kabisa kwamba huwezi kuwa wewe bila wengine kuwepo mahali ulipo nahasa wale wenye umimi inabidi kukumbuka kwamba hata wengine pia ni bora kama walivyo wao

    ReplyDelete
  3. yep Yasita ndani ya utambuzi, keep it up. kama unahitaji vitabu na mchapisho zaidi ya Munga tehenan, basi tuwasiliane mrembo ehe?? kujitambua muhimu sana

    ReplyDelete
  4. nashukuru kama umeupenda ujumbe huu kaka Chacha Wambura.

    Hapo kaka Bennet umenena kuwa wote hapa duniani ni bora .Ahsante kwa hili

    Ndiyo Kamala Yasinta ndani ya utambuzi. Najaribu kuwa mtambuzi...lol.

    ReplyDelete
  5. Oh! Kamala nikihitaji vitabu na michapisho zaidi ntakuambia Ahasante kwa offa.

    ReplyDelete