Friday, March 6, 2009

SITASAHAU MWAKA 2004­-2005

Sitasahau:- Ghafla 18/8 2004 niletewa habari kuwa sina mama tena. Ilikuwa kama ndoto, kwani sikuletewa habari kuwa anaumwa. Kwa hiyo sikuamini kabisa. Kwa kweli ni pigo kubwa sana kuondokewa na mama. Huku mbali ugenini sikujua nifanye nini, kwenda nyumbani ni mbali. Maisha yangu yanazidi kuwa magumu;- ningebaki nyumbani NINGE. Kwani kuna mambo mengi watu wanahitaji kuongea /kupata ushauri wa mama, sasa nitaenda wapi. Kila nikifikiria hili jambo nakosa raha kabisa. Pole mama yangu hajawafaidi /hajacheza na wajukuu wake. Na pia pole mimi sijamfaidi mama. Namshukuru mume wangu pamoja na marafiki wote kwa kunifariji wakati nilipokuwa na majonzi. Naweza kusema ilikuwa si mbali sana ningechanganyikiwa kabisa. Kwani kidogo nilichanganyikiwa niliacha kula nilikataa kwenda kazini pia shuleni nilichotaka ni kulia tu kwa kweli ilikuwa hatari. Ukizingatia pia sikuweza kuhudhuria mazishi kwa maana hiyo inakuwa vigumu sana kuamini. Mwaka huu mzima ulikuwa mwaka wa majonzi na mateso makubwa sana nilipungua/ kilo 10 hivi. Ila kwa maana nyingine nasi tulihudhuria mazishi yake. Tuliwaombe wapige picha (video) lakini hata hivyo sio sawa na kuwa pale. Kwa hiyo mpaka sasa kichwani/akilini mwangu mnaniambia mama bado yupo. Nimesahau kusema mama alitutoka trehe 17/8-04 saa mbili usiku hii siku ilikuwa si siku nzuri kwani pia binti yangu ilikuwa siku yake ya kwanza kuanza shule. Mama alizikwa 19/8-04

Mapema 2005 mwanzoni tukafunga safari kwenda nyumbani Tanzania. Ilikuwa taabu sana nilibadilika, sikutaka kutoka pale nyumbani kwenda mbali. Kama vile kusalimia marafiki Wino-Matetereka. Nilikuwa naogopa, nilikuwanamsubiri mama. Kwani ilionekena kama tu, ameondoka kidogo. Au yupo safarini. Nadhani maisha yangu hayatakuwa kama yalivyokuwa. Wakati mwingine siwezi kuamini eti mama hayupo. Wengi waliumia sana siku ile, ila kwa kuwa mbinafsi nataka kusema mimi niliumia zaidi. Naletewa habari mama hayupo, lakini siwezi kwenda kwenye mazishi pia wala kumwona mama yangu kwa mara ya mwishoyaani ile (BURIANI). Hii ndio maana siwezi/sitaki kuamini pia kusema hili neno marehemu. Kwa sababu kwa mimi mama yupo nami si marehemu.HILI SITASAHAU.

17 comments:

  1. Pengine watu wanaoshughulika na mambo ya kujitambua (Bwaya, Kaluse na Kamala) watatoa maoni mazuri zaidi kuhusu mada hii. Inategemea na falsafa yako mwenyewe kuhusu kifo (wengine wanaamini kwamba kifo ni kutokuwepo wakati upo!). Ninachoweza kusema hapa ni kwamba pengine mama yupo kwenye furaha na anakutakia furaha na mafanikio wewe binti yake pamoja na wajukuu zake. Tekeleza aliyokufundisha na zingatia yote aliyoyapenda, fanya alichotamani, shukuru kwa muda uliokaa naye (wengine hata hatukupata bahati ya kuwaona na kuwajua mama au baba zetu) na utaweza kuishi naye daima katika maisha yako na hao wajukuu zake. Kama anavyosema Da Mija - wewe ni mwanamke wa shoka na ndiyo maana badala ya kupondekapondeka, kama askari shujaa ulinyanyuka, ukafuta machozi mashavuni mwako na kusonga mbele! Endelea kufanya hivyo na mama huko aliko ataendelea kufurahi!

    ReplyDelete
  2. Kaka Masangu Matondo Nzuzullima, ahsante sana kwa maoni yako mazuri roho yangu na moyo wangu umefurahi sana na nimepata nguvu mpya. Pia nimepta imani shukrani sana.

    ReplyDelete
  3. bora mamako kafa. mimi nina mama anaishi tegeta mimi niko mwenge lakini naonana naye mara moja au mbili kwa mwaka na sijawahi kukaa naye.

    wakati mwingine bwana. nilimjua mama baada ya kumaliza kidato cha nne.

    hata hivyo ni lazima tujifuze kupokea mabadililko yaani kila hali kama inavyokuja. wewe miaka yote hukujua kama mamako angekufa tu hata kama haumwi? bado unaogopa kifo mpaka unakonda?

    pole lakini samahani kama hatuelewani

    ReplyDelete
  4. bora mamako kafa. mimi nina mama anaishi tegeta mimi niko mwenge lakini naonana naye mara moja au mbili kwa mwaka na sijawahi kukaa naye.

    wakati mwingine bwana. nilimjua mama baada ya kumaliza kidato cha nne.

    hata hivyo ni lazima tujifuze kupokea mabadililko yaani kila hali kama inavyokuja. wewe miaka yote hukujua kama mamako angekufa tu hata kama haumwi? bado unaogopa kifo mpaka unakonda?

    pole lakini samahani kama hatuelewani

    ReplyDelete
  5. Kamala nimekuelea nami nasema pole sana nawe kwa kukosa upendo wa mama. Maana hakuna kitu kizuri kama upendo wa mama kwa mtoto wake.Tupo pamoja

    ReplyDelete
  6. Ulevi na sigara hamna tofauti mvutaji sigara anajua madhara yake, Anajiua polepole bila kujua ama mlevi atafanya vitu bila kujijua.

    ReplyDelete
  7. Nimeyapenda hayo maoni ya mtoa maoni wa kwanza. Ni maoni ya kutia moyo sana. Afadhali nami ningepata mtu wa kuniambia maneno ya kutia moyo kama haya babangu alipokufa. Nimejifunza. pole Yasinta. Sote njia yetu ni hiyo hiyo moja!

    ReplyDelete
  8. Kamala, jaribu kuwa unafikiria kwanza kabla ya kuweka maoni. Eti unamwambia mtu "bora mamako kafa..." acha hii tabia ya kuropoka hovyo katika blogu za watu. Unajishushia hadhi sana bro na unatutia aibu Wahaya! Tena rekebisha uhusiano wako na mamako vinginevyo utaachiwa laana wewe uhangaike nayo. Pole dada Yasinta kwa kuambiwa eti 'bora mamako kafa"

    ReplyDelete
  9. Profesa Masangu nimesoma maoni yako nami nikafaraja japo sikuwa mlengwa hasa wa maneno hayo. Ninaamini dada Yasinta amepata faraja kwa maneno hayo yenye hekima kubwa.


    Dada yangu Yasinta pole sana. Tekeleza yote aliyokufundisha mama. Songa mbele.

    ReplyDelete
  10. Namwuunga mkono anon wa March 7, 2009 3:14 PM.

    Kamala unahitaji kutumia akili zaidi. Haukuwa na sababu ya kusema hayo ulivyosema. Mara nyingine akili ni kunyamaza unapoona huna mchango wa maana. Ni kwa sababu tu watu hawakwambii lakini unaonekana kituko kwenye michango yako mingi.

    Halafu si lazima kuwa kinyume na kila kinachofikiriwa na wengine. Usihangaike sana kuonyesha unajua negations.

    Nahisi tatizo lako limetokana na malezi mabovu uliyopata tangu utotoni. Ni vyema ukimtafuta mama yako ukazungumza naye vinginevyo utakuwa unajichimbia kaburi lako mwenyewe.

    Mjumbe hauwawi. Bora uchukie lakini tukufahamishe. Kulopoka si tabia ya kijana wa umri wako.

    ReplyDelete
  11. Kama Kamala haongei na mamake mzazi unategemea nini? Keshatupiwa lawama tayari huyo na huku ni kuhangaika tu. Nimeangalia komenti zake katika blogu mbalimbali na karibu zote ni za kutia kichefuchefu. Yeye kila kitu ni negative na hasiti kuropoka. Mtu kweli anamkumbuka mamake aliyemlea na kumpenda sana halafu wewe unamropokea eti bora mamako kafa kwa vile tu eti mamako na wewe hamsalimiani? Kweli? Tujaribuni kuwa wastaarabu jamani vinginevyo hizi blogu zitatushinda. Prof. Masangu Matondo. Nimetoa machozi baada ya kusoma hizo comments zako kwa dada Yasinta. Ni maneno ya busara mno. Pole kwa maneno hayo machafu ya Kamala!

    ReplyDelete
  12. Nisemeni walimwengu,
    Niupunguze uchungu?
    Pole sana nakwambia.

    Mola umtumaini,
    Ni faraja maishani,
    Kwa machungu ya dunia.

    Pole sana kwa kufiwa,
    Mpendwa kuondokewa,
    Kwa Mola katangulia.

    Uyatende yale mema,
    Alokuwa akisema,
    Rohoye itatulia.

    Mungu wetu awe nawe,
    Faraja 'sipungukiwe,
    Mola atakujalia.

    ReplyDelete
  13. Nami nasema asente, kwa kunipa pole, Ndiyo kazi ya Mungu lakini ni vigumu kukubaliana naye. Asante kwa shairi nzuri

    ReplyDelete
  14. nimesema bora mamake kafa. naamini kifo ni kizuri kuliko uhai ni msimamo wangu

    ReplyDelete
  15. Niliguswa sana na maelezo yako, ambayo niliyasoma siku ile ile ulipoandika. Nilielewa vizuri hisia ulizoelezea, baada ya mimi mwenyewe kufiwa na mama mwaka juzi, kule Magagura (Songea) wakati mimi nikiwa hapa Marekani. Niliona heri ningoje kidogo, niandike ujumbe wangu baadaye. Pole sana. Kama wanavyosema, yote ni kazi ya Mungu. Kaza moyo. Ingawa kusahau kuondokewa na mama haitawezekana, kidogo kidogo utapata nguvu ya kuendelea na maisha yako. La muhimu ni kumwomba Mungu amweke mama mahali Pema Peponi.

    ReplyDelete
  16. Usengwili sana niwona yatinipata moyo. Ila moyo guvina sana na nikumnogela sana mawu.Pole na veve wa myangu.

    ReplyDelete
  17. I know this if off topic but I'm looking into starting my own weblog and was curious what all is needed to get setup? I'm assuming having
    a blog like yours would cost a pretty penny? I'm not very web smart so I'm not 100% sure. Any recommendations or advice would be greatly appreciated. Thanks
    my webpage: www.navaidhenna.com

    ReplyDelete