Monday, March 31, 2014

JUMATATU HII YA MWISHO WA MWEZI HUU WA TATU TUANGALIE JINSI YA KUSEMA NENO HABARI ZA KAZI KWA BAADHI YA MAKABILA YA TANZANIA.....

Kwa vile mimi ni MNGONI basi nimeona nianze na KINGONI, na baadhi ya lugha nafahamu na nyingine nimefanya utafiti kuwauliza marafiki na ndugu. Kwa hiyo kama na wewe una lugha/kabila unajua ni namna gani kusema HABARI ZA KAZI basi usisite kuniambia au tu kuandika hapa kibarazani nitashukuru.  KARIBU:-)
1. Kingoni husema:- HABARI za MAHENGU?
2. Kipogoro husema:- HABARIza MAHENGU? pia
3. Kibena husema :- KAMWENE za MADZENGO?
4. Kinyasa husema :- HABARI za NCHITO?
5. kinyakyusa husema.- TWAMBOMBO?
6. Kimatengo husema : HABARI ja MAHENGO?
7. Kijaluo husema : WOCHI MATOCHI?
8. Kinyamwezi/Kisukuma husema :- MAMILIMO?
9. Kichaga cha Marangu/Vunjo husema:- MBONYI TSA KIRUNDIO?
10.Kikurya husema :- AGH-EMEREMO?
11. Kigogo husema :- MILIMONYI?
NAWATAKIENI WOTE JUMATATU HII YA MWISHO YA MWEZI HUU WA TATU IWE NJEMA...

Sunday, March 30, 2014

HAPA NI LEO ASUBUHI NA HIKI NDICHO KILICHOKUWA CHAKULA CHANGU CHA ASUBUHI AMBACHO MIKONO YANGU ILITENGENEZA/KAZI YA MIKONO YANGU

 MAANDAZI
Nilikuwa katika mazoezi ya kukimbia na mara nikawaza MAANDAZI ...kufika nyumbani nikaanza kushughulika. Na hapa ni kikombe changu cha chai na maandazi . Karibuni tujumuike nasi:-) JUMAPILI NJEMA SANA KWA WOTE .

Friday, March 28, 2014

MMMHHH! NINGEPENDA MLO HUU UWE MLO WANGU WA MCHANA WA LEO LAKINI....

.......duh kumbe ni ndoto tu ..kwanza unga sina...nimemaliza, pila mboga nilizoweka akiba zote nimemaliza yaani kutoka kwenye bustani yangu. Ila muda si mwingi nitaanza kulima tena kwa sasa nimewatika/atika. Ila mmmhhh mate yananitoka hapa...maana huyo samaki  eeeehh bwana weee ngoja niache...NGOJA TU NIWATAKIENI MWISHO WA JUMA MWEMA.

Thursday, March 27, 2014

PALE WAZAZI WANAPOAMUA KUWACHAGULIA WATOTO WAO WACHUMBA NA MWISHO WAKE MAISHA YANAPOKUWA MATESO...JE? NANI WA KULAUMIWA?

Mara nyingi sana nimekuwa nikifikiri hili jambo la kuchaGULIWA MCHUMBA. Nimekuwa nikijiuliza je ni nani ataishi na huyu mume au mke? Kwa bahati nzuri leo nimeamka nikiwa nikisoma mail zangu nimekutana na hii habari ambayo nimetumiwa na msomaji wa Maisha na Mfanikio...Jiunge nami na kisa hiki za huyu mdada.....
-----------------------------------------------------------------------------------------------------------------------
Kuna mwanadada mmoja ambaye ni miongoni mwa watu wasomi sana. Amemaliza chuo hapa Milimani. Wakati alipokuwa chuoni alibahatika kupata mchumba walikubaliana kuoana. Na walikuwa katika maelewano mazuri katika uchumba wao.

Baada ya uchumba huo kuendelea, aliamua kumpeleka kwa wazazi wake na kuwafahamisha kuwa mimi nimepata mtu ambaye naona atanifaa katika maisha  yangu. Baada ya kuwafahamisha, mama habari hiyo, mama wa dada huyo alikubaliana na wazo lake la kutaka kuolewa na huyo mchumba wake, lakini upande wa baba yake kulikuwa na shaka. Huyu binti alikuwa karibu sana na baba yake na aligundua kuwa baba yake hataki kukubaliana na wazo lake. Baada ya mazungumzo ya hapa na pale na baadaye mvulana yule kuondoka, binti alimfuata baba na kuzungumza naye na akasema kwa jinsi nilivyomuona huyo mvulana hakufai. Binti akamwambia si vizuri kumhukumu mtu kwa kumwangalia tu. Mimi nimekuwa naye kwa muda mrefu namfahamu vizuri sina shaka naye. Baba yake bado hakukubaliana na hilo lakini upenda wa mama yake hakukuwa na shida.

Uchumba uliendelea na yule mvulana akasema inaonyesha baba yake hataki kabisa, lakini nitaumia sana endeapo kama bado ataendelea kuwa na msimamo wake huo. Ni mtu ambaye nimekuzoea, tumeheshimiana sana. Yule binti akamwambia kila kitu kinawezekana na itawezekana tu.

Siku moja yule binti akiwa katika mizunguko yake ya hapa na pale akiwa mjini, alikutana na kaka mmoja akiwa katika mavazi ya kijeshi, na alikuwa na mwonekano mzuri sana, lakini cha kucshangaza yule kaka baada ya kumwona binti huyu aliduwaa. Baada ya kuduwaa kwa kipindi aliamua kumfuata binti na kumsalimia na kumwuliza kila kitu, na baadaye walianza kuwasiliana mawasiliano ya kawaida kabisa. Lakini mwanajeshi huyo alikuwa na mawazo tofauti, na ndipo siku moja akamweleza  kuwa angetamani siku moja awe mke wake. Yule binti akamwambia hapana, mimi tayari nina mtu wangu na tunaheshimiana sana, mwanajeshi akamwambia sawa. Kwa vile ni marafiki alimrudisha mpaka kwao, kumbe lengo lake yule kijana ni kutaka kujua binti anaishi wapi.
Na ndipo siku moja yule kijana aliamua kwenda peke yake nyumbani kwa wazazi wa binti huyo na kukutana na baba yake (Baba wa binti). Na ndipo alipozungumza ukweli wa kile alichokiona na lengo lake ni lipi. Na mzee aliweza kumdadisi kijana na kumweleza kila kitu. Kwa wakati huo yule binti pamoja na mama yake walikuwa hawapo na binti aliporudi akalezwa na baba yake kuwa kuna kijana mmoja alikuja yupo hivi na hivi aamenieleza kila kitu, nadhani huyo ndiye atakayekufaa. Binti alamwambia hapana, wewe ndiye umemwona na mimi itabidi nimwone. Baaye yule mjeshi akaja wakazungumza.
Baada ya mazungumzo marefu ya hapa na pale yule kijana mjeshi aliamua kuondoka, na kwa kuwa binti hakutaka kukofishana na baba yake aliamua kukubaliana na mawazo yake na baadaye wakamwita tena kijana huyo mjeshi. Baadaye taratibu zote za kuoana na mjeshi huyo zikafanyika, kisha binti huyo alienda kwa mchumba wake wa kwanza na kumweleza yote yaliyotokea na kumrudishia pete ya uchumba waliyovishana hapo awali. Kijana huyo alisikitika sana kwa uamuzi aliouchukua lakini hakuwa na jinsi aliamua kufuata shinikizo la baba yake. Hatimaye baadaye yule binti aliolewa na mwanajeshi na ndoa ilifungwa kanisani.
Baada ya ndoa tu, kilichotokea sasa hivi ni kwamba kosa kidogo tu anaambuliwa kipigo ambacho hajawahi kukipata, kiasi kwamba inampeleka kumkumbuka yule wa kwanza ambaye walikuwa wakiongea naye kwa utaratibu kabisa.
Ndipo baadaye binti (ambaye sasa ni mke wa mwanajeshi) akamfuata yule mchumba wake wa kwanza na kumweleza kila kinachotekea. Lakini kijana huyo aliajaribu kumweleza namana ya kufanya ili waendelee kuishi vizuri na mume wake na kuzidi kumwombea ili waishi vizuri.
Kwa wakati huu kijana huyo alikuwa bado hajaoa na anamweleza binti kuwa itachukua muda mrefu kwa sababu kwanza, itabidi nikusahau wewe, pili nikae chini  nitulie, tatu nianze upya. Hivyo itachukua muda sana.
Kikubwa zaidi ni kuwa binti hyuyo amekubali kuolewa na mwanajeshi kwa shinikizo la baba yake, lakini kinachoendelea ni kwamba kosa dogo tu anaambulia kipigo kisicho cha kawaida. Na kinachomuuma zaidi huyo dada ni kuwa walipotoka nje walienda sehemu ile ile ambayo walikuwa wakienda na mvulana yule wa kwanza na hivyo kuumia zaidi

Swali la Kapulya:- Je? huu kweli ni uungwanana? je? ungekuwa wewe ungmsikiliza baba au ungefuata jinsi moyo wako unavyopenda?

Tuesday, March 25, 2014

MAISHA NA MAFANIKIO IMECHAGUA KUWA HII IWE PICHA YA WIKI.....

Baba Simba hapa nahisi anasema anasema, vipi mama simba leo tutakula nini? ....na mama simba anafikiri kwa makini kweli...hili ni wazo langu. Je wewe mwenzangu unafikiri maongezi yao ni nini? au wanawaza nini?......  TUPO PAMOJA DAIMA!!

Sunday, March 23, 2014

KUMBUKUMBU...LEO NI MIAKA MITATU TANGU MPENDWA WETU ASIFIWE NGONYANI ATUTOKE

ASIFIWE WAKATI WA UHAI WAKE
Ni vigumu kuisahau tarehe 23/3/ 2011, siku hii ndiyo tuliyompoteza mpendwa wetu Asifiwe Ngonyani. Na leo imetimia miaka mitatu tangu ndugu yetu mpendwa Asifiwe atutoke. MWENYEZI MUNGU AILAZE ROHO YA MAREHEMU MAHALI PEMA. AMINA.....TUTAKUKUMBUKA MILELE....

Thursday, March 20, 2014

KWA KIFUPI:- HAPA NI HISTORIA YA MASHUJAA NA MAKUMBUSHA YA VITA YA MAJIMAJI SONGEA!!!

Siku ya leo nilikuwa najisomea kitabu changu kiitwacho THE HISTORY OF THE WANGONI KILICHOANDIKWA NA FR ELZEAR EBNER, OSB..Nitawaonyesha siku nyingine. Nachotaka kusema hapa ni kwamba mara nikakumbuka ziara yangu ya nyumbani Songea na hasa hapa katika makumbusho haya. Hakika kama hujafika Songea basi ukifika usikose kufika hapa Makumbushp ya mashujaa wetu. Basi fuatana nami kwa hizi picha chache na maelezo.......KARIBUNI SONGEA
 
 Maandishi yanampa msomaji picha  halisi ya historia ya Makumbusho ya Majimaji yaliyopo katika mji wa Songea kusini mwa Tanzania. Mkoa wa Ruvuma unapakana na nchi ya Msumbiji kwa upande wa kusini, Kaskazini mkoa huu unapakana na mkoa wa Morogoro, Kaskazini Magharibi mkoa wa Ruvuma  unapakana na mkoa wa Iringa, Magharibi mkoa huu unapakana na nchi ya Malawi na kwa upande wa Mashariki kuna mikoa ya Lindi na Mtwara.
Historia ya Makumbusho haya inahusu vita ya Maji Maji ilivyo tokea kati ya mwezi julai 1905 mpaka Agosti 1907. Vita hiii ilianza katika vilima vya Umatumbi kaskazini mwa mji wa Kilwa mnamo mwezi Julai mwaka 1905.
Waanzilishi wa awali wa vita hii walikuwa ni Wamatumbi chini ya uhamasishaji wa Mganga wa jadi /Nabii aliyejulikana kwa jina la Kinjeketile Vita hii ilikuwa kama moto katika nyasi kavu na kusambaa katika makabila ya Wamwera, Wangindo, Wapogoro, Wangoni, Wabena, Wasangu na wengine. Watu hawa walipigana kupinga kukandamizwa na kulazimishwa na wakoloni wa Kijerumani namna ya kuishi, mazao ya kuzalisha na nani wa kumtumikia.
 
 HAPA NI PICHA YA ASKARI WA KIJERUMANI
Jina la vita hii limetokana na imani ya matumizi ya dawa iliyochanganywa na Maji, punje za mahindi na mtama zilizosadikiwa kuwa zitampa mpiganaji kinga ya kutodhurika kwa shambulio la risasi za majeshi ya Wajerumani. Inakadiliwa watu 75,000 walipoteza maisha yao ukanda wa kusini mwa Tanzania baada ya vita. Katika eneo la Ruvuma inakadiliwa kuwa zaidi ya watu 1,000 walipoteza maisha yao.
Baada ya vita viongozi na askari walishiriki katika vita walikamatwa na kuhukumiwa kunyongwa mpaka kufa. Tarehe 27 Februari 1907 ilikuwa siku ya masikitiko makubwa kwa watu wa Ruvuma ambapo kadri ya watu 60 walinyongwa kwa sababu ya kushiriki katika vita. Mashujuaa hawa walinyongwa nyuma ya eneo ambalo leo hii linajulikana kama "Songea Club". Baada ya kunyongwa miili yao ilizikwa katika kaburi la halaiki, lililoandaliwa na wafungwa kwa muda wa miezi miwili. Siku ya tatu baadaye Chifu alinyongwa na kuzikwa katika kaburi lilikoandaliwa na kaburi la halaiki.

 
 Hapa ni kaburi la halaiki walilozikwa mashujaa wa vita ya Maji Maji, ni watu 66 walizikwa hapa.

Eneo walilozikwa mashujaa hawa limekuwa eneo muhimu sana. Tukio hili lilikuwa la kuhuzunisha sana kwa watu wetu hivyo watu hawakulizungumza kwa kitambo kirefu. Baada ya uhuru (1961). Baadhi  ya wazee walianzisha harakati za kuwakumbuka mashujaa hawa. Walianza kufanya maombi yao na maadhimisho katika eneo lililo karibu na eneo walilonyongwa wapiganaji hao. Shughuli hizi zilifanyika katika nyumba ya Padre Chengula.
Wazo la kuwa na maadhimisho ya Kitaifa lilianzishwa na kamati wa wazee wa Kingoni. Walitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa Bw. Martin Haule aliyekuwa ameteuliwa wakati huo. Baadhi ya wazee waliokuwa katika kamati hii ni pamoja na Xavery Zulu, Padre Chengula, Daudi Mbano, Ali Songea Mbano, Agatha Shawa, Alana Mbawa, Mwl. Duwe, Shaibu Mkeso na Daniel Gama.
Baada ya kuwasilishwa wazo hili kwa Mheshimiwa Martin Haule, alichukua hatua za dhati katika kulishughulikia jambo hili. hatua ya kwanza ilikuwa kutambua eneo ambalo Mashujaa hawa walizikwa. eneo hili walipozikwa Mashujaa lilitambuliwa na Bw. Jumbe Darajani ambaye alishuhudia tukio la kunyongwa kwa wahenga hawa (wakati wa utoto wake). Alama iliyotumika kufahamu eneo hili ilikuwa ni mti mmoja uliojulikana kwa jina la CHIKUNGUTI. Baada ya kutambuliwa eneo hilo mheshimiwa Haule alifanya uchimbuzi na kupata baadhi ya mifupa.
Kaburi la Songea Mbano ambaye alizikwa peke yake. Na la Mji wa Songea limetokana na jina lake.
 
Kabla ya Bwana haule kukamilisha kazi hii alihamishiwa Mkoa wa Ruvuma mwaka 1964. Wazo hili  la kuwaenzi Wahenga hawa liliibuka tena mwaka 1979 wakati Bw Laurence Gama alipoteuliwa kuwa Mkuu wa mkoa wa Ruvuma. Aliendelea na jitihada za kutekeleza wazo hili. Alianza kuhamasidha na kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa makumbusho kwa kushirikiana na wazee wa Ruvuma na wananchi wengine, ujenzi wa jengo la makumbusho ulianza na kukamilika mwaka 1980.
Pamoja na kukamilisha kwa ujenzi wa jengo hili pia zilijengwa Sanamu katika eneo la mbele ya jengo. Sanamu hizi zilijumuisha anamu ya Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Mwl. J.K Nyerere na sanamu 12 zamachifu wa kingoni. Lakini kwa sasa sanamu wa hayati Mal. J.K Nyerere imetolewa baada ya kuona haina kiwango cha juu, hivyo inaandaliwa upya ili iweze kuwekwa upya . Kazi ya kutengeneza sanamu hizi ilifanywa na msanii mmoja huko Arusha.
Vifaa vya awali katika makumbusho haya vilitengenezwa na Mheshimiwa Laurence Gama, Padre Chengula na baadhi ya wazee. Vifaa vilivyokusanywa vilijumuisha ni silaha zilizotumika wakati wa vita ya Maji Maji kama vile:- Kwa lugha ya kingoni Chikopa (Ngao), Chibongo(Rungu), Chinjenje (Kishoka), pia baadhi ya viti vilivyotumiwa na Chifu Mputa,vifaa vya ndani na nguo za magome ya miti.
Kwa Hiyo kuanzia mwaka 1980 baraza la wazee lilianza kuadhimisha maombolezo ya mashujaa walionyongwa kila ifikapo tarehe 27/2 ya kila mwaka. Makumbusho haya yalifunguliwa rasmi tarehe 7/7/1980. Kuanzia hapo makumbusho haya yaliendelea kutoa huduma chini ya usimamizi wa Mkoa wa Ruvuma na wazee wanaendelea kufanya maadhimisho ya siku ya Mashujaa katika eneo la Makumbusho haya kila mwaka. Baadhi ya wazee ndio ambao wamekuwa wakitoa maelezo kwa wageni wanaotembelea makumbusho haya. Tarehe 1/9 2005 makumbusho haya yalikabidhiwa kwa Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Miaka 100 ya vita ya Maji Maji iliadhimishwa Kitaifa katika Makumbusho haya tarehe 27/2/2006 na yalizinduliwa rasmi na Rais wa Tanzania Mhe. Jakaya Kikwete.
TUWAKUMBUKE MASHUJAA WETU DAIMA  WALIFANYA KAZI KUBWA SANA..
 

Tuesday, March 18, 2014

KAPULYA NDANI YA NYEUPE NYEUPE..KUMBE NYEUPE NAYO NZURI!!!

 Hapa ilikuwa 2011
 Hapa 2013
Na hapa ni 2014 ingawa sketi si nyeupe  ila inaelekea huko huko...Kwa kawaida nilikuwa si mpenzi sana wa rangi nyeupe zaidi ya nilipåokuwa shule ya msingi, yaani kuvaa shati nyeupe. Na pia ile ndoto yangu ya kuwa sista maana ningekuwa navaa. Ila sasa ....kama watu wasemavyo mtu hubadilika napenda nyeupe ila sana sana nyeusi na  kijani:-).....SWALI:- Je wewe una rangi ambayo unaipenda sana kupita zote?

Monday, March 17, 2014

EBU JUMATATU HII YA LEO TUANZE NA MSEMA HUU CHEKA UNENEPE:- VICHEKESHO VYETU!!

Katika kuhakikisha wanafunzi wa darasa la kwanza wanaelewa, mara nyingi walimu hutumia mifano mingi sana, nakumbuka baba yangu alivyokuwa akitupatia mifano mingi ili tuelewe...haya fuatana nami na mahojiano yafuatayo ambayo mwalimu alikuwa anajitahidi kuwaelewesha wanafunzi wake:-

Mwalimu:- Nikikupa chapati sita halafu ukala mbili zitabaki chapati Ngapi?
Mwanafunzi:- Ukinipa na chai ya maziwa haitabaki hata chapati moja.

HAYA NIKUTAKIE JUMATATU NJEMA SANA  NA PANAPO MAJALIWA TUTACHEKA TENA JUMATATU IJAYO:-)

Saturday, March 15, 2014

NAPENDA KUWATAKIENI WOTE JUMAMOSI NJEMA /MWISHO WA JUMA UWE MWEMA KWA UJUMLA...UPENDO!!

Upendo ndiyo maji ya pekee yawezayo kakausha  kiu ya moyo wako/mioyo yetu.
JUMAMOSI NJEMA!!!!!!!!

Thursday, March 13, 2014

UJUMBE HUU UNANIPA UTATA...MIPANGO YA MUNGU! KWELI?

Ni MIPANGO YA MUNGU KWELI? Nimejiuliza na mwisho nimeona ni afadhali niulize maana palipo na wengi hapaharibiki kitu. Na kuuliza si UJINGA.  Kapulya wenu...

Wednesday, March 12, 2014

SEHEMU FULANI TANZANIA :- TWENDEN WADOGO ZANGU TUTACHELEWA NAMBA....

Picha hii imenikumbusha enzi hizo:Amka, amka kumekucha x2  Twendeni shuleni.  au Panda, panda  panda, panda mlima panda  panda.....hapo mtu ulishaoga na sasa josho linakuvuja tena ...Duh  kaazi kwelikweli....Je? hapa ni mazingira ya wapi katika Tanzania yetu?

Tuesday, March 11, 2014

MAISHA YA NDOA:- KWA NINI NIMEMWOA?

LEO NIMEAMKIA KUSOMA SOMA KATIKA MOJA YA HABARI NILIZOSOMA NI HII NIKAONA NIWASHIRIKISHE PIA. NI KUTOKA KATIKA KITABU:- NJIA YETU KWA MAPENDO NA NDOA. KARIBUNI......
Vincent na Regina walikuwa wa kabila moja. Na walikuwa wamesoma shule moja. Vincent alikuwa amemaliza darasa la 5 lakini ilimbidi kuacha kwa sababu hakuwa na mtu wa kumlipia karo/ada za shule. Regina naye alipaswwa kuachia darasa la 3. Wazazi wake, kama vile wazazi wa Vincent, walikuwa wakulima. Lakini kwa sababu ya uhaba wa mvua kwa miaka kadhaa iliyoopita, wazazi wake walipaswa kuhamia mahali pabaya pasipokuwa na shule karibu.
Vincent alijiunga na baba yake shambani. Regina, baada ya miaka kadhaa alikwenda kufanya kazi kwa wazungu fulani katika mji wa karibu. Alikuwa yaya. Waajiri wake walikuwa wakarimu kwake na mara nyingi walimpa vitu vingi vizuri. Kila wiki alipokea mshahara wake lakini mara nyingi zaidi yeye aliutumia mara tu alipoupokea.
Siku ya soko kila wiki, Vincent alizoea kwenda mjini na bidhaa za kuuza. Lakini kila mara alihakikisha kwamba amemwona Regina kabla ya kurudi nyumbani. Bila shaka siku nyingine Regina alipaswa kufanya hiki  na kile, hivyo hakuweza kuondoka na kufika sokoni. Siku hizo, Vincent alirudi nyumbani akisemasema manenoo yasiyosikika, hivyo mara nyingi wazazi wake walijiuliza ikiwa Vincent ni mgonjwa?
Mwishowe, Vincent na Regina walioana. Vincent alikuwa amejenga nyumba mpya nzuri kwa ajili yao wawili. Mwanzoni kila kitu kilionekana chema kabisa. Ni kweli kwamba mara kwa mara Vincent alikuwa na wasiwasi juu ya Regina. Alijua kwamba Regina alikuwa amejifunza mitindo ya kigeni kwa wale wazungu katika nyumba ile kubwa. Basi, alijisemea kwamba baada ya muda Regina atayasahau kabisa hayo yote na kuwa mmoja wao tena.
Lakini Regina hakuweza kusahau. Alikumbuka vyakula vizuri, sahani na vikombe vizuri, viti n.k. Yeye hatakuwa kamwe na nyumba ya namna hiyo. Polepole alianza kubadili mwenendo wake kwa Vincent. Alikuwa mkimya kabisa, lakini pengine ukimya wake ulibadilika hata ukamfanya afadhaike na kukasirika kwa sababu ya jambo alilosema au alilofanya Vincent.
Kadiri alivyokasirika zaidi, ndivyo alivyojitahidi kumpendeza zaidi. Hakusema chochote aliporudi nyumbani toka shambani akiwa amechoka na kusikia njaa na kukuta chakula hakijawa tayari. Alikumbuka vema aibu aliyopata siku ile ambayo baba na mama waliwatembelea, na Regina akagoma kuwapikia chakula. Usiku, walipokuwa wameondoka, alimpiga Regina, ilikuwa ni mara ya kwanza kwake kufanya hivyo.
Toka siku hiyo mambo yalizidi kuwa mabaya. Regina aliishi katika nyumba kwa ukimya wa kitoto. Alimjibu Vincent kwa kuguna kila alipomwuliza swali. Hata mara nyingine alikataa kulala na Vincent mpaka naye aahidi kumtendea tendo fulani. Vincent maskini! Hakujua la kufanya. Mara nyingi sana alijisemea: "Maisha ya mjini yamemharibu, kabla yake hakuwa hivi". Alisema kwa sauti ndogo:- "Kwa nini nimemwoa?
Alizidi kutumaini kwamba Regina atabadilika. Miaka ilivyopita Mungu aliwajalia watoto wawili, mvulana na msichana. Hizi zilikuwa ndizo siku njema, wakati kila kitu kilipoonekana kinakwenda sawa tena. Regina alionekana kuwa mtu ambaye Vincent amemtumaini kuwa naye. Lakini jambo fulani likitokea basi, Regina alikuwa anabadilika upesi. Alikuwa anakataa kufagia nyumba, au kupika chakula au hata kuwatunza watoto kwa ujumla.
Wakati kama huu, Vincent alikuwa anajiuliza tena na tena:- "Kwa nini nimemwoa?
Je? hapa wa kumlaumu ni nani na wa kumsikitikia ni nani?
KILA LA KHERI...PANAPO MAJALIWA TUTAONANA TENA!!!

Sunday, March 9, 2014

JUMAPILI YA LEO TUSALI KANISA HILI LA WINO/PAROKIANI

Kanisa hili la Wino lina historia yake fupi katika familia ya akina Ngonyani. Ni kwamba baba yangu mkubwa ameshiriki ujenzi wa kanisa hili. Basi kwa kahistoria haka kafupii napenda kuwatakieni wote JUMAPILI  NJEMA pia kumbukeni mfungo wa PASAKA umeanza....Ni mimi Kapulya!!

Saturday, March 8, 2014

BLOGG YA MAISHA NA MAFANIKIO KATIKA SIKU HII YA WANAWAKE DUNIANI IMECHAGUA WIMBO HUU WA DADA FLORA MBASHA MAANA UMEBEBA UJUMBE MWANANA!!! UKIPATA WASAA SIKILIZA....


NAPENDA KUWATAKIENI JUMAMOSI HII YA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI IWE NJEMA SANA. HONGERA WANAWAKE WOTE KWA SIKU HII! JUMAMOSI NJEMA KWA WOTE ...Mwanamke simama imara wewe ni jeshi kubwa ujitambua.....na kuendelea

Friday, March 7, 2014

TUMALIZE MALIZE HILI JUMA KWA PICHA HII:- NI SEHEMU FULANI KATIKA AFRIKA/TANZANIA YETU

  
Nimejikuta ghafla kama ndo mimi na mama tukitoka shambani kupanda mbegu za mahindi au mpunga na tunaporudi tumeokota na kuni. Maana kifuku hiki sasa bila kuni hakuna huwezi kutoa chakula kilichoiva ...Duh! nimekumbuka sana enzi zile...Je? wewe unakumbuka kazi gani ulikuwa unaifanya sana au ulikuwa hupendi kuifanya:-)....NAWATAKIENI WOTE IJUMAA NJMA NA PIA MWANZO MWEMA SANA WA JUMA KWA UJUMLA...KAPULYA.

Thursday, March 6, 2014

TUSISAHAU TULIKOTOKA:- UDONGO NA MANUFAA YAKE......

Lengo kuu zaidi la kuweka vifaa hivi vya asili ni kutaka kumjibu ndugu yangu KACHIKI katika mada yake kuhusu mitungi/vyungu. na je kwa lugha yangu vipi tunaita?
Chungu kikubwa kidogo ambacho kama familia ni kubwa waweza kupikia chakula kushiba kama vile Makande, au kitoweo:-) Au pengine hata kuwekea maji ya kunywa kama nifanyavyo mimi hapa:
Na hapa ni vyungu vya kawaida kwa kupikia mboga. Nakumbuka hapo zamani vyungu vilitumika kupikia kila na vyakula vyake vilikuwa vitangu sana kwa kweli. Kuna ule utamu wake wa asili ambao ni vigumu kuuelezea ..si kama kupika mboga ,maharagwe, na nyama kwenye sufuria
Undongo wa mfinyazi unaweza kutumika kwa kutengeneza vitu vingi sana ..hapa ni vyombo mbalimbali ..hicho kibakuli ni kwa ajili ya kuwekea sukari au mimi nafanya hivyo..na hivyo vingine ni mapambo tu unaweza kuwekea maua au kuweka kama vilivyo.
Kachiki NAJIBU SWALI LAKO ni kwamba ninavyo kote kote na vilifika salama kabisa kama uonavyo katika picha.  Vyungu kwa KINGONI twaita CHIVIGA na mtungi CHIHULU/CHIFULU. NAPENDA KUWATAKIENI WOTE ALHAMIS NJEMA SANA PANAPO MAJALIWA TUTAONANA TENA:-)

Wednesday, March 5, 2014

RABIA: MALARIA IMENIFANYA NIWE MWALIMU MLEMAVU WA KUSIKIA...

Katika pitapita zangu nikakutana na habari hii ambayo imenigusa sana na nimeona niwashirikishe kama mlikuwa hamjaisoma basi chukua dakika chache na tujadili kwa pamoja...KARIBUNI...
Mwalimu Rabia Abdallah
“Mwaka 1996 hadi 1998, nikiwa nasoma chuo cha ualimu Korogwe mkoani Tanga, nilidharaulika sana na kuonekana kama kituko kwa baadhi ya walimu na wanafunzi, huku wengine wakishangazwa nami kwa jinsi nilivyoweza kumudu masomo yangu wakati sina uwezo wa kusikia,’’ ndivyo anavyoanza Rabia Abdallah (34) ambaye alikuwa mwalimu wa shule ya viziwi Buguruni akielezea jinsi matatizo ya kusikia yalivyomfanya aonekane kituko wakati alipokuwa akisoma.
Anasema jinsi alivyokuwa akisoma ni Mungu tu ndiye aliyekuwa akimsaidia kwani hakuwa akisikia chochote zaidi ya kusoma vitabu baada ya walimu kumaliza kufundisha na njia hiyo ya kusoma vitabu ndiyo iliyomwezesha kushinda mitihani yake na kufanikiwa kutunukiwa Diploma yake ya Ualimu.
“Wengi hawakuamini na walifikiri naigiza lakini wengine waliamini lakini hawakuweza kunisaidia kwa kuwa hakuna aliyekuwa akiweza kuzungumza kwa ishara kwani hata mimi mwenyewe sikuweza kuwasiliana kwa ishara kwa wakati huo, hivyo maisha ya masomo pale Korogwe yalikuwa magumu mno kwa upande wangu…,’’
anasema Mwalimu huyo ambaye hivi karibuni amepokea barua ya uhamisho ikimtaka kuhamia katika darasa maalumu la wanafunzi wenye ulemavu wa kusikia (viziwi) katika shule ya msingi Temeke. Rabia kwa sasa ana watoto wawili, anasema alifikiri kuwa kupata Diploma kungekuwa mwisho wa matatizo yake kumbe ndiyo kwanza matatizo yalizidi kuongezeka, kwani baada ya hapo alikumbana na tatizo la kupata kazi kwani kila alikoomba kazi ya kufundisha alikataliwa kwa kutokana na matatizo yake ya kusikia.
“Tatizo liliibuka upya nikaanza kudharaulika tena kila nilipokuwa nikiomba kazi kwani waliniita kiziwi nisiye na uwezo wa kufanya lolote na walishangaa ilikuwaje nimepewa Diploma wakati ninamatatizo hayo, waliamini kuwa mwenye matatizo ya kusikia hawezi kusoma tena maishani mwake,’’ anasema Rabia.
“Hapo nikalazimika kuomba kazi za kawaida ambapo nilipata kazi ya muda katika taasisi ya CCBRT ambapo nilifanya hapo kwa muda wa miaka mitano kuanzia mwaka 2000 hadi 2005, nikaona tangazo la kazi kwenye gazeti, likieleza kuwa manispaa ya Ilala inataka mwalimu wa kufundisha walemavu wa kusikia katika shule ya Buguruni Viziwi, nikaomba na nilipokubaliwa nikaacha kazi CCBRT,’’ anasema Rabia.
Anasema hata hivyo haikuwa rahisi kama alivyodhani hapo alitakiwa kusoma kwanza katika chuo cha walimu wanaofundisha elimu ya watu wenye ulemavu wa kusikia katika chuo cha Patandi kwa ngazi ya Diploma ndipo apate kazi ya kudumu alikubali na kwenda kusoma.
“Nilikwenda huko lakini nilipoomba wanipatie fedha za kunisomesha walisema nitumie zangu kisha baada ya kumaliza manispaa ingelipa lakini tangu 2005 hadi leo sijalipwa chochote na ndiyo kwanza nimepokea barua ya uhamisho wa kutakiwa kwenda Temeke lakini nao hauna fedha za uhamisho, hata sijui kwa nini,’’ anasema Rabia.
Hata hivyo licha ya kusoma katika chuo hicho maalumu kwa walimu wa kufundisha watu wenye ulemavu wa kusikia, Rabia anasema alipomaliza masomo yake hakuwa akijua kutumia ishara jambo lililomlazimu kujiunga na chama cha walemavu wa kusikia ambapo alijifunza na kufahamu vizuri lugha ya ishara.
Akizungumzia jinsi alivyopata ulemavu wa kusikia, Rabia anasema alizaliwa akiwa anasikia kama kawaida lakini alipofika darasa la nne akapatwa na malaria kali ambayo ilimlazimu kutumia dawa kwa muda wa mwezi mzima na baada ya kupona taratibu uwezo wa kusikia ukawa ukipotea na hatimaye hakuweza kusikia tena hadi leo.
Rabia ambaye ni mkazi wa Ilala Sharifu Shamba anasema kipindi hicho alikuwa na miaka nane.
“Taratibu nilijikuta nikipoteza uwezo wa kusikia lakini kipindi hicho nilipata shida sana kwani wazazi na ndugu zangu walidhani nimeanza jeuri hivyo walikuwa wakinipiga makwenzi na kunidhihaki sana bila kujua kuwa nilikuwa sisikii,’’ anasema Rabia kwa kusikitika.
“Unajua hawakuwa wakijua kama nimepoteza uwezo wa kusikia, kwa kuwa mara kwa mara mama alikuwa akiniita lakini sikuwa nikiitika kwa kuwa nilikuwa sisikii hivyo alikuwa akikasirika sana na kunipiga mara kwa mara na ndugu zangu nao pia walikuwa wakinipiga makonzi, iliniuma sana lakini sikuwa na jinsi ya kuwaeleza wasifanye hivyo,’’ anaendelea kueleza Rabia.
Anasema hali hiyo iliendelea kwa muda mrefu lakini baadaye baadhi ya majirani waliingiwa na wasiwasi na hali hiyo na kumweleza mama yake na ndugu zake kuacha kumpiga makonzi kwani huenda mtoto huyo akawa na matatizo ya kusikia hivyo walimtaka mama yake kwenda kumchunguza masikio hospitalini na alipofanya hivyo iligundulika kweli hakuwa na uwezo wa kusikia.
“Matokeo hayo yalimuhuzunisha sana mama, nilimuona akijisikia vibaya kwa kuwa alikuwa akinipiga makwenzi kwa kudhani kuwa nilikuwa jeuri, lakini hakukuwa na la kufanya, kipindi hicho hakukuwa na shule za wenye ulemavu huo hivyo nikalazimika kusoma kwa kuchanganyika na wanafunzi wasio na matatizo kama yangu,’’ anaeleza Rabia.
Kwa masikitiko Rabia anasema kuwa yeye alikuwa katika hali ngumu kwani ilipofika kipindi cha mitihani hasa somo la Imla hakuwa akiambua kitu na wala hakuwa akipata msaada wowote kwa kuwa walimu wenyewe waliokuwa wakisimamia mitihani hawakuwa wakijua kuzungumza kwa ishara.
‘‘Hivyo katika mitihani yangu yote kuanzia darasa la nne nilikuwa nikikosa maswali yote ya Imla na yale ambayo yalikuwa yamekosewa na kubadilishwa kwa kusomwa kwa kuwa sikuwa nikisikia kitu zaidi ya kuhisi baadhi ya mambo, lakini nashukuru Mungu licha ya kushindwa Imla katika kila mtihani wangu, Mungu alinisaidia nikafaulu mtihani wa darasa la saba na kuchaguliwa kidato cha kwanza katika shule ya sekondari Kisutu,’’ anasema Rabia.
Anasema sekondari nako kulikuwa kugumu zaidi kwani alikuwa hasikii na lugha iliyokuwa ikitumika ni Kiingereza ikawa ngumu kutambua kwa kuangalia mdomo wa mwalimu kwa kuwa maneno hayo hakuwa akiyafahamu, ikawa ngumu kwake kung’amua lolote hata alipojaribu kumuangalia mwalimu wa somo anavyotamka maneno.
Rabia alimaliza sekondari na kupata daraja la nne la pointi 26 hivyo akachaguliwa kujiunga na Ualimu katika chuo cha ualimu Korogwe Tanga.
“Nina ombi kwa serikali, naomba wabadilishe mfumo wa mitihani ya shule za msingi kwa wanafunzi wenye ulemavu wa kusikia, maswali yasifanane na wasio na matatizo hayo ili kila mtu awe na uwezo wa kujibu na pia wasimamizi wa mitihani hiyo wawe walimu wenye uelewa na watu wa namna hiyo,’’ anasema Rabia.
Makala haya yameandikwa na Festo Polea wa Gazeti la Mwananchi

Tuesday, March 4, 2014

UTAMU WA VYAKULA VYA ASILI ..MABOGA, MAHINDI NA MAGIMBI

Asubuhi ya leo nimeamka huku nikiwa na hamu ya chakula hiki cha asubuhi. Maana huu ndio msimu wake hasa kwetu Songea maana ndio msimu wa mvua....mmmmhhh....halafu nikakumbuka ....

 ..mahindi jinsi mtu aendavyo tu shambani kukata/kuvunja mahindi na kwendajikono kuchoma au kuchemsha pamoja na maboga wakati huko nje mvua inanyesha..Ahhh nausikia utamu wake. Halafu nina kahadithi kamoja kuhusu mahindi  tulikuwa tunaitumia sana tulipokuwa wadogo inakwenda hivi:- Kila mtu anakuwa na muhindi, sasa wale wadogo huwa hawawezi kula basi wakubwa walikuwa wakiwaambia leta mimi nikutengenezee barabara ya kwenda ....anataja mji. Sasa yule mdogo aelewi anampa kumbe mwenzake yale mahindi atengenezayo barabara yote yanaingea tumboni ...Utoto bwana. Nilijaribu siku moja na wanangu, nilifanikiwa:-)...mmmhh ngoja niache  niwahi Madaba/matetereke

...maana ndiko nilikojifunza/onja mara ya kwanza Magimbi. Kwa hiyo leo nimekaa na kuota vyakula vingi. Natamani magimbi haya yawe mlo wangu wa mchana huu. Je kuna mlo ambao na wewe unautamani/hujala muda mrefu?

Monday, March 3, 2014

JUMATATU YA LEO TWENDE KUWATEMBELEA NDUGU /JIRANI ZETU HUKO MBINGA!!!

Najua Mbinga kuna milima na mabonde mengi sana. Lakini hapa nimejiuliza hawa waliojenga hizi nyumba ama kweli wana moyo kweli...hapa ni MBUJI ROCH  ILIYOPO LIULI MBINGA...Basi ufikapo Mbinga usikose kutembelea ..

Sunday, March 2, 2014

KATIKA JUMAPILI HII YA KWANZA YA MWEZI HUU WA TATU TUANGALIA HILI, MKE:- FURAHA YA MUME WAKE!

Kitabu cha Mithali kinaeleza jinsi mwanamke mkamilifu alivyo, mwanamke aliye furaha na fahari ya mume wake. Mwanamke huyu anafanya kazi zake kwa bidii, ana hekima, ni mwaminifu na hutunza kwa uaminifu watu na vitu vya nyumbani. (Mit. 31:10-31)