Monday, February 28, 2011

MWANAFUNZI WA MIAKA 12 KUWA MKE WA TATU WA MZEE VISENTI HAULE

Habari hii imenigusa sana sana sanaaaaaaa na nimeona niiweke hapa Maisha na mafanikio ili tuweza kujadili pia kwa pamoja. Jamani hivi SHERIA zinatungwa ili iweje??? Baada ya kusoma habari hii nimekuwa ninajiuliza:- Hivi huu ni mwisho wa dunia? Au wanawake wamekwisha? Miaka 12 kuanza maisha ya ndoa halafu mke wa tatu kweli huu ni uungwana/utu kweli?
Makala hii nimeipata hapa kwani naamini wote tuna nia ya kueleimisha jamii.
Haya hapa ni habari yenyewe tuwe pamoja.

Binti wa miaka 12 katikati Veronika Charlle wa darasa la tano, akiwa na mwenye kiti wa kijiji cha Sinai Talisis Mkanula na mhudumu wa afya msingi Christina Njovu.walijaribu kumsaidia mtoto huyo lakini kukawa na urasimu wa kushindwa kumchukulia hatua mtuhumiwa Bwana Vinsenti Haule kwa kesi ya ubakaji maana huyu mtoto ni sawa na mjukuu wake.

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida Vinsenti Haule mkazi wa kijiji cha Sinai Peramiho wilayani Songea mkoani Ruvuma ambaye ana wake wawili amemuoa mwanafunzi wa darasa la tano wa shule ya msingi Nakahuga Veronika Challe(12) kuwa mke wake wa tatu.Imeripotiwa na Albanos Midelo.

Sunday, February 27, 2011

JUMAPILI NJEMA KWA WOTE:- Ni jumapili ya 8 ya mwaka A

Baba yetu uliye Mbinguni,
Jina lako litukuzwe,
Ufalme wako ufike,
Utakalo lifanyike , duniani kama Mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku,
Utusemehe makosa yetu, kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea.
Usitutie katika vishawishi, lakini utuokoe maovuni.(Kwa kuwa ufalme ni wako, na nguvu, na utukufu, hata milele Amina)




JUMAPILI NJEMA KWA WOTE NA MWANZO MWEMA WA WIKI...TUTAONANA TENA WAKATI MWINGINE

Friday, February 25, 2011

PICHA YA WIKI:- DAIMA KUNA KUWA NA UFUMBUZI!!!!

Harusi yako haiwezi kushindikana kwa sababu ya keki. Daima kuna kuwa na ufumbuzi.Hebu angalia hiyo picha hapo juu. HAKUNA LISILOWEZEKANA:-)
NAWATAKIENI WOTE IJUMAA NJEMA!!!!

Wednesday, February 23, 2011

BLOG YA MAISHA NA MAFANIKIO YATIMIZA MIAKA MITATU LEO!!!

Hapa ni Mwenyewe Mama
Maisha na Mafanikio!!!
Ni kama vile mtoto azaliwapo na kukua katika hatua tofauti tofauti, na mara nyingi hatua hizo huenda sambamba na mabadiliko ya kimwili na kiakili.
Leo hii Blog hii ya Maisha na Mafanikio yatimiza miaka mitatu kamili huku nikijivunia mafanikio niliyoyafikia tangu nilipoianzisha blog hii. Kama nilivyosema hapo awali kuwa mtoto anapozaliwa hukua katika hatua tofauti tofauti na hivyo ndivyo ilivyo kwa blog hii ya Maisha na Mafanikio. Kwani nilianza kama masihara kuandika habari mbalimbali za kijamii, za kufurahisha, za kuhuzunisha na za kuburudisha pia, na kupitia michango ya wasomaji na wanablog wenzangu nimeweza kujifunza mambo mengi sana. Kwa sababu hii napenda kuchukua nafasi hii na kusema AHSANTENI SANA KWA USHIRIKIANO WENU KWANI NAAMINI BILA NINYI, NISINGEFIKA HAPA LEO. KWA KWELI NAAMINI KUWA SISI SOTE NI NDUGU NA NI WATOTO WA BABA MMOJA.UPENDO NA UMOJA WETU UDUMU DAIMA NA PIA MILELE!!!!!

Tuesday, February 22, 2011

SIKU AMBAYO SITAISAHAU

Restieli akiwa amejipumzisha nyumbani
kwao Njoro baada ya kutoka shuleni
Leo hii nimepokea waraka huu kutoka kwa binti Restieli Moses Mbwambo aishiye kule Moshi Kilimanjaro, waraka ambao umetumwa kwa msaada wa mdau wa BLOG YA MAISHA NA MAFANIKIO aliyeko kule MOSHI. Na mie bila kuongeza wala kupunguza neno nauweka kama ifuatavyo:

Ni siku ambayo niliungua na mafuta wakati nilipokuwa mdogo wa umri wa mwaka mmoja na nusu. Ukweli ni kwamba nilisimuliwa na wazazi wangu jinsi tukio hilo lilivyotokea kwa kuwa mri wangu ulikuwa ni mdogo. Walinisimulia kuwa tukio hilo lilitokea hapo mnamo tarehe 17 Julai 2002, siku ya Jumatano jioni.
Siku hiyo mama yangu alikwenda kurekodi nyimbo zao za kwaya huko Arusha na baba alikwenda kanisani kuhudhuria ibada ya jioni katika kanisa lao la Njoro SDA lililopo hapa mjini Moshi, hivyo akaniacha na jirani ili aniangalie.
Wakati baba ananiacha na jirani yao, alikuwa ndio kwanza anajiandaa kuchoma maandazi yake kwa kuwa alikuwa ni mfanyabiashara wa maandazi pale mtaani.
Kutokana na sijui udogo au utundu naambiwa kuwa nilikwenda kwenye kikango cha mafuta na kukishika ambapo kilipinduka na yale mafuta ambayo yalishakuwa yamepata moto yalinimwagikia mwili mzima na kunisababishia majeraha na maumivu makali.
Baba alijulishwa na aliporudi nyumbani akakuta nimeshapelekwa hospitali ya Mawenzi na baadae nikahamishiwa Hospitali ya KCMC kwa ajili ya matibabu.
Mama alirudi majira ya saa kumi na mbili jioni na kujulishwa juu ajali iliyonipata, akaja haraka hospitalini.
Kwa kweli niliungua sana kwa kuwa mafuta yalikuwa ni ya moto sana. Watu walitoka kanisani walipokuwa wakimuimbia mungu na kuja Hosptalini kuniona.
Siku ya Jumamosi ambayo ni siku a sabato ilitangazwa pale kanisani juu ya ajali iliyonipata hivyo waumini wote walipotoka kanisani walikuja moja kwa moja kuniona na walikuwa wengi sana.
Nikiwa ndio nimetimiza miaka kumi mwaka huu, nimelikumbuka sana tukio hili na ndio maana nikaamua kukaa chini na kuandika kumbukumbu hii na kumpa mama na baba yangu kama kumbukumbu ya tukio hilo la kusikitisha.
Namshukuru mungu sana kwa kunilinda mpaka sasa nimetimiza miaka kumi, jina la Bwana lipewe sifa.
Pia nawashukuru wazazi wangu, majirani na washirika wa kanisa la Njoro SDA kwa kuwa karibu na wazazi wangu katika kipindi chote cha madhila yangu.
Natoa wito kwa wazazi na walezi kuwa makini wanapokuwa au wanapoachiwa watoto wadogo kuwaangalia, kwa kuwa watoto hawajui vitu vya hatari, kama moto, visima, magari na kadhalika.
Tarehe 17 Julai 2002 ni siku ambayo sitaisahau
Ni mimi Restieli Moses Mbwambo wa Njoro Moshi.

Monday, February 21, 2011

HONGERA KWA SIKU YA KUZALIWA KWAKO CAMILLA !!!/Grattis på Födelsedagen Camilla!!!

Miaka 13 imepita leo tangu binti yetu Camilla azaliwe. Ni binti ambaye anapenda sana kusoma, kuandika, kucheza mpira wa mikono (handball) anapenda michezo ya kuigiza na kuimba. Twakuomba Mwenywezi Mungu uwe /uzidi kumbariki binti yetu Camilla azidi kuwa kama alivyo. Na pia twakuomba uzidi kutupa sisi wazazi/walezi nguvu ya kumlea ili azidi kuwa binti mwema na mwenye busara. CAMILLA HONGERA SANA KWA SIKU YA KUZALIWA.!!!!!
na hapa ni mziki ambao napenda kusikilizakwa hiyo leo ni siku yangu na nataka kusikiliza pamoja nanyi



.

Sunday, February 20, 2011

UJUMBE WA JUMAPILI HII YA NANE YA MWAKA!!

Unapotafakari mema ya Mungu ya leo:-

WASAMEHE WALIOKUKOSEA,

WAKUMBUKE WALIOKUSAHAU na UILINDE AMANI YA MOYO ISIPOTEE.

Kwani utakuwa na furaha daima!!!




JUMAPILI NJEMA NDUGU ZANGUNI!!!!

Friday, February 18, 2011

NAWATAKIENI WOTE MWISHO WA JUMA/IJUMAA MWEMA/NJEMA!!!



Jamani! Siku zinakimbia kwelikweli leo ni Ijumaa nyingine tena. Ni mwisho wa juma unaanza wengi wetu tumekuwa katika pilikapilika na sasa ni wakati wa kupumzika na wengine ndo kazi kama kawaida. Kwa hiyo kwa wale watakaopumzika na wale wataofanya kazi, napenda kuwatakieni mapumziko mema na kazi njema. Na ndiyo nikaona niwatakieni na mziki kidogo kwani kama tusemavyo kazi na mziki na mapumziko na mziki. Haya ni wakati wa discooooooooooooo. IJUMAA NA MWISHO WA JUMA UWE WENYE FURAHA KWA WOTE.TUONANE TENA WAKATI MWINGINE!!!!

Tuesday, February 15, 2011

MAPAPAI :- UTAMU ,FAIDA NA MATUMIZI YAKE!!

Hapa ni mti wa papai, leo nimekumbuka faida mbili za majani ya mipapai moja ni dawa ya tumbo hasa kama una tatizo la choo kubwa . Unachukua hayo majanai na unachemsha na halafu unakunywa yale maji yake. Pili ni sabuni unaweza au niseme mimi nimewahi kufulia nguo ila usifulie nguo nyeupe basi itakuwa kijana. Nguo nyingine zote sawa kabisa.
Na hapa ni tunda lenyewe nalo lina faida zake kwanza ni kwa ajili ya kula ni tamu sana na pia nalo kama una tatizo la choo kubwa ni nzuri. Halafu jambo jinginge papai ni kilainisho kizuri sana cha chama hasa nyama ya ngómbe. Toa hizo mbege weka kwenye chombo, pondaponda papai na uchanganya na hizo mbegu koroga taratibu katakata nyama vipande vidogovodogo weka humu kwenye mpondo na subiri masaa kadhaa. Hakika utaifaidi nyama yako mno itakuwa lainiiii. Ila kusema kweli nimetamani kweli papai ni muda sasa sijala:-)

Monday, February 14, 2011

Swali la JUMATATU HII!!!

katika ukuaji wangu sikuwahi kusikia watu wakitakiana siku ya kuzaliwa na kuna wengine hata hawajui lini wamezaliwa.

Pia sikuwahi kusikia watu wakitakiana siku ya wapendanao. Au siku ya "Halowini" Hivi ni kwa nini imekuwa hivi? Nimewaza tu kwa sauti!!!

Sunday, February 13, 2011

Jumapili ya leo, Mke: Furaha ya mume wake!!! na ni jumapili ya saba ya mwaka!!


Mwanamke ni furaha ya nyumba!!

Kitabu cha Mithali kinaeleza jinsi mwanamke mkamilifu alivyo, mwanamke aliye furaha na fahari ya mume wake. Mwanamke huyu anafanya kazi zake kwa bidii, ana hekima ni mwaminifu na hutunza kwa uangalifu watu na vitu vya nyumbani. (Mit. 31:10-31)

Kitabu kingine, Hakima ya Yoshua bin Sira, kinamsifu mume mwenye mke wa namna hiyo:-

Apataye mke hujipatia mali iliyo bora, msaidia wa kufaa, na nguzo ya kumtemeza. (Y. b. s. 36: 24).

Yu heri mume aliye na mke mwema kweli,

Mwanamke mwema ni furaha ya mume wake,

Ataishi miaka ya maisha yake katika amani.
Mwanamke mwema ni tunu bora,
Mcha Mungu atatunukiwa huyo watajaa furaraha moyoni hata kama ni maskini au tajiri,
Watakuwa na nyuso zilizochangamka wakati wowote. (Bin Sira 26: 1-4)
Hivi ndivyo mwanamke anavyokusudiwa kuwa kwa mwanaume. Katika maneno yake Mungu kwa nabii Ezekieli, mwanamke huwa; "Furaha ya macho". (Ez. 24-16).

Lakini kwa nabii Hosea, mke huyu aliyekusidiwa kuwa furaha yake, amekuwa chanzo cha mateso ya uchungu wake. (Hos. 2: 4-9) mke huyu hana uaminifu naye huenda kwa wanaume wengine. Amina!!


NAWATAKIENI WOTEEE JUMAPILI HII IWE NJEMA NA PIA BARAKA ZA MUNGU ZITAWALE NYUMBANI MWAKO/MWENU NA POPOTE PALE U/MTAKAPOKUWA.!!!!

Friday, February 11, 2011

BREAKING NEWS: LITTLE MAKULILO AZALIWA


On February 10th, 2011 at 5:42pm, Pacific Time, Marie Makulilo has delivered our cute little Makulilo named BENEDIKT FULBRIGHT MAKULILO. Benedikt has 8.8lbs (weight) and 21 inches (length)

The logic behind the names (Benedikt Fulbright Makulilo)
The name Benedikt (with letter "K" instead of "C" because of Kiswahili and Germany spelling of Benedikt), which comes from the Latin word meaning "the blessed", in honour of both Saint Bendict of Nursia and Pope Benedict XVI. And the name Fulbright is in honour of the prestigious FULBRIGHT scholarship. Fulbright Scholarship is the scholarship which has been named after William James Fulbright, and it has lot of meaning in realizing my dreams today, and MAKULILO is the honor of unsung hero Boniface Makulilo, my father

Thank you all for your prayers and encouragement.

The Makulilos (Marie, Ernest and Benedikt)

Blog www.makulilo.blogspot.com
www.scholarshipnetwork.ning.com

Thursday, February 10, 2011

UNAJUA HAPA NI WAPI?? AU NI JENGO KWA AJILI YA NINI /GANI?


Ni sehemu nzuri sana, ukifika hapa utatamani usiondoke......



Wednesday, February 9, 2011

BABA NA MAMA, NI NANI AMBAYE HAKUCHEZA MCHEZO HUU?

Katika ukuaji wetu, naamini wengi wetu tumeshiriki michezo mingi ya utotoni.
Mingi ya michezo tulioshiriki ni huu wa baba na mama ambao kule kwetu Songea tumezoea kuuita Madangi.

Mchezo huu wa baba na mama huchezwa na watoto kwa kuwaiga wazazi wafanyavyo kwa kuigiza mambo ya mapishi na mambo ya mapenzi ya kitoto.

Mchezo wa Mapenzi ya kitoto ndio ambao ningependa kuuzungumzia leo. Naamini karibu wote sisi, hakuna ambaye hajapitia mchezo huu. Inasemekana watu saba kati ya kumi miongoni mwetu, hakuna asiyefahamu mchezo huo.

Hata hivyo takwimu zisizo rasmi zinaonyesha kwamba watoto wa kiume ndio wanaoshiriki zaidi mchezo huu wa mapenzi ya utotoni kwa asilimia 85, ukilinganisha na watoto wa kike ambao wao hushiriki kwa kiwango cha asilimia 75.

Mchezo huu kiukweli hauna madhara yoyote kwa kuwa washiriki wote ni watoto, isipokuwa, adhabu na kauli zinazotolewa na wazazi hugeuka sumu.
Hebu fikiria watoto wanafumaniwa na mzazi wakicheza mchezo huu wa mapenzi ya kitoto, mzazi huyo anatoa adhabu ya viboko kwa watoto hao kisha kuwaita watoto hao kuwa ni wajinga na shetani wakubwa kwa kufanya jambo hilo ambalo wakati huo litabatizwa jina la mchezo mchafu na usiofaa kabisa, na mara nyingi kauli hizi kuelekezwa kwa mtoto wa kike, lakini mtoto wa kiume huachwa tu kwani kwa wazazi wengine huonekana ni shujaa.

Mara nyingi kile tulichoambiwa utotoni ndivyo tunavyokichukulia hata ukubwani, kwa hiyo zile adhabu za kuchapwa bakora na kuambiwa kuwa huo ni mchezo mchafu na wa kishetani, hubaki akilini mwetu hata leo na ndio maana tendo la ndoa miongoni mwetu hasa wanawake linabeba taswira ya kitu cha aibu na kisichofaa. Hii inatokana na zile kauli tulizoambiwa utotoni kuwa mchezo huo ni mbaya na wa kishetani.

Wanawake ndio wahanga wa kauli hizi na ndio maana hata wale walioko kwenye ndoa wanakosa uhuru wa kujieleza kwa wenzi wao kutoridhishwa na tendo la ndoa inakuwa ni vigumu. Atawezaje kujieleza wakati alimbiwa kuwa huo ni mchezo mchafu na wa kishetani usiofaa hata chembe kufanywa na mwanaadamu?

Unaweza kukuta mwanamke ameolewa lakini hawezi kuwa huru kumueleza mwenzi wake hisia zake za kimapenzi kwa sababu ya kauli hizi kukaa kichwani na kuhisi aibu.

Kwa hiyo kwa kutumia sauti za wazazi wetu au walezi wetu na sauti ya jamii tunalitazama tendo la ndoa kama uchafu ili hali tunalihitaji na ni muhimu ili tuendelee kuwepo.

Monday, February 7, 2011

MAONI YA PROFESA MBELE KATIKA MADA YA KAZI YA UALIMU: TAALUMA MUHIMU ILIYODHARAULIWA

Maoni haya yalitolewa na profesa Mbele tareha 3/2-2011 kwanye mada hii hapa.
Hapa ni mwenyewe profesa J.Mbele
Na hivi ndivyo alivyosema;-
Mimi ni mwalimu, na nilikuwa na wito wa kuwa mwalimu tangu nilipokuwa mdogo, sijaanza hata shule. Kila siku najitambua kuwa niliitwa na Muumba kuwa mwalimu, na sijawahi kutetereka hata siku moja, pamoja na magumu yake.

Nitatoa mifano miwili ya magumu hayo. Nilianza ualimu katika chuo kikuu cha Dar es Salaam, mwaka 1976, baada ya kuhitimu shahada ya kwanza. Baina ya mwaka 1980-86 nilikuja Marekani kusomea shahada ya uzamifu.

Nilifanya juhudi masomoni, hadi kupata tuzo ya mwanafunzi bora, nikanunua vitabu vingi sana, kwa kuelewa kuwa ndio nyenzo nitakayohitaji wakati wa kurejea tena Chuo Kikuu Dar kuendelea kufundisha.

Nilirejea nchini ule mwaka 1986 na shehena kubwa ya vitabu. Wa-Tanzania waliniuliza kama nimeleta gari ("pick-up"). Kwa vile sikuwa nimeleta gari, bali hivyo vitabu, waliniona nimechemsha.

Hii ndio hali halisi, ambayo kwangu ni ngumu. Kwa mtazamo wangu, mwalimu si mtu anayefundisha darasani tu, bali anatakiwa kuwa mfano kimaisha. Nami nilijaribu kuonyesha mfano wa kuthamini elimu.

Kinachonitatiza akilini ni kujiona ninajaribu kuwafundisha watu ambao akili zao ziko kwenye magari, na hapo darasani wanatafuta vyeti tu waende zao kusaka mali. Si kwamba wanathamini elimu kama elimu. Hawanioni mimi mwalimu kama mtu ninayewapa mfano wa kutambua nini kitu muhimu maishani, yaani elimu.

Suala la kuwasukuma wa-Tanzania watambue umuhimu wa elimu lina usumbufu na kero nyingi, kama alivyoelezea Profesa Matondo hapa.

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII YAPATA MKURUGENZI MPYA WA IDARA YA UTALII


Na Tulizo Kilaga wa Wizara ya Maliasili na Utalii
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii amemteua Bw. Ibarahim Mussa kuwa
kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Utalii kuanzia tarehe 01 February 2011.

Uteuzi huo ameufanya kwa mujibu wa kifungu cha 6 (1) (b) cha Sheria ya
Utumishi wa Umma Na. 8 ya mwaka 2002.

Ibrahim A. Mussa (53) ni mtumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii tangu
mwaka 1982 hadi sasa ambapo alifanya kazi katika ngazi mbalimbali, katika
Idara ya Misitu na Idara ya Utalii.

Kabla ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Utalii, Ibrahim A. Mussa alikuwa
Mkurugenzi Msaidizi anaesimamia Utafiti, Takwimu na Mafunzo katika Idara
ya Utalii.

Bw. Mussa ana Shahada ya Uzamili (International Tourism Management)
aliyoipata mwaka 2005 kutoka chuo cha Sheffield nchini Uingereza

Bw. Mussa anachukua nafasi ya Mkurugenzi wa Idara ya Utalii kutoka kwa Bi.
Maria Mmari ambaye amepangiwa kazi nyingine.

Sunday, February 6, 2011

JUMAPILI NJEMA KWA WOTE:-Ni Jumapili ya sita ya mwaka halafu ni tarehe sita pia, na ya kwanza kwa mwezi huu

Napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunilinda mwezi uliopita Januari nimekuwa salama bila kuugua na namshukuru kwa kuuanza mwezi huu wa februari vizuri. Pia namshukuru kwa kuwalinda watu wengine wote waliosalama mpaka siku hii ya leo. Ahsante Mungu. JUMAPILI NJEMA KWA WOTE.!!!!!!!!

Ngoja tumsikilize dada Rose Muhando kidogo pia......

Friday, February 4, 2011

Thursday, February 3, 2011

KAZI YA UALIMU: TAALUMA MUHIMU ILIYODHARAULIWA

Mwalimu akiwa darasani anafundisha!!

Katika maisha yangu nimeishi na walimu sana . Kwa hiyo nimekuwa nikijiuliza miaka yote hii mingi. Na nimekuwa nikipatwa na uchungu sana nionapo watu/serikali jinsi inavyoiona kazi ya Ualimu kama isiyo na maana. Kila nikijaribu kufikiri, kazi zote hapa duniani naona hakuna kazi ngumu kama UALIMU.
Fikiria mtoto aanzapo shule hajui kuandika, kusoma wala kutamka a, e, i, o, u. Lakini mwalimu anahenya kwa kila njia na baada ya muda mtoto anaweza kusoma kuandika kutamka silabi zote bila shida kama mtoto si mgumu kuelewa. Na hii sio walimu wa shule ya msingi tu ni kuanzia chekea (vidudu) kule ndio kuna kazi kubwa zaidi.

Kwa nini walimu wanadharauliwa na pia mishahara yao ni midogo sana. Kwa kweli inatia huruma. Mshahara wa kima cha chini Tanzania hivi sasa ni laki moja kwa kweli hii ni halali/uungwana?

Ni juzi tu nimesikia ya kwamba idadi ya wanaoomba kusoma ualimu hapa sweden inapungua kwa kiwango kikubwa sana. Sijui huko tuendako kutakuwa na walimu. Na pia kuna kupunguzwa walimu katika kila shule watapunguzwa walimu 14. Sasa mbaya zaidi wanawapunguza walimu vijana na wazee wanaendelea kufundisha .

Awali nilidhani matatizo ya Waalimu labda ni kwa nchi za Africa pekee, lakini nilipokuja hapa nchini Sweden, ndio nikajua kuwa hata hapa matatiozo ni yale yale, yaani yanafanana kwa kiasi kikubwa sana. Kwa hapa Sweden walimu wanateseka sana na pia hawaheshimiwi kabisa. Wanafunzi wana dharau sana wanawaona waalimu kama ni watani wao, wanajibizana nao, na wakijaribu kuwaelimisha jambo ni wabishi ajabu, na kuwaadhibu kwa viboko hapa nchini Sweden ni makosa. Hapa hakuna viboko kabisa kwa hiyo kiboko ni maneno tu. Tena maneno yaenyewe inabidi yawe mazuri na ya unyenyekevu. Na kama Mwalimu akijaribu tu kupandisha sauti kumkaripia mtoto anaweza akachukuliwa hatua kali za kinidhamu na anaweza hata kupoteza kazi yake.

Kuhusu swala la mshahara:- Kima cha chini cha mshahara wa mwalimu hapa nchini Sweden ni 3,600,000TSh, kwa pesa ya hapa ni 20,000SEK. Kiasi hicho cha mshahara kwa huko nyumbani Tanzania unaweza kuona ni kiasi kikubwa sana, lakini ukilinganisha na maisha ya hapa ni pesa ndogo sana na usipokuwa makini unaweza kushindwa kumudu baadhi ya ghrama za maisha. Hebu angalia mchanganuo wa makato ya huo mshahara pamoja na matumizi ya lazima, kodi kwa ujumla anahitaji kulipa 1,200,000TSH. Baada ya hapo zinabaki 2,400,000TSH. Chakula, bili n.k ni kama 10,000SEK = 1,800,000TSH. Baada ya hapo zinazobaki kabisa ni kama 600,000TSH. Kwa kiwango cha gharama za maisha ya hapa Sweden, bado pesa hiyo ni ndogo sana.

Kwa kweli waalimu wanayo kazi kubwa, lakini mapato madogo wakati kazi ya ualimu ni nzito na ndio mwanzo wa watu kujua kusoma na kuandika. Bado najiuliza, hivi kwa nini waalimu wanadharauliwa kwa kazi hii ngumu ya kuelimisha.?

Tuesday, February 1, 2011

KWA NINI WANAUME/AKINA BABA WENGI WANAFIKIRI WAO NDIO WAAMUZI/WAFALME WA NYUMBA?

Suala hili limekuwa likinikera sana akilini mwangu kwa miaka mingi. Ya kwamba akina baba/wanaume wao wanafikiri kazi yao kubwa katika nyumba ni kuwa MUME/BABA basi. Mara nyingi utasikia wanasema mimi ndio mkubwa wa nyumba. Na kama wanafanya kazi za ofisini basi ndo itakuwa kero mno. Kwani hapa atataka anaporudi toka kazini akute chakula mezani, maji ya kuoga bafuni tena ya moto, nguo zmepigwa pasi n.k. Na kinyume kama hana kazi basi atakuwa anashinda kilabuni(UGIMBI) na akirudi toka huko basi ni kelele tu, hakuna amani wala maelewano

Bado naendelea, kuna wengine wanaona kupika, kulea watoto, kutafuta chakula ni kazi ya wanawake. Yaani hawawezi hata kujipikia chai kwa vile wao ni wanaume au hata kumbadili mtoto nepi, Mtoto amabaye ni wake. Kikubwa wanachofanya ni kukaa kitini/sofani na kuletewa kile wanachotaka. Wanasahau kabisha jambo la USAWA.

Bado wanaishi dunia ya mababu, mababu na mababuzi. Tuache UBINAFSI tuishi kwa kushirikiana/kusaidiana kwani wote ni SAWA. Nasema tena tuishi kwa kusaidiana hapo wote tutafurahia maisha. Tuache mambo ya UTUMWA