Monday, November 30, 2009

NYIMBO ZA MCHAKAMCHAKA/KUMBUKUMBU

Leo nimekumbuka wakati nasoma shule hasa shule ya msingi saa kumi na moja alfajiri kuwahi shule kisa nini? Kuwahi namba na kukimbia mchakamchaka huku mnatweta kama nini na mkiimba nyimbo:- Kwa mfano:-
1. Panda mlima panda, panda, panda, pasnda usichoke........x2
2. Iddi amin akifa mimi siwezi kulia nitamtupa kagera awe chakula cha mamba.x2
3.Jua lille literemke mama, mwezi nao uteremke mama haiyahiyaaa hiyaa hiyaa mamaaaa.....x2
4. Alisema, alisema, alisemaaa Nyerere alisema vijana wangu wote mwalegea shart tuanze mchakamchakax2.....

Kama kun mtu anakumbuka wimbo mwingine basi karibu kuongezea hapa.

Sunday, November 29, 2009

JE? UNANIKARIBISHA NYUMBANI MWAKO!!!!!!! PIA LEO NI JUMAPILI/DOMINIKA YA KWANZA YA MAJILIO YA MWAKA C



Naondoka nyumbani kwa Yasinta sasa na nimeacha baraka, je? unanikaribisha kwako? Nipokee kwa upendo na unitume kwa wengine/nyumba nyingine ili niweze kuwabariki wao pia. Uwe na siku yenye baraka. Nipo mlangoni, nabisha hodi. Kama kuna mtu ananisikia na afungue mlango. Nitaingia ndani na kula nao/nanyi katika meza yenu/yao. Sasa anaenda nyumbani kwako mwache yeye akubariki na umwonyeshe nyumbanyingine. MUNGU NI MKUBWA!!!!!!!JUMAPILI NJEMA KWA WOTE!!!

Friday, November 27, 2009

TAFAKARI YA LEO KWENU AU KWA PAMOJA!!!!


Wanaume wawili wamekaa na wanavua samaki.Na huku wakiwa na filosofia jinsi wanaume wanywavyo bia/pombe. Baada ya kukaa kwa masaa kadhaa John anamwambia Thomas:
"Mimi nadhani nataka kumwacha mke wangu. Mke wangu hajaongea nami kwa muda wa miezi miwili sasa"
Thomas amekaa kimya kwa muda huku akinywa bia yake kabla hajamjibu john:- Na baadaye akamjibu:- "Mimi ninakushauri jaribu kufikiri kwa makini zaidi. Wanawake wa aina hii ni ngumu sana kuwapata.!!!!!!!

Thursday, November 26, 2009

NAPENDA KUMPONGEZA MDOGO WANGU PEKEE, KWA KUTIMIZA MIAKA LEO... HONGERA SANA MDOGO WANGU!!


Ni mdogo wangu wa mwisho.
Leo ni siku maalum na ya pekee kwa mdogo wangu. Ilikuwa si muda mrefu nilikubeba na ukanikojolea mkojo mgongoni. Kweli sasa naamini miaka inazidi kwenda tena inakimbia kwa haraka sana. Sisi wote hapa nyumbani tunapenda kukupa HONGERA sana kwa kutimiza miaka. Na tunakuombea uwe na maisha mazuri, pia nakuombea kwa sala hii, Mungu akubariki, akuongoze, akufariji na akusaidie katika mambo yako. HONGERA SANA MDOGO WANGU MPENDWA KWA KUTIMIZA MIAKA . HONGERA MAMA MDOGO, SHEMEJI , RAFIKI NK. NAAMINI UNA WAKATI MZURI!!!!!

Wednesday, November 25, 2009

Hata miguu nayo hupendezeshwa!!!! Swali je ni vibaya?

Vikuku ni urembo au?
KUNA mtu kanitumia hiyo picha anauliza hizo shanga za miguuni zinavaliwa kujiremba au zina maana nyingine?
Kwa mujibu wa maelezo yake, amewahi kusikia kwamba, shanga hizo a.k.a vikuku zina maana yake hivyo anaomba kufahamu kama ni kweli.
Anasema, kaelezwa kwamba, kikuku kikivaliwa mguu wa kulia ina maana yake, na kikivaliwa kushoto kinakuwa na maana nyingine, ni kweli?
Kama kila mguu una maana yake, vikivaliwa miguu yote inamaanisha nini?

Tuesday, November 24, 2009

HONGERA KWA SIKU YAKO YA KUZALIWA DADA MARIAM!!!

Nina hakika siku yako ya kuzaliwa ulikuwa na muda mzuri na pia ulipata chakula kizuri. Mwenyezi Mungu akujalie maisha marefu hadi uwaone wajukuu wangu. HONGERA SANA DADA KWA SIKU HII MUHIMU KUONGEZA KAMWAKA AU SIJUI GUMWAKA:-)

Monday, November 23, 2009

ZILIKUWA NI SIKU KUMI ZA KUSIKITISHA KWA MWENETU!!!!

Kwako dada Yasinta, mimi ni msomaji wa blog yako kwa muda mrefu sasa.Kwa kuwa Blog yako inahusiana na mambo ya maisha kwa ujumla nami nina mkasa ambao nimeona nikutumie ili wasomaji wa blog hii nao wajue madhila niliyoyapata mimi na familia yangu.

Katika juhudi zetu za kutafuta mkwanja (Fedha) mimi na mume wangu tukakubaliana tutafute house girl ili atusaidia kukaa na mtoto wetu ikiwa ni pamoja na kufanya shughuli nyingine za usafi kwa ujumla pale nyumbani.

Baada ya kuhangaika sana, maana siku hizi ma house girl wamekuwa adimu sana hapa jijini Dar es salaam, kutokana na juhudi za serikali yetu kuhakikisha kuwa kila mtoto anapata elimu.Tofauti na zamani ambapo ilikuwa kila mwisho wa mwaka watoto hasa wa kike wanaomaliza darasa la saba wanaletwa mjini kutafutiwa kazi za ndani, siku hizi mambo ni tofauti sana, kila mzazi anajua umuhimu wa elimu na kwa kuwa inapatikana kwa urahisi, japo haijakuwa ya kiwango kinachoridhisha, kutokana na serikali kujenga shule nyingi za kata lakini zikiwa haziendi sambamba na kuongeza walimu wa kutosha katika shule hizo, idadi ya watoto wanaoletwa mjini kufanya kazi za ndani imezidi kupungua siku hadi siku.

Hata hivyo, juhudi zetu zilizaa matunda, tulimpata binti ambaye na yeye pia anaye mtoto wa kike makamo ya mwenetu Brian, aliyezalishwa na kutelekezwa huko kijijini kwao Handeni Tanga, alikuja huku mjini kuishi na dada yake binamu lakini inaonekana hakupokelewa vizuri, hivyo ikamlazimu atafute kazi, ambapo aliletwa kwetu.

Alituomba tumpatie nauli ili amrudishe mwanae nyumbani akakae na mama yake ili aweze kufanya kazi kwa ufanisi, tuliafiki, lakini baadae tukaona ni vyema akiishi na sisi pamoja na mwanae kwa kuwa mwenetu alishaanza kuzoeana na hako ka binti ikabidi turidhie abaki na mwanae kama vile kampani kwa mwenetu.

Tulimwambia wazi kuwa pamoja na kumlipa mshahara lakini ataishi na sisi kama ndugu kwa maana akiwa na shida yoyote ile aseme tutamsaidia nje ya mshahara. Alionekana kuwa mpole sana na mwenye nidhamu na wote tulimpenda sana.

Tulikuwa tunampenda yeye na mwanae na tulikuwa tunamuhudumia mwanae sawa na mwenetu, bila ya ubaguzi na tuliamua kumpa pesa akafanye shopping ya nguo zake na mwanae. Lakini kukawa na hali ya uchafu pale nyumbani, na watoto wakawa hawaogeshwi na kama ni kuogeshwa inakuwa ni kuwaloweka tu kwenye maji na hata nguo nazo zikifuliwa hazitakati. Tulijadiliana na mume wangu tukaona labda ni kutokana na kutingwa na kulea watoto, kwani watoto wote walikuwa ni watundu, mwenetu ni mtundu na mwanae pia ni mtundu.

Tuliona ni vyema amrudishe mwanae huko kwao Handeni ili asiwe na majukumu mengi.Tuliandaa nauli na kumweleza kuwa siku mbili zijazo atasafiri kwenda kwao kumpeleka mtoto.
Aliaga kumpeleka mtoto wake akasukwe huko kwa dada yake na tulimruhusu, lakini hapo ndipo tulipokuja kugundua mengi tusiyoyajua.

Hakurudi siku ile na siku iliyofuata tuliamua kufanya usafi wenyewe, dada Yasinta, tulikutana na vitu vya ajabu chini ya kitanda, ambao haufai kuelezea humu. Tulikuta vidonge vya majira pamoja makorokoro mengine ambayo yalikuwa yanatia kinyaa.

Tulishikwa na kinyaa, lakini ni nyumba yetu tutaacha huo uchafu? Ikabidi tusafishe chumba mpaka kikawa kusafi pamoja na kufua nguo zote pale nyumbani ikiwa ni pamoja na za kwake na za mtoto wake.

Tulipozungumza na jirani yetu mmoja ili kujua hali halisi ya pale nyumbani maana sisi wote ni wajasiriamali na hatushindi nyumbani. Kwa kusita sita sana ndio akatueleza. Kumbe kila tukiondoka nyumbani yule binti na yeye anatoka zake kwenda kwa mabwana zake na kurudi mchana lakini anakuwa kambebea mwanae chipsi, na mwenetu Brian anashinda na njaa kwa kuwa hawezi kula chipsi kavu, inatokea watoto wa jirani yetu humpa chakula na kila akiulizwa anasema kuwa eti hatujaacha pesa za matumizi, wakati tulikuwa tunampa pesa za kutosha.

Alikuwa kila siku ananunua nguo mpya na pesa zetu, na kibaya zaidi ilikuwa Brian akilia njaa anamtukama matusi makubwa kama mtu mzima….eti anamwambia ku*****la mama yako msenge wewe sasa unalia nini…….kamlilie mama yako huko…..Hivi hayo matusi anastahili mtoto kama Brian ambaye ndio atatimiza miaka miwili mwezi ujao?

Tulisimuliwa vituko vyake vingi sana mpaka nililia kwa uchungu. Ilipofika usiku ndio akarudi, mume wangu hakuwa na maneno mengi alimlipa mshahara wake wa siku kumi alizoishi na sisi na akamwamuru arudi alipotoka usiku ule ule. Aliacha nguo zake mpaka leo hajaja kuzichukua, lakini kuna siku alikuja mahali ninapofanyia biashara zangu kunisalimia na kuniomba radhi. Alikiri kufanya hayo niliyosimuliwa na aliomba tumpe nafasi nyingine, ila mume wangu amekataa katakata kumpokea tena. Ila nilipomchunguza alionekana kuwa na hali mbaya sana na alinilalamikia kuwa hajala huko kwa dada yake, na hata mtoto wake naye anaonekana afya yake imedorora sana kutokana na kutopata chakula.

Nilishikwa na huruma na nilimpa fedha kidogo ili akamnunulie mtoto chakula.Hivi sasa anatangatanga mtaani na nadhani ashaanza kufanya umalaya kwani kuna siku nilikutana naye majira ya usiku nikitoka kwenye biashara zangu, hizo nguo alizovaa, zinatia aibu, yaani dada Yasinta alikuwa amevaa kinguo kifupii na kiblauzi kilichoacha mgongo na sehemu ya kitovu nje, nilimsimamisha na kumuuliza anakoelekea usiku ule, kwa aibu sana aliniambia kuwa anakwenda kwa rafiki yake.Sikusema kitu nilimuacha aendelee na safari zake na mimi nikajirudia zangu nyumbani kwangu, yaani dada, niliogopa, kumbe nilikuwa naishi na fuska ndani ya nyumba bila kujua. Kusema kweli dada nilibaki na maswali mengi sana ambayo sikuweza kupata majibu yake.

Hivi mtu kama huyo anaweza kusingizia kuwa anafanya umalaya kwa kuwa hana fedha au ni kutafuta fedha kwa njia ya mkato? Je hakuna shughuli yoyote ambayo angeweza kufanya zaidi ya umalaya? Je akipata ukimwi, ni nini hatima ya mwanaye?

Sasa sijui tulifanya ukatili kumfukuza au alistahili……..naomba ushauri wako……..

Sunday, November 22, 2009

AHSANTE MUNGU WANGU!!!!!

Dear GOD:
I want to thank You for what you have already done.
I am not going to wait until I see results or receive rewards.
I am not going to wait until I feel better or things look better.
I'm not going to wait until people say they are sorry or until they stop talking about me.
I am not going to wait until the pain in my body disappears.
I am not going to wait until my financial situation improves.
I am not going to wait until the children are asleep and the house is quiet.
I am not going to wait until I get promoted at work or until I get the job.
I am not going to wait until I understand every experience in my life that has caused me pain or grief.
I am not going to wait until the journey gets easier or the challenges are removed.
I am thanking you right now. I am thanking you because I am alive. I am thanking you because I made it through the days of difficulties. I am thanking you because I have walked around the obstacles.
I am thanking you because I have the ability and the opportunity to do more and do better.

I'm thanking you because FATHER, YOU haven't given up on me.
Have a great day, and an even better tomorrow.

Hii nilitumiwa na rafiki mwema nimeipenda na nimeona si mbaya kama nikiweka hapa kibarazani ili tuombe kwa pamoja. Amina. JUMAPILI NJEMA KWA WOTE !!!!!!!!!!

Friday, November 20, 2009

SIJUI HUYU DADA NI NANI KAMA NAMFAHAMU VILE?


Hakika kuna sehemu nimemwona lakini sikumbuki ni wapi tena nimewahi kula naye ugali na matembele. Labada wenzangu mtanisaidia.

Wednesday, November 18, 2009

+RAFIKI YANGU MPENDWA AGNESTA MAPUNDA+

Kutokana na sheria au sijui niseme mipango ya Tanzania kuwahamisha/shwa walimu:- Nakumbuka ilikuwa mwaka 1985 baba alipata uhamisho kutoka Lundo s/m kwenda kijiji kimoja chenye shule iitwayo Kingoli. Nilikuwa darasa la tano. Nilipofika pale shuleni nilikutana na wanafunzi wengi, lakini Agnesta alinipokea kwa namna yake.
Tulianza urafiki wetu, uarafiki ambao tulikuwa wakati wa jumamosi au jumapili tukitembeleana majumbani. Yaani, tulikuwa tukitembeleana, huku tunachuklua zawadi(ndundu) unga kwenye jamanda na kuku. Na ukifika kwake unachinjiwa kuku pia.

Nliachana mwaka 1988 na rafiki yangu Agnesta. Mwaka 2007 nilikuwa nyumbani TZ. Siku moja nilikuwa mjini – Songea, katika pitapita ghafla mtu akanishika bega na kunisalimia dada Yasinta shikamoo! Nikashtuka na kugeuka alikuwa mdogo wake Agnesta. Nikasema moyoni AHSANTE Mungu. Kwa kufurahi kupata habari za rafiki yangu Agnesta. . Lakini habari nilizozipata hazikuwa nzuri Agnesta rafiki yangu alikuwa hayupo tena nami alishafariki muda mrefu labda miaka mitatu iliyopita. Sikuamini masikio yangu, nilisikitika sana , kwani alikuwa rafiki yangu mpendwa. Na leo naona amenishukia nkwani nimemkumbuka sana ndio maana kisa cha kuandika hapa. Mwenyezi Mungu Aiweke Roho yako PEPONI AMINA..

Tuesday, November 17, 2009

NGOJA LEO TUMSIKILIZE MTAKATIFU SIMON KITURURU NA WIMBO WAKE NAMPENDA



Sikujua kama kaka Simon ni mtungaji pia wa nyimbo. Siku njema kwa wote na wimbo huu au ngoja tumsikilize na huu wimbo akiwa akimsifia Hukwe Zawose karibuni:-


Monday, November 16, 2009

Mapenzi bila Mawasiliano ni kujidanganya

Inatosha mwanamume kumpa mkewe fedha na kila kitu bila kuzungumza naye na kusikiliza hisia zake? Inatosha mwananke kumpa mapenzi ya kila aina mumewe wawapo chumbani bila kusema hisia zake kwake na kuwa tayari kufunga njia za kujadili mambo yanayowahusu? Hebu soma mfano huo hapo chini kwani kuna uvumbuzi wa ni kwa nini tunaweza kuwa na kila kitu kimapato au kisura na kimaumbile, lakini wapenzi wetu wakatuacha.
Johnson amerudi nyumbani kutoka kwenya shughuli zake na kama kawaida yake, salaam yake ya kwanza kwa mkewe ni kuuliza, “Mbona viatu vimewekwa njiani.” Pengine siyo salaam tu, bali hilo litabaki kuwa tamshi au kauli pekee kwa muda mrefu ujao wa jioni ile. Baada ya hapo Johnson huingia chumbani ambako hukaa sana hadi chakula kinapoiva. Mkewe anajaribu kumuuliza jinsi kazi ilivyokuwa kwa siku ile. Johnson, baada ya kujivuta sana anajibu kwa kifupi, “safi tu”.

Mkewe anajaribu tena kutafuta njia ya kuwasiliana na mumewe. Anajaribu kumsimulia jinsi gari moja la mchanga lilivyotaka kumuuwa utingo wake hapo mtaani mchana ule. Johnson anasikiliza habari hiyo bila kuonyesha hali yoyote ya mabadiliko na wala hajibu wala angalau kusema,. “Hawa utingo nao wana hatari.” Haoni, hana sababu ya kujibu. Lakini bado anaamini na anadai kwamba huyo ni mkewe, tena wakati mwingine akisema ni mkewe mpendwa. Wengi wetu ni kama Johnson au tuna wanaume kama yeye.
Tunaweza kuwa na kila kitu kwa upande wetu. Mali, umaarufu mkubwa, kazi nzuri, watoto wazuri na vingine, lakini tukakosa hisia kwa wapenzi wetu. Tukakosa kuwa na uwezo wa kubaini haja ya kujali kuhusu hisia za tuwapendao au tunaodai kuwa tunawapenda. Kukosa uwezo wa kubaini hisia ni kushindwa kwetu kufungua njia na mawasiliano kwa wenzetu hao.
Mawasiliano katika ndoa ni nini? Inaweza ikaonekana kama vile swali hili ni rahisi kupatiwa jibu, lakini kwa kweli ni wanandoa wachache sana wanaoweza kutoa jibu sahihi la swali hili. Mawasiliano kwa wengi ni kuzungumza au kijibizana. Huenda hiyo ni kweli, lakini hata wanaogombana huzungumza na kujibizana pia. Mawasilino katika uhusiano kwa kifupi, lakini kwa ufasaha, yana maana ya wanandoa kuzungumza kila mmoja kwa uhuru na kwa uadilifu. Wanandoa au watu wengine wowote wanapowasiliana vizuri, huzungumza juu ya matatizo yao, furaha, huzuni na kile kinachoenda kwenye akili au mawazo ya kila mmoja-huzungumza hisia zao.
Huwa tunasema na kushauri kuhusu mawasiliano mazuri ndani ya ndoa. Huwa tunasisitiza sana kuhusu wapenzi kuwa makini wanapojaribu kusema au kuwasilisha hisia zao kwa wenzao. Lakini huenda ugumu uko kwenye kufahamu maana ya mawasiliano ndani ya ndoa, achilia mali mawasiliano mazuri.
Lakini bila shaka kutokana na fasili hiyo fupi, tunaweza kuwa na picha angalau ndogo kuhusu maana ya mawasiliano katika ndoa. Mawasiliano mazuri ina maana vitendo fulani ambavyo vikifanyika katika utaratibu fulani, ndoa kukomaa na kushika mizizi kwa kiwango cha juu sana cha uimara, na ambayo yasipofanyika, uwezekano ni kwa ndoa husika kuanguka.
Pengine mtu anaweza kuuliza, inakuwaje watu ambao tulikutana tukiwa hatujuani, tukavutiana kwa sababu mbalimbali hadi tukafikia uamuzi kwa furaha kwamba tunaweza kuishi pamoja, leo hii tushindwe kuzungumza kwa uhuru na uadilifu? Kwa nini wanandoa hushindwa kuwasiliana? Kuna sababu nyingi, lakini inayokusanya zote ni moja-wengi hatujui umuhimu wa mawasiliano na pengine hatuoni kuwasiliana kama sehemu muhimu kwenye maisha yetu ya kindoa.
Kuna wakati tunadhani kimakosa, kwamba kuwasiliana kunaweza kutuharibia uhusiano wetu badala ya kujenga. Kwa hiyo, tunaamua kuzifutika hisia zetu, mawazo yetu na ushauri wetu vifuani mwetu. Mtu amepatikana na tatizo, anadhani akimwambia mwenzake atamvunja nguvu, atamtisha au atamfanya amlaumu au kumuona hana maana. Hivyo, anaamua kunyamaza. Inapokuja kufahamika, mwenzake hudhani alimficha kwa kutomjali, kutomwamini au kutompenda. Badala ya kutatua tatizo, hali hiyo inakuwa imezua tatizo jipya.
Lakini kuna ukweli ambao sisi kama binadamu, kila mmoja wetu ni lazima aukubali. Ukweli huu ni ule kwamba, ndani kabisa ya mioyo yetu huwa tunatamani kuzungumzia hisia zetu. Tungependa sana bila shaka kuonyesha undani wetu, yaani hisia zetu kwa wengine. Siyo jambo la nasibu tu kwamba wengi wetu tunajikuta tunataka au tuna rafiki wa karibu angalau mmoja kwenye maisha yetu. Hii ni kwa sababu tunataka mahali pa kuonyesha nafsi zetu halisi, yaani kusema tunavyohisi. Tungependa kuwa atatudharau au kutuona tuna mapungufu. Badala yake atashiriki nasi katika hisia hizo, ziwe mbaya au nzuri, za kutisha au kufurahisha na za aibu au za sifa.
Lakini siyo kwa sababu ya sisi kusikilizwa na kueleweka u , lakini pia tungependa kuwasikiliza wale ambao nao wanatusikiliza. Kusikia hisia zao za ndani na ukweli unaoenda kwenye mawazo au hisia zao. Ukiangalia sana kutokana na ukweli huo, utaona kwamba, moja ya sababu ya kuoa au kuolewa ni kuwasiliana. Sasa kama hadhi ya chini sana, ni kama vile hiyo ndoa haipo kabisa. Bila mawasiliano, ndoa inakuwa ni sawa na muungano wa watu wawili wanaoishi chini ya paa siyo watu wawili wanopendana.
Hebu tujiulize. Unawezaje kusema au kupima kwamba ndoa fulani haina mawasiliano? Suala hili linaonekana kama vile liko wazi sana, lakini kamwe siyo hivyo. Watu wengi kwenye ndoa wanakabiliwa na migogoro na kutoelewana kwingi, lakini kamwe hakuna ajuaye kati yao kwamba tatizo ni kukosa mawasiliano. Kukosa mawasilino kunaweza kuzaa hali ambayo ndiyo inayoonekana kuwa ndicho chanzo cha tatizo ndani ya ndoa, kukosa mawasiliano kwenyewe kukiwa kumejificha au kukiwa wazi, lakini kwa sababu hatujali kuwepo au kutokuwepo kwake tukashindwa kuona.
Wakati mwingine ni kweli kwamba tatizo lililopo siyo kukosa mawasiliano, lakini kwa sababu hakuna mawasiliano, tatizo hilo huwa kubwa na pengine kuzaa matatizo mengine ambayo hatimaye huwa magumu kusuluhishwa. Matatizo ambayo yangesuluhishwa hufikia mahali yakaiangusha ndoa sababu yamekosa kusemwa na kutafutiwa ufumbuzi. Yatasemwa wapi na saa ngapi, wakati hakuna mawasiliano.

Makala hii nimeichukua kutoka kwenye kitabu cha Maisha na Mafanikio kilichoandikwa na Hayati Munga Tehenan ambaye alikuwa ni Mwalimu mzuri wa maarifa ya Utambuzi akitoa elimu hiyo kupitia magazeti yake ya Jitambue, vitabu na semina zake nchini Tanzania kabla ya kufariki dunia.

Sunday, November 15, 2009

NI JUMAPILI/DOMINIKA YA 33 YA MWAKA B

Sala ya baba yetu
Basi nanyi salini hivi:-

KISWAHILI
Baba yetu uliye Mbinguni,
Jina lako litukuzwe,
Ufalme wako uje,
Mapenzi yako yatimizwe,hapa duniani kama huko Mbinguni.
Utupe leo riziki yetu,
Utusemehe deni zetu, kama sisi nasi tuwasamehevyo wadeni wetu.
Na usitutie majaribuni, lakini utuokoe na yule mwovu.
(Kwa kuwa ufalme ni wako, na nguvu, na utukufu, hata milele Amina)

Mt. 6, 9-13

DADI WITU

Hinu nyenye pemwisali, msala naha:-
CHINGINI/KINGONI
Dadi witu,
Witama kunani kulihundi,
Lihina laku lihyuwanike,
Ubambu waku utibwerele,
Chewifuna wenga vakiti vandu,
pamlima apa ngati chevikia kunani kulihundi,
Utiletele lelu chakulya chitu cha magono goha,
Utiwusile getihokili,
ngati tete tukuwawonela lipyana vevahoki kwa tete.
Ukotoka kutileka kulemala nichihaki,
nambu utiwusile vihaki.
(Ndava ubambu waveve na makakala na uvaha, magono gaha. Pepayi)
Mt. 6, 9-13.

DOMINIKA YABWINA KWA WOHA/JUMAPILI NJEMA KWA WOTE.!!!!!!!!!!

Saturday, November 14, 2009

HONGERA KWA SIKU YA KUZALIWA KAKA FADHY MTANGA!!

Leo ni siku maalumu kwa kaka, rafiki, mdogo, mtoto, ndugu , jamaa bila kusahau mtani Fadhy Mtanga. Katika upekuzi wangu nimegundua ya kwamba leo anatimiza miaka, kwa hiyo napenda kumpongeza kwa siku hii kwa kutimiza miaka. kukutumia ua litasinyaa, kadi itachakaa. Kwa hiyo nakuombea kwa sala hii Mungu akubariki, akuongoze, akufariji na akusaidie katika mambo yako. HONGERA SANA FADHILI MTANGA KWA KUTIMIZA MIAKA . HONGERA MTANI!!!

Thursday, November 12, 2009

TUSISAHAU LUGHA ZETU ZA ASILI/KINGONI:- MLYELELU = MLO/MILO

Mwenzenu leo nimetamni kweli kuongea kingoni hii ndio sababu nimeamua kuandika hapa:-

Mlyelelu
Mngoni ilya mara ppadatu kwa kuhwela, Kulawuka, muhi, kulalila. Vandu vangi vilya lukumbi lumonga tu kwa kuhwela. Lukumbi lungi lwa muhi ilya kwa kunonganonga vyakula videbevidebe ngita, liyawu, mbubudu, madonga, matevele, matoki, yembe matangamanga nk.

Kulawuka
Lukela pakuyimuka mungoni ilawuka. Pakulawuka ihopa wuji, lukumbi lungi ihopa wuji na kulyelela vimungulu au manyawu gatelekanu, au gayochanu, ama wuji na chimbwinya cha mayawu galovekanu au ga bundula. Ligono lingi ilawuka chimbala che vakuchipolosa huti. Kadeni vangoni valaukayi kilu, hinu ugali wa kulya kilu vikemela ngunguluku.

Ugali wa muhi

Ugali wa muhi vangi vilya lilanga pamuhana. Vandu vangi vilya he muhi, yitosha chevilawuka lukele. Vanu vangi vilya ugali lukela na kuhamba kumahengu mpaka chimihi nde pevilya ugali wa kulalila.

Ugali wa kulalila

Uwu nde ugali wa kuhambila kugana. Ndava ya mahengu ga muhi, lukumbi lwa kulya ugali wa kulalila nakumanyikana. Vangi vilya kwkona kulizwarara, vangi pakuyingila ngúku kugona, vangi kilu ya chitita.

Vyakulya vya Mngoni

Ugali: Chakulya cha kawaida cha mngoni ni ugali. Uvi ugali wa malombi, ugali wa mayawu gakondowoli au bundura. Uvi ugali wungi wa ulehi na ugali wa mapemba.
Wali: Kuna sambali zamahele za mpunga, ngita lingwindimba, kula na bwana, faya, bungare, sindano nk.
Ugali ama wali vilyelela likolo ngita, nyama, likolo la manyahi, ngowani, ngundi, chipele, mangatungu, chikandi, chimbondi, mawungu, madede, mbeleveta nk.
Ugali vibakulila mchiheneku au mulupalu na likolo vibakulila mu mkere. Vilya ugali kwa mawoko au kwa lukorombi. Vyakula vingi nde ngita mdojolela, mbatata, vingovi, maboga makumbu, nk.

Naona niishia hapa kwa leo mmmmhhh roho yangu imefurahi kuandika hapa ni kama nimeongea na mtu ana kwa ana. Raha jipe mwenyewe mwaya.

Wednesday, November 11, 2009

POLE KWA MSIBA DA MDOGO KOERO MKUNDI

Nimetoka kazini nimerudi nyumbani, baada ya muda nafungua computer na nasoma ujumbe wenye kicha cha habari NIMEFIWA kutoka kwa da mdogo Koero Mkundi usemao hivi:-
DADA KUNA MAPOROMOKO YA MLIMA YAMETOKEA HUKO UPARENI KIJIJINI KWA MAMA YETU NA KUNA WATU ZAIDI YA 20 WAMEPOTEZA MAISHA MIONGONI MWAO KUNA NDUGU ZAKE MAMA YAANI SHANGAZI YAKE NA WATOTO WAO NA MJOMBA PIA WAMEKUFA, HIVYO KESHO NASAFIRI NA MAMA KWENDA UPARENI KUHANI KWANI WAMEZIKWA LEO HII...... WOTE TUKO HAPA NYUMBANI TUNAOMBOLEZA...........ILA BIBI KOERO NI MZIMA TEGEMEO LANGU. Habari zaidi soma hapa.

JE UPWEKE NI UGONJWA?/ UPWEKE

Wapendwa posti iitwayo JE UPWEKE NI UGONJWA hii niliandika 27/8/2009 naomba kama hukusoma basi ipitie ndo utajua kwa nini nimeweka shairi hili la kaka Fadhy Mtanga.

Upweke

Upweke jama adhabu, upweke unasumbua,
Upweke ni maghilibu, kukufanya kuugua,
Watamani wa karibu, nenolo taelijua,
Upweke.

Upweke hutesa sana, umpendaye awe mbali,
Utamuwazia sana, hata mara alfu mbili,
Kwa usiku na mchana, maumivu ni makali,
Upweke.

Upweke unakondesha, chakula hukitamani,
Upweke unahenyesha, simanzi tele moyoni,
Homa pia hupandisha, na mwokozi humuoni,
Upweke.

Upweke tele mateso, hata machozi kulia,
Moyoni ni manyanyaso, nao moyo kuumia,
Wala si kimasomaso, kwani huleta udhia,
Upweke.

Upweke ni kama jela, huleta nyingi simanzi,
Huwezi hata kulala, maisha tele majonzi,
Utapiga hata sala, uruke vyote viunzi,
Upweke.

Upweke sawa na shimo, mtu ukatumbukia,
Nako shimoni uwamo, wateswa nayo dunia,
Kwani hauna makamo, kuweza kuvumilia,
Upweke.

Tuesday, November 10, 2009

UJUMBE KUTOKA SWEDEN KWA KAKA LAURENT KINUNDA

Kaka Laurent Kinunda.
Katika ukuaji wangu/akili yangu nilikuwa nafikiri ya kwamba ndugu ni yule mliyezaliwa mama mmoja na baba mmoja. Lakini kumbe nilikuwa na mawazo finyu. Ndugu ni mtu yeyote yule sio TU yule mliozaliwa tumbo moja.

Ilikuwa mwaka 1993 nilipokutana kwa mara ya kwanza na kaka LAURENT KINUNDA. Kaka Laurent, napenda kukushukuru kwa moyo ulio nao, wema wako na upendo wako. Umekuwa karibu sana nasi. Umekuwa huna kinyongo na familia yangu mara kunapotokea shida pia kunapokuwa na raha unakuwa nasi.

Nakumbuka kila tujapo TZ, hakuna mwingine anayekuja kutulaki uwanja wa ndege, isipokuwa ni wewe kaka Kinunda. Kwa hili napenda kutoa shukrani zangu/zetu za dhati. Umekuwa nasi katika matukio mbalimbali na umetusaidia na unatusaidia mambo mengi ambayo siwezi kuyahesabu hapa. Ninachoweza kusema. NAOMBA MWENYEZI MUNGU AKULINDE WEWE NA FAMILIA YAKO MUWE NA AFYA NJEMA NA MAISHA MEMA. TUNAWAPENDA WOTE. UPENDO DAIMA.

Monday, November 9, 2009

TUJIVUNIE LUGHA YETU NZURI KISWAHILI



Dada Sarah Hilwat mtalii wa kibelgiji aliyekipenda kiswahili na maisha ya waswahili baada ya kutembelea Lamu, Kenya kwa masomo. Sasa anakichapa kwelikweli!

VECKANS GÅTA= FUMBO LA WIKI HII

KISWIDI;-
Vad är det som har fyra ben på morgonen,
Två ben på dagen och tre ben på kvällen?

KISWAHILI:-
Ni nini ambacho kina miguu mnne asubuhi,
Miguu miwili mchana na miguu mitatu jioni?

Je? Jibu lake ni nini?

Saturday, November 7, 2009

MAISHA NI KURIDHIKA NA ULICHONACHO!!!!

Hapa ni mimi na mume wangu wakati ni kikongwe!

Sio lazima kuendesha Mercedes, Land Rove, X6 au Hummaer ili kujiona wa maana. Watu wenye furaha sio muhimu kuwa na kila kitu kizuri. Tufurahie kile (kitu )tulichonacho.
!!!!!!!!JUMAMOSI NJEMA JAMANI!!!!!

Thursday, November 5, 2009

DAWA YA MAPENZI.......... HADITHI.!!!!!

Palitokea Mwanamke, aliyekuwa ametolewa, akashindwa kuishi vizuri na mumewe. Kwa hivyo mumewe hakuridhika naye akaamua atafute mwanamke atayemfaa zaidi, aishi naye. Kwa wivu, yule mke wa kwanza, akatafuta dawa ya kuweza kumrudisha mume wake. Akatafuta dawa aina nne. Aina ya kwanza, ilikuwa ya kujipaka mwilini, aina ya pili, ya kutilia yule mawanaume kwenye chakula, aina ya tatu, ilikuwa ya kuoganayo, aina ya nne, ilikuwa ya kuchoma kwa moto. Hizo dawa aliamini zitamfanya mume wake, amwache mke wa pili, na kwamba mapenzi yao yataongezeka, kwa hivyo wataishi pamoja tena. Baada ya kuzipata dawa hizo na kuzitumia kikamilifu, bado hali ikawa ile ile, hakuna lililobadilika. Mumewe akaendelea kuishi na mkewe wa pili.

Yule mke wa kwanza, akaenda kwa bibi kizeemmoja ambaye alisifiwa kuwa mganga hodari akamwomba amsaidie. Bibi kizee hakusita akamwambia akatafute ubongo wa Fisi, yaani akamuue Fisi ampasue na kuuleta ubongo ukiwa bado mzima! Ubongo huo, ndio utatumika kutengenezea dawa ya mapenzi.

Mwanamke akarudi nyumbani akaanza kufikiria jinsi atakavyomtega Fisi na kumuua. Akapata wazo la kununua nyama na kuikata vipande, kuviweka njiani ambapo fisi hupendelea kupita mara kwa mara. Kesho yake akakuta ule mtego mtupu, na nyama imeliwa. Akanunua nyama kwa wingi akaiweka toka pale alipotega jana yake njiani pote mpaka nyumbani kwake. Fisi walipofika, kwa uroho na ujinga wao kana tunavyowafahamu, wakaanza jula vile vipande vya nyama mpaka ndani ya nyumba ya yule mwanamke. Akamkuta yule mwanamama amejitayarisha vizuri na shoka. Kwa nguvu zake zote. Akampiga kipigo kimoja tu na yule Fisi akafa hapo hapo. Akampasua kicwani akatoa ubongo, na akaenda nao kwa bibi kizee mganga.

Alipofika, bibi kizee akauliza: “Mwanangu, umeniletea ile dawa niliyokutumia?” Mwanamama akajibu. “Ndiyo mama, lakini nimeipata kwa shida sana!” Akamkabidhi bibi kizee ule ubongo wa Fidi. Alipokwisha upokea akakaa kitako akafikiri sana. Halafu akasema: “Mwanangu, sasa nitakueleza kila kitu vizuri sana umetumie akili na ujuzi mwingi, kutega Fisi na kumwua. Sasa nenda ukatumie akili na ujuzi wako wotw ulionao, ili uweze kupata mapenzi ya mumeo, ili uweze kupata mapenzi ya mumeo tena. Nina maanisha kusema, lazima uwe msafi, uvae vizuri na upikie chakula kizuri mume wako. Vile vile, jaribu kujipendezesha kwa mume wako kwa kila hali. Utaona mumeo anarudi nyumbani na kumuacha mke aliyekuwa naye sasa hivi, na mataishi kwa amani na furaha.

Aliporudi nyumbani, akafanya, yote aliyoambiwa na yule bibi kizee. Haukupita muda, mumewe akamfukuza mke wa pili na akarudi nyumbani kwa mke wake wa kwanza. Wakaishi vyema kwa mika mingi sana mpaka vifo vikawatengenisha.

FUNDISHO:- Inaaminika kuwa, watu wanapoishindwa kuishi pamoja katika ndoa, hutumia dawa za kienyeji kwa sababu ya kusitawisha maisha yao.

Wapo akian mama wengi amabao wanaamini kabisa kwamba kuna dawa ya mapenzi.
Lakini ukweli ni kwamba, dawa ya mapenzi ni moja tu nayo ni: Kuhakikisha kwamba, kina mama wanaheshimu ndoa zao na kutii waume zao. Nyumba yenye mapenzi, inamfanya mume apende kukaa nyumbani, na asitembee tembee ovyo.

Nimeitoa katika kitabu cha HADITHI na visa kutoka Tanzania.

Wednesday, November 4, 2009

KARIBUNI KANDA YA KUSINI TUCHEZE MGANDA-RUVUMA/SONGEA



Kama unatamani nyumbani fanya kama mimi sikiliza ngoma za asili na ikibidi cheza pia, haya karibu tuungane kwa ngoma hii ya mganda.

MWANAUME WA MIAKA 112 AMUOA BINTI WA MIAKA 17

Umri ni namba tu!!
Mamia ya watu walihudhuria sherehe za harusi ya mzee Ahmed Muhamed Dore mwenye miaka 112 akiaoana na binti aitwaye Safia Adulleh mwenye miaka 17.
“Leo Mungu ameniwezesha kufikia ndoto yangu” alisema mzee Ahmed Muhamed Dore baada ya kuoana na binti mbichi kabisa kutoka maeneo ya Galguud huko katikati ya Somalia.

Mambo yanayovutia kuhusu hii ndoa
Wanafamilia wa binti wanasema binti yao amefurahi kupata mume.
Bwana harusi alikuwa anasubiri kwa karibu zaidi binti aendelea kukua hadi amshauri waoane bila kumlazimisha bali kumvutia kwa upendo ili waoane.
Ni ndoa ya aina yake kwenye eneo ya Horn of Africa kwa babu miaka 112 kuoana na binti wa miaka 17.
Wapo watu ambao hawaridhiki na tofauti ya umri ingawa katika sheria za kiislamu inaruhusiwa.
Wapo waliofurahi na kukiri kwamba umri si kizuizi linapokuja suala la ndoa na kupendana.
Bwana harusi tayari ana watoto na wajukuu 114 huku kijana wake wa kwanza akiwa na miaka 80.
Bado anaamini huyu mke mpya ataendelea kumzalia watoto.
Zaidi anakiri kwamba ni Baraka sana kuwa na mtu unayempenda na akaendelea kukutunza.

Soma zaidi BBC

Tuesday, November 3, 2009

KITABU CHA MAISHA NA MAFANIKIO......

SEHEMU YA PILI...................

Huwezi kuwa kamili bila mwingine kukamilika

Sisi kama binadamu tunajipenda na hakuna awezaye kulizuia jambo hili. Lakini kujipenda kwa ziada kunaweza kuzuilika kama mtu ataamua. Kujipenda kwa ziada ndiko ambako kunapelekea dunia kuwa kama ilivyo leo kwa upande wa uharibifu. Yale yote ambayo hayakwenda sawa kufuatana na mpango wa Mungu yamesababishwa na uziada wa kujipenda kwa binadamu, Mpango wa Mungu ni kuwa na dunia ambayo haina makovu wala vidonda. Lakini dunia hii tunamoishi imejaa vidonda na makovu zaidi kuliko uzima. Vidonda na makovu haya, kama ambavyo tumesema ni matokeo ya binadamu kujipenda kupita kiasi, kujipenda ambako kunamfanya adhani kwamba yeye anastahili zaidi kuliko mwingine na kumfanya awe pia mvivu wa kufikiri.

Ni binadamu wachache sana ambao wako tayari kukaa chini na kujiuliza kama kweli wana tofauti na wengine. Ni wachache kwa sababu kila mmoja anaamini kwamba ni taofauti na mweingine, iwe ni kwa mwenye mali au asio nayo, iwe ni kwa mwanamke au mwanaume, au kwa msomi au asiyesoma, kila mmoja anaamini kwamba ana tofauti na mwingine. Anashindwa binadamu kujua kwamba, yeye kama binadamu hana tofauti na binadamu mwingine.

Labda tukumbushane kwamba binadamu hawi binadamu kwa sababu ana magari makubwa mia moja au ana nyumba za fahari mji mzima, lakini pia hawi binadamu kwasababu anashinda na kulala na njaa au anatembea makalio yakiwa nje kwa ulitima (Umaskini). Binadamu anakuwa binadamu kwa sababu kuna sifa ambazo hupatikana kwake na kwa mwingine bila kujali huyo mwingine yukoje kimwili na kihali.

Kushindwa huku ndiko ambako huwafanya binadamu kuwapa wenzao kile ambacho kama wengepewa wao kungezuka balaa kubwa. Binadamu wamekuwa wakijaribu kuridhisha miili yao na pengine nafsi kama siyo tamaa zao kwa kuwafanyia wengine lile ambalo kwao lingekuwa ni gumu sana kulivumilia.

Leo hii kuna binadamu ambao kwa kujali fedha wanauza sumu kwa binadamu wenzao. Kwa kutaka fedha huuza vyakula ambavyo wanajua wazi kwamba, vitawashuru afya za wengine na kuwauwa. Wanauza vyakula hivyo wakiwa na uhakika kwamb, baada ya muda fulani, hao waliouziwa wataugua kansa au maradhi mengine hadi kufa. Lakini ni wazi wao wasingekubali kufanyiwa jambo hilo.

Kuna wale ambao kwa matumizi ya vyeo vyao huwakosesha wengine haki zao kwa sababu tu wengine hao hawana nguvu na uwezo wa kupambana nao. Hawa kwa makusudi huwafanya watu wengi kuishi katika ulitima wa kudumu wakati wangeweza kuinuka na kuishi kama wao.

Kuna kundi kubwa la binadamu ambalo kamwe halijawahi kufanya jema kwa wengine, halijawahi kutamka jema kwa wengine na halijawahi kufikiria jema kwa wengine. Kundi hili lina watu ambao wao kila siku wanafikiria ni kwa namna gani watatumia ujinga wa wengine kwa manufaa yao, ujinga wa wengine kwa kujupatia ziada na “kutanua” huku wengine hao wakiporomoka na kuingia kwenye shimo la kiza cha ukosefu na majuto.

Umefika wakati ambapo inabidi tuanze kuhushimu nguvu za maumbile, inabidi tuanze kuhushimu ubinadamu katika ujumla wake. Inabidi tujue kwamba kinachotufanya tusimame leo na kujidai, kujuvuna na kujiona tu bora sana ni kwa sababu kuna banadamu wengine wanaotuzunguka. Kinachotufanya leo hii tutamani kuonekana wakubwa zaidi, wenye uwezo zaidi na wenye heshima zaidi ni kuwepo kwa binadamu hata kidogo kama tunavyodhani, bila binadamu wengine kuwepo.

Mbaya zaidi ni kwamba, sisi siyo binadamu kamili kama wenzetu siyo kamili. Ukamilifu wao ndiyo unatupa sisi ukamilifu. Ukitaka kuthibitisha jambo hili unaweza, kwani ni rahisi sana. Hebu anza sasa kutenda yale ambayo hata wewe ungependa kutendewa na kuacha kuwatenda wengine yale ambayo hata wewe usingependa kutendwa. Tuna uhakika baada ya muda fulani utagundua ukweli fulani na bila shaka utawasiliana nasi kutufahamisha. Hutapoteza chochote kufanya jaribio hilo bila shaka.
MWISHO.......
Makala hii nimeichukua kutoka kwenye kitabu cha Maisha na Mafanikio kilichoandikwa na Hayati Munga Tehenan ambaye alikuwa ni Mwalimu mzuri wa maarifa ya Utambuzi akitoa elimu hiyo kupitia magazeti yake ya Jitambue, vitabu na semina zake nchini Tanzania kabla ya kufariki dunia.

Monday, November 2, 2009

KITABU CHA MAISHA NA MAFANIKIO......

SEHEMU YA KWANZA...........

Kila binadamu anajipenda, ingawa wengine hujipenda zaidi kiasi kwamba hujiona wao wenyewe tu, kama kwamba wako peke yao hapa duniani. Kwa kujipenda kwao sana, wengi huingia mahali ambapo huamini kuwa matatizo na shida zao maishani ni matokeo ya wale wanaowaita adui zao wa aina mbalimbali. Kwa kujipenda kwao zaidi husahau kabisa kwamba bila wengine kuwepo na kukamilika, wao pia siyo kamili. Mada hii inaelezea namna ambavyo adui wa watu wengi ni watu hao wenyewe na siyo wengine na inafafanua kuhusu ukamilifu wa binadamu usivyowezekana pale ambapo wengine hawajakamilika.

Mbu anapokuuma utapata malaria huwa unahesabu kama adui yako. Unaweza kutangaza kwa maringo na kujivuna kwamba uko kwenye kampeni ya kumuangamiza adui mbu ili uondokane na adha ya malaria. Lakini je, ni kweli mbu ndiye adui yako?

Siku hizi kuna virusi vya HIV ambavyo vinahesabiwa kama maadui wa watu wote. Kila kona hapa duniani kuna juhudi za kila aina katika kupambana na virusi hivi. Ukimuuliza mtu atakwambia, virusi hawa ndiyo adui zetu katika suala la maradhi haya, lakini je, kuna ukweli wowote katika hili? Kila mtu anafahamu vizuri mazingira ya aina mbalimbali ambao kwake huyaita adui, kila mtu anawafahamu watu wa aina mbalimbali kwake kwa sababu mbalimbali anawaita adui zake na kila mtu anafahamu vizuri vitu fulani maalum ambavyo kwa sababu fulani anaviita na kuamini kwamba ni adui zake.

Lakini huenda hakuna ambaye anajua ni kiasi gani tabia, mienendo na mawazo yake ni adui zake wakubwa. Ni mara chache sana na ni watu wachache sana ambao wako tayari kujiuliza na kukiri kwamba, tabia mienendo na mawazo yao kwa kiasi kikubwa sana huwa vinawadhuru na kuwaumiza, kuwaharibia mipango yao na maisha kwa ujumla, kuliko wanavyodhani kwamba athari hizo hutoka nje yao.

Ni wachache kwa sababu, binadamu hujipenda sana kiasi ambacho huogopakufunua macho zaidi na kuukabili udhaifu alionao. Ukweli ni kwamba, kama mtu atataka kuishi bila kujidanganya, atagundua kuwa hata mbu na virusi wa ukimwa siyo adui zetu atagundua kuwa kwamba, tabia mienendo na mawazo yetu ndiyo adui zetu. Kama mtu ataamua kujikinga dhidi ya mambo yote yanayoweza kumwambukiza virusi wa ukimwi au kuishi katika mazingira ya mbu wengi na kuchukua tahadhari dhidi ya wadudu hao, anakuwa amemkwepa kwa karibu asilimia tisini huyu au hawa anaowaita adui zake.

Kila siku, hata pale ambapo tunatangaza kamba akina fulani ni adui zetu, huwa tunafanya hivyo kwa makosa kwa sababu tu ya kujipenda na hivyo kujipendelea katika kuutazama ukweli. Tunapofilisika tunajitahidi sana kutafuta maadui wa hali hiyo, huku tukiwa tumesahau kwamba tabia zetu ndizo zinazotufilisi. Tunaposhindwa kupata tunachokitafuta maishani, hatuzitazami tabia, mitazamo,mienendo, imani na mawazo yetu, bali tunatazama nje yetu ili kumpata adui. Ilivyo ni kwamba, kama tunatafuta adui, kwa sababu tunataka kumpata ni lazima tutampata. Hivyo tukishampata tutaamini kabisa kwamba huyu ni adui yetu na kuziweka nguvu zetu hapo kujaribu kupambana naye.

Inachukua muda, na wakati huo tunakuwa tumechelewa sana tunapokuja kugundua kwamba tuliyemdhani ni adui alikuwa ndani mwetu. Lakini kwa bahati mbaya sana ni kwamba huwa hatufanikiwi kungámua kwamba huyu tunadhani ni adui yetu siyo adui yetu. Kwa hali hiyo, huwa tunaishi katika katika dhiki, misukosuko na nuksi zisizokwisha tukijaribu kupambana na adui ambaye siye, huku adui yetu akiwa ni sisi wenyewe. Kupigana huku na adui asiyekuwepo popote bali ndani mwetu huweza hata kutupotezea maisha yetu. Kwa nini basi kabla hatujatangaza au kudhani fulani ndiye adui yetu, tusitazame au kuzigundua kwanza tabia zetu, mienendo, imani, na mawazo yetu? Wanasema wataalamu wa nyanja zote za kimaisha katika nadharia zao nyingi kuhusu maisha kwamba, adui wa mtu ni mtu mwenyewe. Tulitafakari hilo kwa makini.

Tusipolitazama kwa makini tutajikuta kila siku tukizidi kuongeza idadi ya maadui huku hali zetu kielimu, kiuchumi na kijamii kwa ujumla zikizidi kudorora. Zitazidi kudorora kwa sababu yule tunayemdhani ni adui yetu atatupitezea muda wetu na kutusumbua sana, wakati adui yetu tunaye ndani mwetu na tunaweza kumuondoa kwa saa kadhaa tu kama tutamgundua.

Kwa nini huwa ni vigumu kwetu kmjua au kumgundua adui yetu pale mambo yetu yanaposhindwa kwenda kama tulivyotarajia au kutaka? Ni kwa sababu tumefundishwa na mazoea kwamba sisi ni vitu vilivyo nje yetu na hivyo, kusimama au kuanguka katika maisha yetu hutegemea wengine na mazingira ya nje yetu. Tunapopata fedha na kuzitumia vibaya, hatujikagui na kujiuliza kama chanzo cha kufikia hatua hiyo siyo sisi wenyewe, bali tunaanza kuwaambia wake zetu kwamba wana nuksi au kuwasingizia jirani zetu kwamba wametuendea kwa waganga kutuharibia bahati zetu.

Tunapotoka nje kwenye ndoa zetu na kufanya uzinzi, hatuko tayari kujikagua ili kuuona ukweli, bali tunachoweza kufanya ni kuwasingizia wake au waume zetu kwamba wao ndiyo chanzo kwa sababu hawatujali, kwa sababu ni dhaifu wa tendo la ndoa au kwa sababu hawana fedha. Ni vigumu kwetu kujiuliza kama sisi siyo chanzo au kujiuliza mchango wetu kwenye suala zima. Tunajipenda sana na kuamini kwamba sisi ni watu nav itu vinavyotuzunguka.

Tunapopoteza kazi zetu hatujikagui kama sisi wenyewe hatukuchangia kufukuzwa huko, kwani adui zetu siku zote wako nje yetu na ni lazima tutawatafuta. Tunaweza kumnyooshea kidole cha lawama bosi wetu au walio chini yetu, tunaweza kudai kwamba ni jirani au ndugu zetu ambao ati siku zote hawakuwa wakifurahia mafanikio yetu. Ndiyo ubaya wa kujipenda na kuamini kwamba adui zetu wako nje yetu na ni lazima kila linalokwenda kinyume na matarajio yetu liwe limesababishwa na watu hao au mazingira hayo. Umefika wakati ambapo inabidi tubadilike sana na kuanza kuujua ukweli kwamba sisi ndiyo waamuzi na waendeshaji wa maisha yetu.Kila linalotutokea ni matokeo ya tabia, mienendo na mawazo yetu.

Makala hii nimeichukua kutoka kwenye kitabu cha Maisha na Mafanikio kilichoandikwa na Hayati Munga Tehenan ambaye alikuwa ni Mwalimu mzuri wa maarifa ya Utambuzi akitoa elimu hiyo kupitia magazeti yake ya Jitambue, vitabu na semina zake nchini Tanzania kabla ya kufariki dunia.

ITAENDELEA...............